Sunday, October 1, 2017

SEKTA YA UTALII YAENDELEA KUKUA KILA MWAKA



Na Mwandishi Maalum, IRINGA
Sekta ya utalii imekuwa ikikuwa na kuchangia katika mapato ya Taifa zaidi ya dola za kimarekani milioni 2,000 mwaka 2016.

Kauli hiyo ilitolewa na waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe wakati wa kufungua maadhimisho ya siku ya utalii Duniani, maonesho ya Karibu Kusini na maonesho ya shughuli za viwanda vidogo (SIDO) mjini Iringa jana.

Prof. Maghembe alisema kuwa mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka dola za marekani milioni 1,353.29 mwaka 2011 hadi kufikia dola za marekani 2,131.57 mwaka 2016. “Mapato haya yamechangiwa na watalii wa kimataifa waliotembelea nchini ambao waliongezeka kutoka watalii 867,994 mwaka 2011 hadi kufikia watalii 1,284,279 kwa kipindi hicho. Takwimu zinaonesha kuwa sekta hii inachangia zaidi ya 11% ya ajira zote hapa nchini” alisema Prof. Maghembe.

Akiongelea mchango wa utalii katika ukuaji wa uchumi, waziri huyo alisema kuwa sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta zinazochangia sana ukuaji wa uchumi nchini. “Nyote mtakubaliana na mimi kwamba, utalii ni moja kati ya sekta inayochangia ukuaji wa uchumi nchini kutokana na kuwa chanzo cha kuliingizia Taifa fedha za kigeni. Utalii huongeza ajira na kipato kwa jamii, pia ni chachu kwa ukuaji wa sekta zingine. Sekta hii huchangia 25% ya mauzo nchi za nje.

Prof. Maghembe alisema kuwa ukuaji wa sekta ya utalii nchini unachangiwa kwa kiasi kikubwa na juhudi za serikali katika usimamizi, uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali, utangazaji, mazingira bora ya uwekezaji pamoja na ushirikiano madhubuti baina ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Nae mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza alisema kuwa mkoa wake daima utakuwa mstari wa mbele kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa ya mfano na kukua kwa kasi.
=30= 

Thursday, September 21, 2017

WADAU WAOMBWA MICHANGO KUFANIKISHA UTALII NA KAZI ZA VIWANDA VIDOGO



Na. Dennis Gondwe, IRINGA
Wadau wa maendeleo ya utalii mikoa ya nyanda za juu kusini wameombwa kuchangia maonesho ya Utalii Karibu Kunisi na shughuli za wajasiliamali wa viwanda ili yafanikiwe na kuchangia katika uchumi wa Taifa.

Ombi hilo lilitolewa na katibu msaidizi wa kamati ya maonesho ya utalii mkoa wa Iringa, Hawa Mwechaga alipokuwa akikabidhi stakabadhi ya malipo kwa mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Jackson Ngowi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa jana.

Mwechaga alisema “nichukue nafasi hii kwa niaba ya Katibu Tawala mkoa wa Iringa, kumshukuru Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kwa mchango wake wa shilingi milioni moja fedha taslimu katika kufanikisha maonesho ya Utalii Karibu Kusini na shughuli za wajasiliamali wa SIDO”. Alisema kuwa wadau wa utalii na biashara wana nafasi nzuri kuchangia katika kufanikisha maonesho hayo kwa sababu watafahamika na kukuza biashara na huduma wanazofanya.

Mwechaga alisema kuwa kupitia sekta ya utalii inayokuwa kwa kasi nchini, wadau wameweza kutangaza bidhaa na huduma wanazotoa na kuwafikia wananchi wengi zaidi. Lakini kupitia maonesho ya utalii wananchi wengi wameweza kupata maono mapya ya kufanya kazi za kiutalii na wengine kuboresha kazi walizokuwa wakifanya awali.

Maonesho ya Utalii Karibu Kusini mwaka 2017 yatafanyika mkoani Iringa kwa pamoja na maonesho ya shughuli za wajasiliamali wa viwanda vidogo (SIDO) yakihusisha mikoa ya nyanda za juu kusini katika uwanja wa Kichangani mjini Iringa kuanzia tarehe 27/9/2017 -02/10/2017.
=30=  

Tuesday, September 19, 2017

MAFUNZO ELEKEZI KWA WATUMISHI WAPYA IRINGA KULETA MABADILIKO CHANYA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wapya katika ofisi ya mkuu wa mkoa Iringa yataleta mabadiliko chanya katika utumishi wa umma mkoani Iringa.

Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Takwimu katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Iringa, Hildegarda Kimaro katika mahojiano maalum yaliyofanyika katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa jana.
Afisa Takwimu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Hildegarda Kimaro

Kimaro alisema “mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wapya ni mazuri, tumejifunza mambo mbalimbali ambayo hatukuyafahamu awali. Mfano sheria ya utumishi wa umma na kanuni zake na utunzaji wa kumbukumbu”. 

