Thursday, May 28, 2015

KILIMO CHA MILIMANI IRINGA BASI




Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Serikali ya mkoa wa Iringa imepiga marufuku uharibifu wa vyanzo vya maji na kilimo maeneo ya vyanzo vya maji.

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Kilolo, Bw. Selemani Mzee aliyemuwakilisha mkuu wa mkoa wa Iringa, Bibi. Amina Masenza katika hafta fupi ya makabidhiano ya mradi wa maji wa Ismani na vifaa, tukio lililofanyika katika kiteka maji katika kijijini Mbigili wilaya ya Kilolo.

Bw. Mzee amesema “halmashauri zote za wilaya ya Kilolo na Iringa lazima zihakikishe zinatunza, kuhimiza na kusimamia utunzaji wa vyanzo vya maji ili viwe endelevu”.  Wale wote wanaolima maeneo ya milimani na kuharibu na kutishia uharibifu wa vyanzo vya maji lazima waondolewe, alisisitiza Bw. Mzee. 

Amesema kuwa mradi wa maji Ismani unahudumia vijiji 25 na una uwezo wa kuhudumia zaidi ya vijiji hivyo na kuwataka wananchi kuutunza na kuulinda mradi huo. Aidha, ameitaka jumuiya ya watumia maji Ismani na Kilolo kuusimamia vizuri mradi huo kwa kufanya ukarabati wa mara kwa mara uharibifu unapotokea. Ameongeza kuwa wananchi lazima wachangie mita ili kujihakikishia uendelevu wa mradi na upatikanaji wa maji.

Katika taarifa fupi ya mradi wa maji wa Ismani kwa mgeni rasmi iliyowasilishwa na Mhandisi wa Maji wa Mkoa wa Iringa, Mhandisi Shaban Jellan amevitaja vijiji vinavyohudumiwa na skimu hiyo kuwa ni 25 na kuongeza kuwa vijiji vinne vipo katika Halmashauri ya wilaya ya Kilolo na vijiji 21 vipo katika Halmashauri ya wilaya ya Iringa. Watu wanaohudumiwa na skimu hiyo ni zaidi ya 42,957.

Akiongelea hali ya upatikanaji wa maji katika vijiji 25 vya mradi wa maji wa Ismani, Mhandisi Jellan amesema “mradi huu umeendelea kuwa tegemeo kubwa la maji kwa vijiji vyote 25, kuharibika kwa mara kwa mara na ongezeko la watu na mifugo kuna sababisha upatikanaji wa maji kutokuwa kwa uhakika”. Amesema kuwa vijiji vya mwanzo vimekuwa vikiongeza matumizi ya maji na kuanzisha matumizi ambayo hayakutegemewa kama umwagiliaji maji katika bustani na kusababisha baadhi ya vijiji kuanza migogoro ya kugombea maji na kuharibu miundombinu ya kupitishia maji ili maji yamwagike katika maeneo yao. Ameongeza kuwa kutokana na uharibifu huo vijiji vya mbali katika Kata za Kihorogota na Malengamakali vimeathirika zaidi na kuwa na uhaba mkubwa wa maji wakati wa kiangazi. 

Msimamizi wa mradi wa Maji Ismani, Bw. Edoardo Chiappa, aliwashukuru wananchi wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika ukarabati wa mradi wa maji wa Ismani na kusema kuwa wamewasaidia sana na kufanya kazi yao kuwa nyepesi. Amesema kuwa mradi huo ulikuwa na lengo la kuhakikisha wananchi walio katika eneo la mradi wananufaika na huduma hiyo ya maji. Amesema kuwa wamefanikiwa kuanzisha kamati 24 za maji vijijini na kutoa mafunzo kwa vijiji 24 juu ya ukusanyaji wa mapato ya maji. Kazi nyingine ameitaja kuwa ni uhamasishaji kwa shule 21, mikutano ya hadhara 55 na kutembelea zaidi ya makazi 2,822 kuelimisha umuhimu wa utunzaji miundombinu ya maji.

Mradi wa maji wa Ismani unaohudumia vijiji 25 ulianza kujengwa kwa mara ya kwanza miaka ya 60. Ukarabati mkubwa umefanywa kuanzia mwaka 2013 na serikali ya Italia kupitia shirika la Movimento per la Lotta contro la Fame nel Mondo, MLFM/ AVIS kwa gharama ya Tshs. Bilioni 4. Sehemu kubwa ya ukarabati ni ujenzi wa mtambo wa kutibu maji, ukarabati wa matanki ya kuhifadhi maji, ukarabati wa vituo vya kutekea maji, ukarabati wa mabomba, uchimbaji wa visima virefu 2 na uimarishaji wa jumuiya ya watumia maji ya Ismani.
=30=

No comments:

Post a Comment