Friday, May 25, 2012


WAKUU WA WILAYA WAAPISHWA IRINGA

IRINGA

Wakuu wapya wa Wilaya Mkoani Iringa wametakiwa kuwa karibu na wananchi katika wilaya zao ili kuweza kuzifahamu changamoto zinazowakabili na kuwahudumia kwa ufanisi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma muda mfupi baada ya kuwaapisha wakuu wapya wa wilaya za Mufindi, Iringa na Kilolo.

Dkt. Christine amesema kuwa ili kuweza kuwahudumia vizuri wananchi ni lazima kuzifahamu changamoto zinazowakabili wananchi husika. Amesema ili kuzifahamu changamoto hizo ni lazima kuwa nao karibu na baada ya kuzifahamu changamoto hizo na rahisi kuweza kuwahudumia kwa urahisi na ukaribu.

Amesema kuwa mkoa wa Iringa unasifika kwa ustadi katika shughuli za kilimo kwa mazao ya chakula na biashara ambazo ndizo shughuli kuu za uchumi. Amesema kuwa kilimo kinaajiri karibu asilimia 85 ya wakazi wa mkoa wa Iringa na kuchangia zaidi ya asilimia 50 ya pato la mkoa.

Akiongelea matarajio yake kwa wakuu hao wa wilaya, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa kwa kipindi mkoa umekuwa na upunguwa wa wakuu wa wilaya, hivyo uteuzi huo utawezesha kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi katika mkoa wa Iringa.

Akielezea matarajio yake, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu amesema kuwa ushirikiano alioupata kutoka kwa wananchi wa Wilaya ya Mufindi ulimuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na jukumu lakekama Mkuu wa Wilaya kuwa rahisi. Amesema anatarajia ushirikiano huo kuendelea kwa kasi zaidi ili wote kwa pamoja waweze kusukuma mbele gurudumu la maendeleo katika Wilaya ya Mufindi na Mkoa wa Iringa kwa ujumla.

Ikumbukwe kuwa Rais Jakaya Kikwete aliteua wakuu wapya wa Wilaya tarehe 09 Mei, 2012 na mkoa wa Iringa kupata wakuu watatu wa wilaya. Wakuu hao na wilaya zao katika mabano ni Evarista Njilekiro Kalalu (Mufindi), Dkt. Leticia Moses Warioba (Iringa) na Gerald John Guninita (Kilolo). 
=30=

No comments:

Post a Comment