Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wahanga wa mafuriko ya mto Mapogoro zaidi
ya 300 wametakiwa kuhama katika nyumba zao kutokana na kupata unyevu kiwango
cha kuhatarisha maisha yao.
Tahadhari hiyo ilitolewa na mkuu wa
mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipowatembelea wananchi wa Kijiji cha Mapogoro
katika Tarafa ya Idodi wilayani Iringa walioathiriwa na mafuriko yaliyosababishwa
na mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali wilayani Iringa.
Masenza alisema “nyumba zilizopata
unyevu kutokana na mafuriko ya maji muhame, sitaki kusikia mwananchi hata mmoja
amedondokewa na nyumba. Kutokana na nyumba nyingi kujengwa bila misingi na hata
zinazojengwa kwa misingi, misingi hiyo inakuwa si imara hivyo hatari ya
kudondoka nyumba inaweza kuwa kubwa katika kipindi hiki ambacho mvua
zinaendelea kunyesha”. Kwa tathmini ya haraka kaya 137 katika kitongoji cha
Kitanewa chenye wakazi zaidi ya 300 wanatakiwa kuhama ili kuepukana na kadhia
ya mafuriko.
Akiongelea sababu za mafuriko hayo,
Masenza alisema kuwa miongoni mwa visababishi ni uharibifu wa mazingira. Alisema
shughuli za kilimo pembezoni mwa kingo za mto na ukataji miti ovyo vinachangia
mafuriko ya mara kwa mara maeneo yasiyotarajiwa. Aliwataka waheshimiwa madiwani
na watendaji wa kata na vijiji kuwaelimisha wananchi dhidi ya athari ya
uharibifu wa mazingira.
Mkuu wa mkoa aliwataka wazazi na
wananchi kwa ujumja kuwalinda watoto dhidi ya hatari ya maji hayo. “Ndugu zangu
lazima muwe waangalifu kwa watoto wasiende kwenye maji na kusombwa nawaomba
sana” alisisitiza.
Mafuriko hayo yalisababisha maafa ya
kusombwa nyumba 14, hekari 717 katika vijiji vya Idodi, Mapogoro na Kitisi,
eneo la banio la maji katika mfereji Mapogoro limefunikwa na mchanga na sehemu
ya barabara kusombwa na maji na kusababisha magari ya upande mmoja kushindwa
kuvuka kuelekea upande wa pili. Aidha, meneja wa Tanroads mkoa wa Iringa,
mhandishi Daniel Kindole alisema kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha barabara
iliyomegwa na maji inakarabatiwa na kuendelea kupitika kama kawaida. Aliongeza kuwa
vifaa kazi zinaendelea kukusanywa ili kupelekwa eneo la tukio kurejesha hali ya
kawaida.
Uongozi wa wilaya, mkoa na shirika la
msalaba mwekundu wanaendelea ja jitihada za kutafuta mahema na chakula kwa
ajili ya kuwasaidia watu ambao nyumba zao zilizolewa na chakula chao kuharibiwa
na maji hayo.
=30=
No comments:
Post a Comment