Serikali ya Tanzania iliamua kupitisha Sheria ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa kila mtu kwa kuchangia kidogo ili kumuwezesha mwanachi kutibiwa hata kama hana fedha pindi anapougua.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Iringa, Dr. Christine Ishengoma, katika hotuba yake ya ufunguzi wa kongamano la wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wa Mikoa ya Iringa na Njombe uliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Highland, Manispaa ya Iringa.
Dr. Ishengoma amesema “lengo kuu wa kupitishwa kwa Sheria hii ilikuwa ni kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa kila mtu kwa kuchangia kiwango kidogo kabla ya kuugua, ili anapougua aweze kutibiwa hata kama hatakuwa na fedha za kulipia wakati huo”. Amesema kutokana na gharama za matibabu kuwa juu jambo linalomuwia ugumu mwananchi wa kumudu, ndio msingi ulioifanya Serikali kuanzisha utaratibu wa mwananchi kulipia gharama za matibabu kabla ya kuugua kwa utaratibu wa Bima. Amesema ili utaratibu huu uwe mahususi Serikali ilitunga Sheria inayoanzisha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii.
Mkuu wa Mkoa amesema kuwa afya bora ni jambo muhimu sana kwa wananchi na ndio chachu ya wananchi kujiletea maendeleo kutokana na uzalishaji sababu kama wananchi hawatakuwa na afya nzuri na imara uzalishaji utashuka na jamii kuendelea kuwa masikini. Amesema kuwa familia inayosumbuliwa na maradhi muda mwingi haiwezi kuzalisha mali.Amesema suluhisho lake ni familia kuwa na uhakika wa matibabu pindi wakiugua, ni vema kuhimiza wananchi kujiunga na Mifuko ya afya ya Jamii katika Halmashauri.
Dr. Ishengoma alionesha kusikitishwa sana na takwimu zinazoonesha kuwa kati ya mwezi Desemba, 2009 na Desemba, 2011 jumla ya shilingi bilioni 3.5 zililipwa na serikali kwa Halmashauri nchini kama tele kwa tele. Kati ya fedha hizo mikoa ya Iringa na Njombe haijaambulia chochote.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Aseri Msangi amewataka viongozi wa bima ya afya katika ngazi za mikoa kuwasilisha taarifa zao katika ofisi ya waku wa wilaya na mikoa ili ziwawezeshe kupanga ratiba za ufuatiliaji na kuhamasisha uhamasishaji kwa wananchi ili mfuko huo wa afya ya jamii iweze kuwa na manufaa na endelevu. Aesema pia changamoto ya mawasiliano na uelewa mdogo pia inahitaji kuangaliwa kwa jicho la karibu na wadau wa bima ya afya kwa lengo la kupanua uelewa wao na wananchi kwa ujumla.
Kaimu Mkurugenziwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Immaculate Senje, amesema kuwa ili mfuko wa Afya ya Jamii uweze kuwanufaisha wananchi wengi, suala la uhamasishaji jamii linahitaji kupatiwa uzito unaostahili. Amesema kuwa wananchi wapo tayari hasa pale wanapohamasishwa na viongozi na kupatiwa taarifa sahihi hasa manufaa yanayotokana na kujiunga na mfuko huo.
No comments:
Post a Comment