Sunday, March 16, 2014

ONGEZEKO LA WATU IRINGA WAONGEZA MAHITAJI YA ARDHI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Ongezeko kubwa la idadi ya watu katika manispaa ya Iringa linaenda sambamba na ongezeko la shughuli kuichumi hatimae kusababisha kuongezeka kwa mahitaji na matumizi ya ardhi.
 
Afisa Mipango Miji wa Manispaa ya Iringa, Immaculate Senje
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Mipango Miji wa Manispaa ya Iringa, Immaculate Senje alipokuwa akiwasilisha mada ya Mpango kamambe wa mji wa Iringa (Iringa Master Plan) 2015-2035 katika mkutano wa wadau wa maandalizi ya Mpango Kamambe wa Mji wa Iringa uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari ya Lugalo.

Senje amelitaja ongezeko la idadi ya watu katika mji wa Iringa linaloenda sambamba na ongezeko la shughuli za kiuchumi linasababisha kuongezeka kwa mahitaji na tumizi ya ardhi. Amesema ili kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya matumizi ya ardhi upo umuhimu wa kuwa na mwongozo unaotoa dira ya ukuaji wa mji ambao ni endelevu.

Akiongelea matumizi ya ardhi, Afisa Mipango Miji wa Manispaa ya Iringa amesema kuwa mji wa Iringa kama ilivyo miji mingine nchini unayo maeneo ya makazi yaliyopangwa na kupimwa pamoja nay ale yanayoenelezwa kiholela. Amesema kuwa eneo la makazi lililopangwa wakati wa ukoloni liko katika makundi matatu ambayo ni ujazo wa chini, ujazo wa kati na ujazo wa juu.

Akiongelea maeneo ambayo yameendelezwa kiholela, ameyataja maeneo hayo kuwa yanapatikana katika kata za Mwangata, Ruaha, Mkwawa, Mtwivila, Kihesa na Nduli. Amesema kuwa yapo maeneo ya vijiji vilivyoingia katika Manispaa siku za karibuni kama Kigonzile, Nduli, Mgongo, Mkoga na kitongoji cha Ulonge kuwa yana makazi yaliyotawanyika.

Akielezea matarajio yake baada ya mkutano, Senje amesema kuwa masuala muhimu, kero na changamoto zinazowakabili wakazi wa Iringa zitaibuliwa na kuwa msingi mkuu utakaoongoza uandaaji wa Mpango Kamambe utakaokidhi mahitaji ya wakazi wa Manispaa ya Iringa.
=30=

SERIKALI KUTENGENEZA MASTER PLAN KWA KUSHIRIKISHA WADAU



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Serikali imedhamiria kuona mji wa Iringa unakuwa na kuwa na maendeleo endelevu kwa ustawi wa kwa kuandaa mipango shirikishi kwa wananchi.
 
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita
Kauli hiyoimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa wadau wa maandalizi ya mpango kamambe wa mji wa Iringa (Iringa Master Plan) iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita.

Dkt. Ishengoma amesema “lengo kuu la kuandaa mpango kamambe ni kuwezesha ukuaji wa mji ambao ni endelevu katika Nyanja za kiafya, usalama, mpangilio mzuri, muonekano mzuri na ustawi wa jamii”. Amesema kuwa katika kufanikisha mpango huo, ushirikishaji mipango iliyopita na inayoendelea ya kisera katika ngazi mbalimbali za utendaji utazingatiwa.

Mkuu wa Mkoa amesema kuwa mpango kamambe husimamia uendeshaji wa mji kwa muda wa miaka 20. Amesema kuwa mpango huo unaweza kufanyiwa mapitio baada ya miaka mitano (5). Akiongelea umuhimu wa mpango amesema kuwa mpango hutoa mwongozo wa matumizi mbalimbali kwa ujumla kulingana na mahitaji ya jamii husika. Ameyataja matumizi hayo kuwa ni makazi, biashara, viwanda, kilimo, ufugaji na matumizi mengineyo.

