Friday, May 25, 2012


WAFANYAKAZI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA JUHUDI 

MUFINDI
Serikali Mkoani Iringa imewataka Wafanyakazi Mkoani hapa kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na nidhamu ili kujiletea maendeleo katika kazi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake ya Siku ya Wafanyakazi Duniani iliyofanyika katika ngazi ya Mkoa Wilayani Mufindi.

Dkt. Christine amesema ili mfanyakazi yeyote aweze kuheshimika katika jamii, inampasa kuelewa umuhimu wa nafasi yake katika jamii, kwa kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na nidhamu na kujituma kazini kwake, bila ya kufuatwafuatwa”. Kwa waajiri amesema “mwajiri anao wajibu mkubwa wa kutoa vitendea kazi bora, kujali usalama wa wafanyakazi na kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wafanyakazi wake”.

Akiongelea wajibu wa vyama vya wafanyakazi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa vyama hivyo vinawajibika kuwaelimisha wananchama wao ambao ni watumishi wa Serikali, taasisi, mashirika mbalimbali, wafanyakazi wa hoteli na wafanyakazi wengine juu ya kuheshimu nafasi waliopewa katika jamii na kuelewa msingi wa ufanyakazi bora wa umma. Amesema miongoni mwa wajibu huo ni kuelimisha juu ya sheria, taratibu na kanuni za kazi, kufanya kazi kwa hekima na uadilifu, kuheshimu maadili na taaluma, kutunza siri za serikali, kutekeleza wajibu wake kama wafanyakazi,pasipo upendeleo.

Akiongelea kero dhidi ya wafanyakazi, Dkt. Christine amesema kuwa serikali imeendelea kutatua kero nyingi zinazowakalibi wafanyazi katika utendaji kazi wao. Amesema “hapo awali kulikuwepo kero nyingi zinazohusu wafanyakazi, kama vile ucheleweshaji wa mishahara, ucheleweshaji wa malipo kwa wastaafu, kero ya kutopata mikopo kwenye benki”. Amesema kuwa hali hiyo kwa sasa imerekebishwa na wafanyakazi ni mashahidi. Aidha, amekiri kuwa maboresho haya hayajafikia kiwango cha asilimia mia moja.

Akiongelea Sensa ya watu na makazi, Dkt. Christine amewataka wafanyakazi wote kushiriki kutoa taarifa na elimu kwa wananchi dhidi ya sensa ya watu na makazi itakayofaanyika tarehe 26 Agosti, 2012. amesema kuwa lengo la Sensa hii ni kupata idadi ya watu wote katika nchi, kwa umri na jinsi, mahali wanapoishi, hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo na hali ya makazi. Amesema sensa hiyo ni muhimu sana kwa sababu inalenga kutathmini utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Mkakati wa Kupunguza Umasikini na kukuza Uchumi Tanzania (MKUKUTA) na mpango wa Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA). Napenda kuwahamasisha wananchi wote kujitokeza kwa wingi na kutoa taarifa zao kwa usahihi ili kufanikisha zoezi hilo.

Maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yalianza katika karne ya 19 huko ulaya wakati wafanyakazi kwenye viwanda vya nguo na vingine walipoamua kudai maslahi na mazingira bora ya kufanyia kazi. Maandhimisho hayo mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘mshahara duni, kubwa kubwa na mfumuko wa bei ni pigo kwa wafanyakazi’.
 =30=  



SERIKALI KUTATUA KERO ZA WAFANYAKAZI 

MUFINDI

Serikali itaendelea kutatua kero za wafanyakazi ili kuwawezesha wanyakazi kufanya kazi katika mazingira bora na rafiki ili wazidishe ufanisi katika utendaji kazi wao.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akiongea na wafanyakazi wa Mkoa wa Iringa katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yaliyofanyika kimkoa mjini Mafinga wilayani Mufindi.

Dkt. Ishengoma amesema kuwa hapo awali zilikuwepo kero nyingi zilizokuwa zikiwakabili wafanyakazi, nakuzitaja kero hizo kuwa ni ucheleweshaji wa malipo kwa wastaafu, ucheleweshaji wa mishahara, na kero ya kutokupata mikopo katika benki. Amesema “hali hii sasa imerekebishwa na wafanyakazi ni mashahidi wa haya ninayoyazungumza, ingawa maboresho haya hayajafikia kiwango cha asilimia mia moja”. Amesema “kero inayoendelea hivi sasa ni suala la mishahara duni iliyo na kodi kubwa ambayo haiendani na hali ngumu kiuchumi inayoikabili nchi yetu.  Serikali inalitambua hilo na inaendelea kulifanyia kazi ili kuipatia ufumbuzi wa kudumu”.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa lazima wafanyakazi watambue nafasi yao katika jamii na kuwataka kufanya kazi kuwa juhudi, nidhamu na maarifa na kujituma kazini pasipo kufuatwafuatwa. Amesema kufanya hivyo kutawafanya wafanyakazi kuheshimika katika jamii. Amewataka waajiri kuendelea kutoa vitendea kazi bora na kutoa kujali usalama wa wafanyakazi wote ili kuboresha utendaji kazi wao.

Aidha, Dkt. Ishengoma amevitaka vyama vya wafanyakazi kuwajibika kuwaelimisha wanachama wao ambao ni watumishi wa Serikali, Taasisi, Mashirika mbalimbali, Watumishi wa hotelini na Majumbani pamoja na Wafanyakazi wengine juu ya kuheshimu nafasi waliyopewa katika jamii na kuelewa msingi wa utumishi bora kwa Umma.

Akiongelea mchakato wa uundwaji wa Katiba Mpya, Mkuu wa Mkoa amewataka wafanyakazi wote kushiriki katika kuhamasisha na kuwaeleza wananchi ili washiriki katika mchakato huo kwa kutoa elimu. Amesema “napenda kutoa wito kwa wananchi wote kuwa huru kutoa maoni yenu kwa Tume itakapopita na kukusanya maoni yenu”.

Chimbuko la maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniali lilianza karne ya 19 huko ulaya na mwaka huu Kauli Mbiu ya Maadhimisho haya ni ‘maisha duni, kodi kubwa na mfumuko wa bei ni pigo kwa wafanyakazi’.

=30=



No comments:

Post a Comment