Katibu Tawala Mkoa,
Wakurugenzi wa Halmashauri,
Viongozi wa Serikali na Taasisi mbalimbali
Waandishi wa Habari,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kujumuika na kushiriki kikamilifu
katika Siku ya Uzinduzi wa Wiki ya
Usafi wa Mazingira Kimkoa inayofanyika hapa kijiji cha Uhambingeto.
Napenda kutoa pongezi maalum kwa wananchi wa
Uhambingeto kwa kufika hapa kwa wingi kushiriki katika uzinduzi huu wa maadhimisho
haya kimkoa. Kufika kwenu ndiyo ufanisi wa shughuli hii na mafanikio yake.
Nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitawashukuru washirika wetu wa maendeleo kwa
michango na misaada yao adhimu. Marafiki zetu wametuunga mkono katika juhudi
zetu za kuboresha huduma za usafi wa mazingira mijini na vijijini. Ninawaomba,
wawakilishi wa mashirika waliopo hapa, wazipokee na kuzifikisha shukrani zetu
za dhati, kwa wakuu wa mashirika yao.
|
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza |
Umuhimu wa
Maadhimisho
Ndugu Wananchi;
Maadhimisho ya Siku ya kunawa mikono Duniani,
Siku ya choo Duniani na wiki ya Usafi Tanzania, ambayo yameanza rasmi mwaka
2013, ni ushahidi wa umuhimu ambao Serikali na wananchi wanaoutoa katika
kuboresha usafi wa mazingira nchini. Kwa miaka mingi tarehe 19 Novemba dunia imekuwa ikiadhimisha
siku ya choo
duniani na 15 oktoba siku ya kunawa mikono kwa sabuni Duniani. Mwaka 2013 Umoja
wa Mataifa ulipitisha tarehe 19 Novemba kuwa ni siku rasmi ya maadhimisho ya
Choo Duniani kutokana na ukweli kuwa kati ya malengo yote ya maendeleo ya
milenia ndio lengo pekee ambalo liko nyuma kiutekelezaji. Katika mwaka huo huo
Tanzania ilipitisha rasmi wiki ya tarehe 13 hadi 19 Novemba kuwa ni wiki ya
Usafi Tanzania. Tanzania huadhimisha kwa pamoja katika wiki hii Siku ya Kunawa
Mikono Duniani na Siku ya Choo Duniani. Kwa mwaka huu Maadhimisho haya Kitaifa
yanafanyika Mkoani Njombe.
Lengo kuu la maadhimisho haya ni kuhamasisha
jamii ili iweze kuchukua hatua katika kukabiliana na changamoto za kukosa
huduma za choo bora na uboreshaji wa usafi wa mazingira kwa ujumla, ambapo
mkazo huwekwa katika uhamasishaji wa matumizi ya vyoo bora, unawaji wa mikono
kwa sabuni, njia sahihi za kutibu na kutunza maji ya kunywa majumbani, na
usafishaji wa maeneo yanayotuzunguka.
Maadhimisho haya pia yanatoa nafasi kwa wadau
kujadili mafanikio yaliyopatikana na matatizo yaliyopo katika kuendeleza usafi
wa mazingira ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyoo bora na kuyatafutia ufumbuzi.
Kwa pamoja, kama taifa, tunapata fursa ya kufanya tathmini ya tulikotoka,
tulipo sasa na kuainisha malengo na mipango yetu kwa siku zijazo.
Kauli Mbiu ya Maadhimisho
Ndugu Wananchi; Kauli mbiu ya Maadhimisho
ya mwaka huu ina ujumbe mzito sana: Kipindupindu Hakikubaliki, Zuia Maambukizi Mapya, Zingatia
Usafi wa Mazingira”. Ni ukweli ulio wazi kuwa bila kuchukua jitihada za
makusudi za kuboresha usafi wa mazingira yetu janga hili la kipindupindu litaendelea
kuwepo na watu wataoendelea kupoteza maisha na kupunguza nguvu kazi.
Kwa kutambua ukweli
huo kuhusu usafi wa mazingira, katika siku ya leo na katika wiki yote hii
tafakuri zetu tuzielekeze kwenye kutafuta mikakati na mbinu za kuhakikisha kuwa
tunaboresha usafi wa mazingira katika maeneo yetu. Naomba tutambue kuwa mkakati
wowote kwa ajili hiyo hauna budi ujielekeze katika kufanya mambo yafuatayo:
1.
Kujenga vyoo bora na kuvitumia
2.
Kunawa mikono kwa maji safi na sabuni katika nyakati tano
muhimu,
3.
Kusafisha maeneo yanayotuzunguka,
4.
Kuboresha usafi binafsi na kuaacha tabia ya kutupa taka ovyo.
Ndugu Wananchi;
Huduma duni za
usafi wa mazingira zinachangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa milipuko ya
magonjwa ya kuhara ikiwemo kipindupindu na kusababisha vifo ambavyo vingeweza
kuzuilika. Katika mlipuko wa Kipindupindu unaoendelea nchini takriban watu 106
wameshapoteza maisha. Idadi hii ni
kubwa na pengo kubwa kwa familia zao na Taifa kwa ujumla.
