Thursday, March 10, 2011

...UKOMBOZI WA MWANAMKE!

Ukombozi wa mwanamke ni suala mtambuka katika jamii na unalenga kumuwezesha mwanamke katika kulea familia yake katika misingi ya haki na usawa wa kijinsia.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka, aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa Wilayani Njombe.

Mpaka amesema “jukumu la kumkomboa mwanamke si jukumu la Serikali peke yake bali linamgusa kila mwanajamii katika nafasi yake”. Amesema jukumu la mwanamke kama mzazi ni kuilea familia yake katika misingi ya haki na usawawa kijinsia. Aidha, amewataka wanansiasa na viongozi wa dini kuhubiri haki na usawa wa kijinsia kwa wananchi katika ujumla wao.

 Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka (kulia) akosoma Hotuba yake wakati wa Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Kimkoa Wilayani Njombe, kushoto ni Katibu Tawala Wilaya ya Njombe, Evergrey Keiya aliyeshika kipaza sauti

Katibu Tawala Mkoa ameyataja maeneo manne ya utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa Beijing China uliofanyika mwaka 1995 ambayo Tanzania imeyachagua kuyatekeleza kama vipaumbele kutokana na uchache wa rasilimali zilizopo kuwa ni pamoja na kujenga mazingira ya usawa katika elimu na ajira, kuwawezesha wanawake kutambua haki zao kisheria. Eneo lingine ni kuwajengea uwezo wanawake wa kushiriki masuala kisiasa na kufanya maamuzi na pia kuwajengea wanawake uwezo kiuchumi ili waweze kuondokana na umasikini.

Akiongelewa eneo la kumuwezesha mwanamke kutambua haki zao kisheria, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Iringa, Menrad Dimosso amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2010/ 2011 jumla ya wanawake 3,756 wa mkoani Iringa walipatiwa mafunzo juu ya Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999, Sera ya Wanawake, Sheria ya Mirathi,, Haki za Binadamu na Sheria ya Ndoa. Ameendelea kusema kuwa Sekta ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto mkoani hapa imejipanga kuendelea na zoezi hilo kwa lengo la kuwajengea uwezo wanawake wengi zaidi kutambua haki zao kisheria.

Maazimisho hayo yanaongozwa na kauli mbiu isemayo ‘fursa sawa katika elimu, mafunzo, sayansi na teknolojia; njia ya wanawake kupata ajira bora’.

No comments:

Post a Comment