Aliongeza kuwa awali utunzaji kumbukumbu lilifahamika kuwa ni jukumu la watunza kumbukumbu wasaidizi katika ofisi ya mkuu wa mkoa, lakini baada ya mafunzo imebainika kuwa utunzaji kumbukumbu ni jukumu wa watumishi wote wa umma kwa nafasi zao.

Akiongelea umuhimu wa mafunzo hayo elekezi ya awali kwa watumishi wa umma, Kimaro alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kutokuvunja sheria za utumishi. “Mafunzo haya ni muhimu na yatatusaidia kutokuvunja sheria ambazo tungevunja bila kufahamu. Kwa mafunzo haya tumeweza kufahamu jambo ambalo ni sahihi kufanya katika utumishi wa umma na ambayo si sahihi kufanya katika utumishi wa umma” alisema Kimaro.     

Kimaro alishauri kuwa watumishi wapya wanapoajiriwa wapewe mafunzo elekezi ya awali angalau ndani ya miezi mitatu ya awali. 

Katika kuongeza umakini wa mafunzo, ni vizuri mafunzo hayo yakatolewa nje ya eneo la kazi ili kuwawezesha washiriki wa mafunzo kujikita katika mafunzo kuliko kutekeleza majukumu mengine ya kiutumishi jambo linaloathiri utulivu na usikivu wakati wa mafunzo” alishauri Kimaro.

Mafunzo elekezi ya awali ya siku tano kwa watumishi wapya wa umma yameandaliwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na chuo cha utumishi wa umma (TPSC) yakishirikisha watumishi wapya 107 kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa, ofisi za wakuu wa wilaya na hospitali ya rufaa ya mkoa.
=30=





WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI NA NIDHAMU IRINGA



Na Mwandishi Maalum, IRINGA
Watumishi wa umma mkoani Iringa wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na nidhamu katika kutekeleza majukumu yao wanapowahudumia wananchi.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akifungua mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wapya wa umma walioajiliwa katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa, mafunzo yalifanyika katika ukumbi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa jana.

Ayubu alisema kuwa msingi wa utumishi wa umma umejikita katika uadilifu, hivyo mtumishi wa umma lazima afanye kazi kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu. Aliongeza kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dr John Magufuli imejipambanua kwa kusimamia nidhamu na uwajibikaji kwa watumishi wa umma. Aliwataka watumishi wa umma mkoani Iringa kuwa mfano mzuri wa kuingwa katika nidhamu na uwajibikaji wanapowahudumia wananchi ili wabaki na kumbukumbu ya huduma njema.

Akiongelea umuhimu wa mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wa umma, Katibu Tawala mkoa alisema kuwa watumishi wengi wanatoka katika maeneo tofauti yenye mitazamo tofauti hivyo, kuitaji kufundishwa utaratibu wa kazi katika serikali. 

Mafunzo haya ni muhimu sana unapoingia katika utumishi wa umma. Tunatoka katika vyuo tofauti na tamaduni tofauti hivyo, hata tabia zinakuwa tofauti. Mafunzo haya yanalenga kutufundisha namna utumishi wa umma ulivyo na jinsi mtumishi wa umma anavyotakiwa kuonekana na kutenda kazi” alisema Ayubu.

Aliwataka watumishi hao kubadilika baada ya mafunzo kimtazamo na kiutendaji na kuzingatia viwango vya juu katika utumishi wao. 

Unajua unapoingia katika utumishi wa umma, unajikuta unafanya makosa, ila tunashindwa kukuchukulia hatua za kiutumishi badala yake tunalazimika kukufanyia ushauri zaidi. Tunabadilika na kuwa wazazi na walezi katika kuwaelimisha watumishi” alisema Ayubu. 

Aliongeza kuwa baada ya mafunzo haya watakuwa wakiwachukulia hatua stahili za kiutumishi watumishi wote watakaotenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma.

Alisema kuwa katika mafunzo hayo watumishi wa umma watafundishwa muundo wa serikali, uendeshaji wa shughuli za serikali, utunzaji wa kumbukumbu, maadili ya utumishi wa umma, maboresho ya utumishi wa umma, huduma kwa mteja, sheria ya utumishi wa umma namba 8 ya mwaka 2002 na kanuni zake, mpango wa kudhibiti ukimwi kwa watumishi wa umma na upimaji wa wazi utendaji kazi kwa watumishi wa umma.

Mafunzo elekezi ya awali ya siku tano kwa watumishi wapya wa umma yameandaliwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na chuo cha utumishi wa umma (TPSC) yakishirikisha watumishi wapya 107 kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa, ofisi za wakuu wa wilaya na hospitali ya rufaa ya mkoa.
=30=