JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA KWA UMMA
ASALI YA TANZANIA NI NZURI NA INAYO
UBORA WA KIMATAIFA
Wizara ya Maliasili na Utalii inatoa taarifa kuwa asali ya Tanzania ni nzuri kwa matumizi ya binadamu na kuwa ina viwango vya ubora vya kimataifa. Ukweli huu umedhihirishwa na maabara mbalimbali duniani, hasa zile za Jumuiya ya Ulaya ambao ndio wanunuzi wakubwa wa asali ya Tanzania.
Ufafanuzi huu unatolewa kufuatia taarifa ya hivi karibuni kupitia baadhi ya vyombo vya habari iliyosema kuwa kuna asali kutoka Tanzania ambayo ilikataliwa nchini China baada ya kuonekana kuwa na kemikali ya Nicotin. Wizara haina taarifa na asali hiyo maana haijatoa kibali chochote cha kusafirisha asali kwenda nchini China kwa miaka ya karibuni. Kisheria asali hairuhusiwi kusafirishwa kwenda nchi za nje bila kupata kibali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.
Kupitia Mpango wa udhibiti Kemikali Katika Asali (Chemical Residue Monitoring Plan) Wiraza ya Maliasili na Utalii inahakikisha kuwa asali ya Tanzania inakidhi viwango vya ubora wa kimataifa. Wizara hukusanya sampuli za asali kutoka maeneo mbalimbali nchini na kuzifanyia uchambbuzi kwenye maabara teule (Accredited Laboratory) na matokeo yake yanapelekwa kwa wanunuzi, hasa Umoja wa nchi za Ulaya ambao ndio wanunuzi wakubwa wa asali ya Tanzania.
Tanzania ni nchi mojawapo kati ya nchi 4 za Afrika zinazoruhusiwa kuuza asali yake katika nchi za Umoja wa Ulaya. Kwa mfano, taarifa zinaonyesha kuwa asali inayozalishwa mkoani Tabora haijawahi kupatikana na kemikali ya Nicotin, wala kemikali yoyote inayodhuru binadamu.
Ili kudumisha ubora wa asali ya Tanzania Wizara inazingatia yafuatayo kabla ya kutoa Kibali cha kusafirisha asali kwenda nchi za nje:
- Asali inakaguliwa na wataalam wa nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii;
- Asali inapimwa na kuchunguzwa kwenye maabara za hapa nchini na nchi za nje kabla ya kusafirishwa;
- Kibali cha kusafirisha kinatolewa kufuatana na taarifa ya maabara.
Tarifa za maabara zinaonyesha kila mwaka kuwa asali ya Tanzania haina kemikali zozote zinazoweza kudhuru. Sababu mojawapo inayoifanya asali ya Tanzania iwe na ubora wa asili ni kwa kuwa inazalishwa mbali kutoka kwenye mashamba yanayotumia kemikali. Kwa mfano zaidi ya aslimia 90 ya asali ya Tabora huzalishwa kwenye mapori ya akiba na misitu ya hifadhi (Game , Forest Reserves).
Kwa mfano, katika Wilaya ya Sikonge asali huzalishwa katika Misitu ya Hifadhi ya Nyahua, Ugunda, Uwala na Iswagala. Katika Wilaya ya Urambo asali huzalishwa katika pori la akiba la Ugala na Myovosi/Kigosi na Misitu ya Hifadhi ya Mpanda line, North Ugala, na Igombe. Aidha katika Wilaya ya Uyui asali huzalishwa kwenye Misitu ya Hifadhi ya Igombe, Ilomelo Urumwan na Goweko. Katika maeneo yote haya wafugaji nyuki hutundika mizinga zaidi ya kilomita 60 kutoka makazi na mashamba ya tumbaku.
Aidha, ufugaji nyuki husimamiwa na Sheria ya Ufugaji Nyuki Namba 15 ya mwaka 2002 ambayo inakataza kufuga nyuki karibu na mashamba yanayotumia kemikali. Inasisitizwa kuwa ufugaji nyuki ufanyike umbali wa kipenyo cha kilomita 7 kutoka mashamba ya tumbaku au mengine yanayotumia viwatilifu.
Sheria hii inatuhakikishia ubora zaidi kuliko Sheria za kimataifa ambazo zinakataza kuzalisha asali katika kipenyo cha kilometa 3 tu. Wizara ya Maliasili na Utalii ikishirikiana na Halimashauri za Wilaya inawaelimisha wafugaji nyuki kupitia ughani (Extension Services) kuhusu umuhimu wa kufuga nyuki kwa kuzingatia Sheria ya Ufugaji Nyuki.
Wizara inawakumbusha wafanyabiashara taratibu za kufuata ili kuuza mazao ya nyuki nchi za nje:
- Awe na Kampuni ya biashara iliyosajiliwa;
- Awe amesajiliwa kama mfanyabiashara wa mazao ya nyuki;
- Awe na leseni halali ya Biashara;
- Awe na kitambulisho cha mfanyabiashara (TIN);
- Awe amepata umepata soko nchi za nje na kuonyesha bei yake;
- Ubora wa mazao yake yahakikiwe na Wizara ya Maliasili na Utalii na kupewa kibali cha kusafirisha nje ya nchi.
Inasisitizwa kuwa wafanyabiashara wote wanatakiwa kupata kibali cha kusafirisha asali nje ya nchi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
Tarehe 21 Septemba 2011
No comments:
Post a Comment