Wednesday, February 23, 2011

HUDUMA YA MAJI VIJIJINI YAONGEZEKA IRINGA
Zaidi ya asilimia 60 ya wakazi wote wa vijijini wanapata huduma ya maji safi na salama kwa teknolojia ya mtiririko, kusukuma maji kwa mitambo ya umeme na dizeli na visima katika Mkoa wa Iringa hadi kufikia Disemba 2010.
Takwimu hizo zimetolewa na Mhandisi wa Maji wa Mkoa wa Iringa, Mhandisi Amos Mbelwa Byemerwa wakati akiwasilisha taarifa ya sekta ya Maji kwa mkoa wa Iringa kwa Waziri wa Maji, Prof. Mark J. Mwandosya (Mb) alipofanya ziara ya kikazi Mkoani Iringa katika ukumbi wa NSSF.
Amos Mbelwa Saulo Byemerwa, Mhandisi wa Maji Mkoa
Mhandisi Byemerwa amesema kuwa teknolojia inayotumika kuwapatia wananchi maji karibu na maskani yao ni miradi ya mtiririko, kusukuma maji kwa mitambo ya umeme na visima vilivyofungwa pampu za mkono. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa inaongoza kwa asilimia 67.5 ilifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe yenye asilimia 67.4 wakati Halmashauri ya Mji Njombe ndiyo yenye asilimia ndogo ikiwa na asilimia 51 pekee.
Mhandisi Byemerwa ameongeza kuwa mkoa unavijiji 498 vyenye kamati za maji kati ya jumla ya vijiji 720 vya mkoa wa Iringa. Ameongeza kuwa vijiji 366 vinamifuko ya maji iliyokuwa na kiasi cha shilingi 255,635,452 hadi kufikia Desemba 2010.  Aidha, vijiji 92 vilivyopo katika awamu ya kwanza ya programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji vimekusanya jumla ya shilingi 209,787,799 kama sehemu ya asilimia 2.5 ya gharama za ujenzi wa miradi katika vijiji vyao. Amesema kuwa mkoa ulikuwa na vyombo huru 20 vya watumiaji maji vikiwa ni jumuiya za watumiaji maji 13 na mamlaka za maji 7.
Akiongelea ulinzi na utunzaji wa vyanzo vya maji Mhandisi Byemerwa amesema “mkoa unachukua mbalimbali kutunza vyanzo vya maji na kuhakikisha havichafuliwi wala kuharibiwa kutokana na kazi za kibinadamu karibu na vyanzo hivyo”. Amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuvitambua vyanzo vya maji na kuviwekea mipaka na kutayarisha mpango wa kuhifadhi kila chanzo kilichotambulika kwa kushirikiana na wananchi. Hatua nyingine ni pamoja na kuunda vyama vya watumiaji maji katika mabonde madogo ya mito na kushirikiana na ofisi ya Bodi ya bonde la Rufiji na Ziwa Nyasa na mashirika yasiyo ya kiserikali kutoa elimu kwa wananchi juu ya hifadhi ya mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za maji.
Waziri wa Maji, Prof. Mark Mwandosya (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji
IRUWASA Mhandisi Mfugale wakifuatilia taarifa ya Maji Mkoa
Akichangia katika taarifa hiyo Waziri wa Maji, Prof. Mark Mwandosya amesema kuwa programu ya maendeleo ya sekta ya maji si ya serikali pekee bali inahusisha wadau mbalimbali wa ndani na nje kutokana na kuwa na malengo mbalimbali. Aidha, amesema “ugumu uliopo unatokana na kuzungumzia rasilimali finyu tulizonazo hivyo inahitajika nguvu ya ziada”.

No comments:

Post a Comment