Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu amekemea kitendo cha mkandarasi wa ujenzi wa barabara kutoka Namtumbo kwenda Tunduru unaofanywa na kampuni ya M/S Progressive Higleig JV kutoka India kuwa na kasi inayotia shaka
Amesema hayo wakati akifungua Kikao cha bodi ya barabara mkoa wa Ruvuma kilichofanyika leo katika ukumbi wa Songea Club mjini Songea
Alisema mradi wa ujenzi wa barabara ya Namtumbo hadi Tunduru ni sehemu ya mpango wa serikali kuhakikisha kuwa ukanda wa Maendeleo ya Mtwara unaunganishwa kwa lami kutoka bandari ya Mtwara hadi bandari ya Mbambabay
Aliongeza kuwa mradi huo unahusisha ujenzi wa barabara kwa iwango cha lami yenye urefu wa kilometa 193 ambapo kazi ya ujenzi ilipaswa kuanza Machi mwaka huu na utakamilika Mei 2013 lakini hadi sasa hata vifaa muhimu kwa kazi hiyo havijaletwa.
“Hadi mimi nakwenda kutembelea mradi husika hivi karibuni ndio mkandarasi anaanza kutoka usingizini kwa kuanza kusafisha msitu hii haikubaliki hata kidogo kwani watu hawa kuachiwa kufanya uzembe huu” alisema Mkuu wa mkoa
Mwambungu alisisitiza ya kwamba hafurahishwi hata kidogo na kazi ya mkandarasi Progressive kwani kuna uwezekano mkubwa wa kazi kutokamilika kwa wakati yaani miezi 27 hivyo akaeleza kuwa anawasiliana na wizara ya ujenzi kuona hatua za kuchukua dhidi mkandarasi
Akielezea mafanikio ya serikali katika Kuboresha Miundombinu Mwambungu alisema kuwa lengo la serikali ni kuunganisha maeneo yote kwa barabara yenye kiwango cha lami
Alisema kwa mkoa wa Ruvuma kazi ilianza mwaka jana kwa miradi ya ujenzi wa barabara kutoka Mbinga –Peramiho (km 78) unaendelea,Songea –Namtumbo (km 67) kazi inaendelea na Namtumbo-Tunduru (km 193) kazi imeanza hivi karibuni
Aidha kwa upande wake Meneja wa TANROADS mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ibrahim Kisimbo alikiambia Kikao kuwa mradi huo wa Namtumbo hadi Tunduru unakadiliwa kugharimu shilingi bilioni 180 ambazo ni ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDP),shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na serikali ya Tanzania
Katika hatua nyingine mkuu wa mkoa amekemea tabia ya Halmashauri za wilaya na Manispaa mkoani kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha chini kwa kigezo cha fedha kidogo kuwa halikubaliki
“Fanyeni kazi zenu kwa kuhakikisha ubora wa miradi unaendana na thamani ya fedha iliyotolewa “ na kuongeza kuwa wakumbuke kuwa wakaguzi wakuu wa kazi za ujenzi wa barabara ni wananchi hivyo tusiwaangushe kwa kusimamia miradi yenye ubora hafifu alisema Mkuu wa mkoa
Mkoa wa Ruvuma una mtandao wa barabara kiasi cha kilometa 5,485.59 ambapo kilometa 219.93 ni za lami na zilizobaki ni za changalawe na udongo