Akiongelea Sheria ya Mipango Miji namba 8 ya mwaka 2007 na Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria nyinginezo, hifadhi ya mazingira husimamiwa na mamlaka ya upangaji kwa kushirikiana na wadau wa mji husika.
=30=

UCHAGUZI WA JIMBO LA KALENGA KUFANYIKA KWA AMANI NA UTULIVU



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa amewataka wananchi wa jimbo la Kalenga kujitokeza kwa wingi kupiga kura za kumchagua mbunge wa jimbo hilo.
 
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma
Kauli hiyo ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma ameitoa alipoongea na waandishi wa habari ofisini kwake kuelezea hali halisi katika jimbo la uchaguzi la Kalenga na kuwataka wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi kumchagua mbunge katika uchaguzi utakaofanyika tarehe 16/03/2014.

Akiongelea ulinzi na usalama, Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama katika Mkoa wa Iringa amewahakikishia wananchi kuwa ulinzi utakuwepo wa kutosha na vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kuhakikisha amani na usalama kwa wananchi katika kipindi chote cha kupiga kura na wakati wa kutoa matokeo.

Dkt. Ishengoma amesema kuwa maandalizi yamekamilika na vifaa vyote vinavyohitajika vimefika katika vituo vya kupigia kura. Amesema kuwa vituo vyote vitakuwa wazi kuanzia asubuhi hadi jioni kwa muda uliopangwa.
=30=

Saturday, February 22, 2014

TATHMINI YA MAZINGIRA KUFANYIKA TENA KABLA YA STENDI YA IGUMBILO



Serikali imelitaka baraza la usimamizi wa mazingira (NEMC) kufanya upya tathmini ya athari za kimazingira katika eneo la Igumbilo inapotarajiwa kujengwa stendi mpya ya mabasi na halmashauri ya Manispaa ya Iringa.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira, Dkt. Binilith Mahenge alipofanya ziara ya kutembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya mabasi mjini Iringa.


Waziri wa Nchi OMR- Mazingira, Dkt. Binilith Mahenge (wa tatu kushoto)
 
Dkt. Mahenge amelitaka baraza la usimamizi wa mazingira kufanya upya tathmini juu ya athari za kimazingira na kuwasilisha taarifa hiko kwake. Kauli hiyo imekuja kutokana na mvutano wa muda mrefu sasa baina ya Manispaa ya Iringa na wadau wa maji kwamba mradi huo itaharibu chanzo pekee ya chaji katika mji wa Iringa. Aidha, Dkt. Mahenge amesema kuwa katika kipindi chote manispaa ya Iringa isifanye shughuli zozote za maendeleo katika eneo hilo.

Waziri wa Nchi OMR amesema kuwa lengo la kutembelea eneo la Igumbilo ni kujionea hali halisi kufuatia hoja zilizotolewa na wadau mbalimbali hasa wa maji kuhusu ujenzi wa stendi hiyo. Amesema kuwa baada ya tathmini hiyo wataalam watamshauri kitaalam kwa mujibu wa taaluma. Amesema kuwa maamuzi ya kitaaluma hayawezi kufanywa kisiasa.

Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa, Gervas Ndaki litaka suala hilo lisichukuliwe kisiasa. Amesmea kuwa wapo baadhi ya wafanyabiashara wanaopinga kwa nguvu dhana ya stendi hiyo kuhamishwa mjini na kujengwa eneo la Igumbilo kutokana na maslahi yao ya kibiashara.

Katika taarifa fupi ya mkoa wa iringa iliyowasilsihwa kwa Waziri wa nchi OMR na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu amesema kuwa mradi wa ujenzi wa stendi, unatokana uhitaji mkubwa wa uboreshaji wa miundombinu ya usafiri katika manispaa ya Iringa na mkoa kwa ujumla. Amesema lengo la ujenzi wa stendi mpya ni kuboresha muindombinu ya stendi ndani ya mji kutokana na misongamano mikubwa katikati ya mji na kukosa nafasi ya kupanua stendi. Amesema kuwa halmashauri hiyo kwa kujenga stendi hiyo inakusudia kuongeza kuboresha vyanzo vya mapato na kukuza shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wake.