Aidha, Kwa mujibu wa Shirika la UNICEF na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
Ugonjwa wa kuhara bado ni miongoni mwa magonjwa makuu matano yanayochangia
katika vifo kwa watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano nchini Tanzania.
Takwimu zinaonyesha kwamba moja ya tatu ya vifo vya watoto vinavyotokea ndani
ya mwezi wa kwanza wa maisha ya watoto vinatokana na maambukizi au magonjwa ya
kuhara yanayosababishwa na:
·
Ukosefu wa maji safi na salama,
·
Mazingira machafu na kutozingatia tabia za usafi.
·
Madhara mengine yatokanayo na ukosefu wa maji safi na salama,
·
Mazingira machafu na kutozingatia tabia za usafi ni kudumaa (mtoto kuwa na
kimo kifupi kisichoendana na umri na kuathiri ukuaji)
Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 53 ya watoto chini ya miaka mitano mkoani
Iringa wamedumaa.
Kunawa mikono kwa sabuni ni mojawapo ya njia rahisi na yenye gharama nafuu
kuzuia maambukizi. Njia hii hupunguza uwezekano wa kupata maambukizi kwa 50% na
matumizi ya choo bora hupunguza kwa 32%. Takwimu za utafiti uliofanywa na
shirika la UNICEF katika mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya zinaonyesha kuwa kaya
zenye vyoo bora ni 23%, kaya ambazo zina vyombo vya kunawia mikono na sabuni ni
9%, uoshaji wa mikono baada ya kumhudumia mtoto ni 56%, uoshaji wa mikono kabla
ya kuandaa chakula ni 2% na uoshaji wa mikono kabla ya kumlisha mtoto ni 18%.
Ndugu Wananchi;
Uboreshaji wa usafi wa mazingira na kuzingatia
kanuni zake ndio ngao pekee ya kujikinga na janga hili kubwa la ugonjwa wa
kipindupindu.
Hatua Zilizochukuliwa na Serikali kukabiliana na changamoto
Ndugu Wananchi;
Baadhi ya jitihada zinazofanywa na Serikali kukabili changamoto za usafi wa
mazingira nchini ni:
(i) Utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Usafi wa Mazingira ambayo inalenga
kuongeza idadi ya watu wenye vyoo bora na kuboresha usafi wa mazingira katika
maeneo ya mikusanyiko, maeneo ya barabara kuu na kwenye Taasisi. Kwa mkoa wa
Iringa kupitia Kampeni hii jumla ya mafundi 156 kutoka vijiji 156 wamefundishwa
jinsi ya kujenga vyoo bora kwa gharama nafuu. Nawaomba tuwatumie mafundi hawa
ili tuweze kujenga vyoo bora vijijini kwetu.
Nimesikia kuwa Mkoa wa Iringa tayari kuna kata
33 zinatekeleza Kampeni hii, naomba Wakurugenzi wa Halmashauri wapanue
utekelezaji huu katika kata nyengine kwa kutumia vyanzo vya ndani vya mapato.
Aidha, utekelezaji wa Kampeni hii kwa mkoa wetu hauridhishi kulingana na
malengo kama tulivyosikia katika Taarifa ya Mganga Mkuu wa Mkoa. Hivyo
nawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kila Halmashauri inafikia
malengo kwa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Kampeni hii na kuwachukulia
hatua watendaji wasio wajibika. Katika
utekelezaji wa Kampeni hii ili mwisho wa siku kila wananchi awe na Choo bora.
(ii) Kusimamia sheria zilizopo za usafi wa
mazingira na kuwachukulia hatua wale wote wanaoenda kinyume na sheria hizi
zikiwemo sheria ndogo za Halmashauri na vijiji.
Hivyo nachukua nafasi hii kuaagiza Wakurugenzi
wa Halmashauri kusimamia kikamilifu Sheria hizo ikiwa ni pamoja na kuwachukulia
hatua wale wote watakaokiuka na kuifanya Kampeni hii isifanikiwe.
Ndugu Wananchi;
Usafi wa Mazingira ni jukumu letu sote , na ni jukumu endelevu rai
yangu kwenu ni kuendelea kufanya usafi katika maeneo yote yanayotuzunguka na
kuhamasisha ujenzi na matumizi ya vyoo bora ya vyoo kwa afya ya kaya na Taifa
kwa ujumla. Lazima tuzingatie Kanuni
zote za Usafi kama tunavyoelekezwa na wataalamu wa Afya.
Baada ya kusema haya natamka kuwa uzinduzi wa maadhimisho siku
ya kunawa Mikono Duniani, Siku ya Choo Duniani, na wiki ya Usafi wa Mazingira
Tanzania imezinduliwa rasmi,
Aksanteni kwa kunisikiliza.
HAPA KAZI TU!!