HALMASHAURI ZAAGIZWA KUTENGA MAENEO YA MITI
Halmashauri za Wilaya, Manispaa na Mji Mkoani Iringa zimeagizwa kutenga maeneo makubwa ya kupanda miti kwa faida ya Halmashauri husika na mkoa kwa ujumla kutokana na mkoa kuwa na hali nzuri ya hewa.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Georgina Bundala wakati akisoma hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa katika uzinduzi wa siku ya upandaji miti kimkoa uliofanyika katika Halmashauri ya mji wa Njombe.
Bundala amesema “nachukua nafasi hii kuziagiza Halmashauri zote za Mkoa huu zitenge maeneo makubwa kwa ajili ya kupanda miti kwa ajili ya faida ya Halmashauri husika”. Amesema mkoa wa Iringa una hali ya hewa nzuri inayofaa kwa zao la miti na kuwataka wananchi kutunza vizuri upendeleo huo mkoa uliojaaliwa na Mwenyezi Mungu ili kupiga hatua ya maendeleo.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Ludewa ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya njombe amesema kuwa mkoa wa Iringa una eneo kubwa la Misitu ya asili na ya kupanwa. Amefafanua kuwa Mkoa unamisitu ya hifadhi zaidi ya 64 yenye eneo la hekta zaidi ya 325,650. Vilevile amesema misitu ya kupandwa inaukubwa zaidi hekta 110,283 na kufafanua kuwa misitu hiyo ni pamoja na ile Halmashauri, vijiji, watu binafsi, makampuni na vikundi.
Wananchi wakiwa wamejiandaa vilivyo kushiriki zoezi zima la upandaji miti
Aidha, alichukua nafasi hiyo kuwataka wananchi kuendelea na zoezi la kuotesha miche na kuipanda, kuhifadhi ardhi kwa madhumuni ya kuzuia mmomonyoko wa ardhi, kuhifadhi misita ya asili na kuhifadhi vinazo vya maji.
Amesema uongozi wa mkoa umeamua siku ya upandaji miti kimkoa ifanyike tarehe 10 Januari, 2011 kwa kuwa hali ya hewa inaruhusu kwa zoezi hilo kwa mkoa mzima hivyo hauwezi kusubiri mpaka mwezi Aprili. Siku ya upandaji miti mwaka huu inaongozwa na ujumbe usemao “MISITU NI UHAI; PANDA MITI KWANZA NDIPO UKATE MTI”.
“Ujumbe huu unatuasa tupande miti mingi sana na tukate mti mmoja na tukifanya hivyo tutafanikiwa kuhifadhi mazingira ya nchi yetu” amesema Bundala.
Akielezea takwimu amesema kuwa Mkoa wa Iringa ulipanda miti zaidi ya 6,603,296 katika Halmashauri zake katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari 2001 hadi Januari 2010. “Upandaji miti ni jambo muhimu sana, lakini muhimu zaidi ni kuitunza miti iliyopandwa. Haina maana kutumia nguvu zetu kuotesha na kupanda miti na kisha kuicha miti hiyo iungue moto au kuliwa na mifugo inayochungwa katika maeneo yaliyopandwa miti” Alisisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.
Aliagiza kuilinda miti hiyo kwa nguvu zote na pia ifanyike sensa ya miti ili kuwa na takwimu sahihi zinazoonyesha idadi ya miti iliyopona na iliyopo mashambani.
Shughuli hii ya kupanda miti hufanyika kila mwaka hapa nchini kwa kuwashirikisha wananchi wa maeneo mbalimbali. Kwa kawaida siku ya upandaji miti kitaifa kila mwaka ilikuwa inafanyika tarehe mosi ya Mwezi Januari lakini kuanzia mwaka jana 2010 shughuli ya upandaji miti Kitaifa inafanyika Mwezi wa Aprili.