Friday, December 10, 2010

…UMITASHUMTA NI VIWANGO TU

Wanamichezo na watendaji wametakiwa kuendesha mashindano na kambi ya mkoa wa Iringa kwa viwango vilivyo bora ili mkoa uweze kujivunia hazina ya vipaji iliyopo kwa wananfunzi wa shule za msingi.

Bartholomew Mwellange Mwella, Afisa Tarafa ya Makambako,
akipiga mpira kuashiria ufunguzi rasmi wa UMITASHUMTA Mkoa wa Iringa

Rai hiyo imetolewa na Bartholomew Mwellange Mwella, Afisa Tarafa ya Makambako, kwa niaba ya Katibu Tawala Wilaya ya Njombe, Evergrey Keiya wakati akifungua rasmi mashindano ya michezo ya shule za msingi ngazi ya mkoa wa Iringa uliofanyika katika Mji mdogo wa Makambako.

Mwella amesisitiza kuepuka kasoro zote zilizojitokeza hapo awali na kupelekea mashindano hayo kufutwa mwaka 2001. Aidha alisisitiza kutokuwa na uvumilivu kwa mtendaji yeyote atakayetaka kuharibu mashindano hayo kwa namna moja au nyingine.

Amesisitiza kuwa wakati wa kuchagua timu ya mkoa lazima walimu na wachezaji watakaochaguliwa wawakilishe uhalisia wa mkoa na pasiwepo na masuala ya upendeleo kwa kuangalia udugu, mahusiano mazuri na mtu Fulani, wala Halmashauri anayotoka.

Aidha amewataka washiriki kutumia vizuri fursa waliyoipata kushiriki katika michezo hii kwa kuonesha vipaji vyao na kuuwakilisha vema mkoa katika mashindano ya kitaifa. Afisa Tarafa huyo amesisitiza kucheza kwa amani na utulivu wa hali ya juu mbali na halmashauri wanazotoka kwa kuzingatia wao ni watoto wa mkoa mmoja na ni ndugu.

Akiongeleza sababu za kufutwa kwa mashindano ya UMITASHUMTA mwaka 2001 Mwella amesema kuwepo kwa mapungufu mengi ndiyo sababu ya msingi ya kufutwa kwake. Ameyataja mapungufu hayo kuwa ni pamoja na malezi hafifu hasa kwa wanafunzi wa kike, mapungufu ya idadi ya siku za masomo, tatizo la chakula kwa wanafunzi, watumishi kutopewa stahili zao wanazostahili, udhibiti wa nidhamu kwa wanafunzi na vyombo duni vya usafiri kwa wanafunzi hao.

Nae Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Iringa, Mwalimu Euzebio Mtavangu ameutaja umuhimu wa mashindano hayo kuwa ni kusaidia kuibua vipaji vya wachezaji katika timu za wilaya, Mkoa na Taifa, kuimarisha afya za washiriki, kusaidia kujenga uzalendo wa kulipenda Taifa. Aidha amezitaja faida nyingine kuwa ni sehemu ya muendelezo wa vipaji vya darasani na hivyo kuwafanya wanafunzi wazingatie masomo wakati wote, kusaidia kuimarisha udugu na urafiki miongoni mwa wanamichezo.

Afisa Michezo wa Mkoa wa Iringa, Keneth Komba amesema kuwa lengo la mashindano hayo ya UMITASHUMTA ni kuwajengea umoja wanafunzi wa shule za msingi na kuwafanya wajue kuwa wao ni wamoja. Ameongeza kuwa Mkoa wa Iringa umepata heshima kubwa kuwa miongoni mwa mikoa 10 iliyoteuliwa katika kushiriki katika mashindano hayo. Mikoa hiyo ni Morogoro, Kilimanjaro, Pwani, Singida, Dodoma, Arusha, Tanga, Mbeya, Dar Es Salaam na Iringa yenyewe.

Mashindano ya UMITASHUMTA yatafanyika mjini Kibaha, Mkoani Pwani kuanzia tarehe 13 Disemba, 2010 na yatahusisha michezo ya mpira wa miguu, pete na riadha.           

No comments:

Post a Comment