Friday, December 10, 2010

IRINGA YAONGEZA KIWANGO CHA UFAULU DARASA LA SABA

Mkoa wa Iringa umefanikiwa kuongeza kiwango cha kufaulu kwa wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka 2010 kutoka asilimia 59.65 ya mwaka 2009 hadi 63.01 mwaka 2010 imefahamishwa.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude K Mpaka katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao cha uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2010 kilichofanyika katika kituo cha vijana cha Nazareth Njombe.

Afisa Elimu Mkoa wa Iringa, Mwl Salum Maduhu (kushoto),
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bibi. Gertrude Mpaka (katikati) na
Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Bibi.  Sara Dumda (kulia)

Mpaka amesema “nachukua nafasi hii kuwapongeza Maafisa Elimu wa Wilaya, Waratibu wa Elimu Kata Walimu Wakuu na walimu kwa ujumla kwa kazi nzuri wanayoifanya na kufanya Mkoa wa Iringa kuongeza kiwango cha ufaulu kutoka asilimia 59.65 ya mwaka 2009 hadi asilimia 63.01 mwaka 2010”.

Amezitaja takwimu za watahiniwa wa kuhitimu elimu ya Msingi mwaka 2010 kuwa ni watahiniwa 44,275. Kati yao 20,991 ni wavulana na 23,284 ni wasichana. Aidha jumla ya waliofaulu ni mtihani mwaka 2010 ni 27,899 wavulana wakiwa 13,709 na wasichana ni 14,190, ambao ufaulu huo ni sawa na asilimia 63.01 ya watahiniwa wote.

Katibu Tawala Mkoa ametaja changamoto inayoukabili Mkoa katika Sekta ya elimu kuwa ni wanafunzi wanaosajiliwa kufanya mtihani kutofanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro. Amesema kuwa utoro unachukua karibu asilimia 75.19 ya watahiniwa wote. Idadi ya wanafunzi walioshindwa kufanya mtihani mwaka huu ni 566, ikilinganishwa na 816 walioshindwa kufanya mtihani huo mwaka 2009 na kuagiza litafutiwe ufumbuzi wa kina.

Akiainisha sababu za wasiofanya mtihani Afisa Elimu Mkoa wa Iringa, Salum Maduhu amezitaja kuwa ni utoro wanafunzi (496), vifo (18), ugonjwa (38), mamba (13), sababu nyingine (1).

Kwa upande wa mahudhurio siku ya mitihani yamepanda kutoka 98.43% ya mwaka 2009 hadi 98.74% mwaka 2010. Aidha kiwango cha kumaliza elimu ya msingi kimeshuka kutoka 80.39 (2009) hadi 76.80% (2010) ambayo ni sawa na upungufu wa 3.59%.

Kwa upande wa ufaulu na nafasi kimkoa kwa kila Halmashauri 2010 ni Iringa Manispaa 77.33% (1), Mufindi H/M 71.67% (2), Njombe Mji 71.29% (3), Njombe H/M 66.47% (4), Makete H/M 62.88% (5), Ludewa H/M 58.83% (6), Iringa H/M 42.56% (7) na Kilolo H/M 39.71% (8).

Aidha Afisa elimu Mkoa amezitaja shule 10 zilizofanya vizuri kuwa
ni St.
Benedict (Mji Njombe), Southern Highland (Mufindi), Brooke Bon (Nufindi), Livingstone (Njombe Mji), Ukombozi (Iringa Manispaa), Lupalama A (Iringa H/M), Lihogasa (Njombe Mji), Star (Iringa Manispaa), Lugarawa (Ludewa) na St. Dominic Savio (Iringa Manispaa).

Maduhu pia amewataja wahitimu wawili ambao ni mapacha walioungana kimwili, kutoka shule ya msingi Ikonda, Halmashauri ya Wilaya ya Makete. Wanafunzi hawa wamefaulu na kwa mchanganuo wa alamaufuatao:

JINA
MASOMO
Kis
Eng
M/Jamii
Hisb.
Say
Jumla
Consolatha Mwakikuti
32
34
29
27
29
151
Maria Mwakikuti
32
36
25
27
31
151


Mkoa wa Iringa umekamata nafasi ya tatu kitaifa kwa miaka mine mfululizo tangu mwaka 2007 hati 2010 na unajumla ya shule 853 za msingi.

No comments:

Post a Comment