Akiongelea sheria iliyoanzisha mamlaka za maji, Ayubu amesema kuwa sheria hiyo inazitaka mamlaka kusambaza kwa wananchi maji yaliyo safi na salama. Amesema kuwa ikitokea mamlaka imewasambazia wananchi maji ambayo hayako katika viwango mamlaka itakuwa inakiuka sheria. Amesema kuwa wananchi wa manispaa ya Iringa watakuwa kwenye mazingira hatarishi kwa kunywa maji yenye takakemikali na kupelekea madhara kiafya.
=30=
  

SEKTA YA KILIMO KUAJIRI ZAIDI




Sekta ya kilimo inachangia asilimia kubwa katika maendeleo ya taifa na kuajiri watu wengi zaidi nchini. 

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika kongamano kati ya serikali na wadau kuhusu siku ya kilimo na usalama wa chakula afrika lililofanyika katika kijiji cha Kaning’ombe wilayani Iringa.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la wadau wa kilimo (ANSAF), Audax Rukonge

 Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma aliyemuwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

 Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (watatu kushoto) aliyemuwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Dkt. Bilal amesema “kama tujuavyo kilimo ni uti wa mgongo kwa uchumi wa taifa letu. Kilimo hutegemewa na watanzania wengi hasa akina mama, na asilimia 75 ya kipato cha watanzania hutokana na kilimo”. Amesema kuwa kilimo kinasaidia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wan chi (GDP). Akiongelea umasikini, amesema kuwa pamoja na ukweli kwamba umasikini bado upo nchini kilimo ni suluhisho la mabadiliko kwa watanzania wengi. Amesema kwa msingi huo ni vizuri dira na malengo yaelekezwe katika kilimo cha kibiashara.

Makamu wa Rais amesema kuwa elimu ya uzalishaji bora wenye tija kwa wakulima wadogo itolewe ili waondokane na umasikini. Amesema kuwa kufanya hivyo uchumi wan chi utazidi kukua na kuongezeka kwa ustawi wa jamii.

Dkt. Bilal amesema kuwa serikali itaendelea na jitihada za kuendeleza na kuimarisha sekta ya kilimo nchini. Amesema program ya kuendeleza sekta ya kilimo ilizinduliwa rasmi mwaka 2005/2006 ambapo malengo makubwa ya program hiyo ni kuhakikisha kilimo kinakua kwa asilimia 6 kwa mwaka. Amesema hadi sasa lengo halijafikiwa sababu ukuaji bado ni asilimia 4 tu.  Amesema malengo ya hayawezi kufikiwa bila kuunganisha nguvu na jitihada za pamoja. Ameseme kupitia mkakati wa kilimo kwanza, serikali inaendelea kusimamia na kutekeleza malengo iliyojiwekea na kwa kuzishirikisha sekta binafsi ili kuleta mafanikio makubwa kwa pamoja.

Akiongelea makubaliano na ahadi za Maputo mwaka 2003, Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la wadau wa kilimo (ANSAF), Audax Rukonge amesema kuwa katika kilele cha mkutano wa umoja wan chi za Afrika, AU mwaka 2003 wakuu wan chi walikubaliana kuwa kila nchi itenge kiasi cha asilimia 10 ya bajeti ya kitaifa iingizwe kwenye kilimo.

Amesema kuwa kiwango hicho kilitarajiwa kutosha kuchangia kuongeza uzalishaji na tija, kukuza sekta ya kilimo kwa asilimia 6 kwa mwaka na kuondoa tatizo la njaa na umasikini. Amesema kuwa miaka kumi baadae ni nchi nane tu za Afrika zimetimiza ahadi hiyo na kilimo katika nchi hizo kimekua kwa asilimia 6 na zaidi.

Amesema kuwa unahitajika mtazamo mpya wa kibiashara dhidi ya kilimo tofauti na kisiasa kwa kuwekeza maeneo ya kimkakati na yenye ufanisi mkubwa.

Kongamano hili ni fursa ya kuhakikisha yanapatikana mafanikio katika kilimo kwa kuzikabili changamoto mbalimbali kwa kuzifanyia kazi ili kupata mazao bora yenye tija. Aidha, ni muendelezo wa Kongamano la Umoja wa Bara la Afrika uliozinduliwa na Rais Yayi Boni wa Benini, Mwaka 2012, katika kuendeleza Kilimo na Usalama wa chakula  ili kupata chakula cha uhakika.
=30=