WAANDISHI HABARI HAMASISHENI SENSA
Mkuu wa Mkao wa Iringa amewataka waandishi wa
habari, viongozi wa dini na wazee mashuhuri Mkoani Iringa kuhamasisha wananchi
juu ya uelewa wa Sensa ya watu na Makazi ili waweze kujitokeza na kuhesabiwa
hapo Agosti 26, 2012.
Wito huo ameuto Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt.
Christine Ishengoma katika taarifa yake aliyoitoa kwa waandishi wa habari,
viongozi wa dini, wazee mashuhuri na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu
uhamasishaji wa wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi leo
alipokutana nao katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Dkt. Christine amesema kuwa kutokana na umuhimu wa
Sensa ya Watu na Makazi nchini, nafasi za makundi mbalimbali ni muhimu sana
katika kusaidia kutoa elimu na hamasa, amesema “hamna budi kufahamu kuwa
takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ndizo zitakazoiwezesha Serikali kutambua
hali halisi na mahitaji halisi ya huduma zilipo katika maeneo yenu hivyo
kuingizwa katika mipango ya maendeleo ya taifa”.
Amesema kutokana na msingi huo makundi hayo
aliyokutana nayo yanapaswa kuhamasisha wananchi ili waweze kuhesabiwa na
kusisitiza kuwa kuhesabiwa huko iwe ni mara moja tu kuwezesha takwimu
zitakazokusanywa ziwe sahihi na za uhakika. Amesema kuwa iwapo takwimu zote
zitakazokusanywa zitakuwa sahihi, huo ndio utakuwa utimilifu wa takwimu za
Sensa kitaifa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa mambo muhimu
ya kuzingatia wakati ya kuhamasisha wananchi ni pamoja na tarehe ya Sensa,
umuhimu wa Sensa na yatakayojiti wakati wa zoezi la kuhesabu watu.
Akiwatoa hofu wananchi kuhusu mawazo potofu dhidi
ya zoezi la Sensa, Mratibu wa Sensa Mkoa wa Iringa, Fabian Fundi amesema kuwa
zoezi la Sensa ya Watu na Makazi halihusiani kabisa na hofu walizonazo
wananchi. Amesema “ni muhimu sana kuwatoa hofu wananchi kwa kuwaelimisha kuwa
zoezi la Sensa halihusiani kabisa na hofu au imani walizonazo”.
Fundi, amesisitiza kuwa wananchi wawe huru kutoa
taarifa watakazoulizwa katika dodoso na kuwahakiihsia kuwa taarifa hizo
zitatumika kwa mambo ya kitakwimu pekee na kwa usiri mkubwa.
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka
amesema amewataka wananchi kuwatoa watoto wote na watu wenye ulemavu ili waweze
kuhesabiwa na kuiwezesha Serikali kuangalia njia bora ya kuwahudumia vizuri
zaidi. Aidha, amekemea tabia ya baadhi ya wanajamii kuwaficha watoto wenye
ulemavu katika shughuli mbalimbali kutokana na ulemavu walionao.
=30=
No comments:
Post a Comment