Friday, May 25, 2012



SENSA YA WATU NA MAKAZI KUTELA MAENDELEO
MUFINDI
Sensa ya Watu na Makazi inaumuhimu sana katika kutathmini utekelezaji wa mipango mikubwa ya maendeleo inayolenga kukuza uchumi na kupunguza umasikini.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akiwasilisha taarifa ya Mkoa wa Iringa katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kijiji cha Igomaa, Wilaya ya Mufindi.

Dkt. Ishengoma amesema kuwa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 ina umuhimu wa kipekee kwa sababu inalenga kutekeleza mipango ya kupunguza umasikini nchini. Amesema “Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 ina umuhimu wa kipekee kwani mbali ya kutimiza malengo ya kawaida, takwimu zitakazokusanywa katika Sensa hiyo zitatumika katika kutathimini utekelezaji wa mipango yetu mikubwa ya maendeleo ambayo ni Mpango wa kupunguza umasikini na kukuza uchumi Tanzania (MKUKUTA, na Mpango wa kukuza uchumi Zanzibar (MKUZA)”.

Amesema takwimu za Sensa ya Watu na Makazi 2012 manufaa yake ni makubwa sana katika mipango ya maendeleo ya Mkoa wa Iringa na kusaidia kufanya mipango sahihi ya maendeleo kulingana na mahitaji halisi sambamba na kuweka uwiano mzuri wa matumizi ya rasilimali kulingana na idadi ya watu katika Mkoa.

Akiongelea maandalizi ya Sensa hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa Mkoa umekuwa ukichukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linafanikiwa kwa ufanisi. Amezitaja hatua hizo kuwa ni uhakiki na utengaji wa maeneo madogo madogo ya kuhesabia watu na uhamasishaji wa ushiriki wa jamii katika Sensa.

Mwenge wa Uhuru umeanza mbio zake katika Mkoa wa Iringa ambapo unatarajiwa kukagua, kuzindua, kufungua na kuweka mawe ya msingi miradi 48 yenye thamani ya shilingi bilioni 1,867,759,277.
=30=


MUFINDI

Wananchi wa Mkoa wa Iringa wamefahamishwa kuwa wanawajibu wa kuenzi misingi iliyowekwa na waasisi wa Taifa iliyoifanya nchi iwe na amani na utulivu jambo linalowawezesha wananchi kutekeleza shughuli za kujiingizia kipato kwa ufanisi mkubwa.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akitoa taarifa ya mkoa wa Iringa katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kijiji cha Igomaa wilayani Mufindi.


Dkt. Christine amesema kuwa “watanzania tunao wajibu wa kuwaenzi waasisi wa Taifa letu na kwa kuweka misingi mizuri ambayo imeendelea kulifanya Taifa letu kuwa mfano wa kuigwa na mataifa mengine katika kudumisha amani, umoja wa kitaifa na mipango mizuri ya maendeleo. Hatuna budi kudumisha na kuendeleza tunu hizi kwa maendeleo na ustawi wa Taifa letu”.


Akiongelea mapambano dhidi ya dawa za kulevya, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa Mkoa wa iringa unaendelea na jitihada za kuhamasisha wananchi katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, kwa kutumia mpango wa polisi jamii na ulinzi shirikishi. 



Amesema kuwa Mkoa wa Iringa umeendelea kuendesha misako mbalimbali mijini na vijijini kwa malengo ya kuvunja vijiwe vya wauzaji wa dawa za kulevya na kukamata wamiliki wa mashamba ya bangi na kuyateketeza.  “Katika mapambano haya tayari jumla ya kesi 52 kati ya mwaka 2011 na 2012 za kupatikana na dawa za kulevya zimefikishwa mahakamani ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa” amesema Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Serikali ya Mkoa imeendelea kutoa elimu juu ya uanzishaji wa vikundi vya uzalishaji mali na kuhamasisha vijana kujihusisha na michezo mbalimbali ili kuepukana na matumizi na biashara ya dawa za kulevya ukiwa ni mkakati kulitokomeza kabisa tatizo hili la dawa za kulevya.


Akiongelea mapambano dhidi ya rushwa, Dkt. Christine amesema kuwa mapambano dhidi ya rushwa katika Mkoa wa Iringa yanafanyika kwa kuzingatia Mkakati wa Kitaifa wa kupambana na rushwa awamu ya pili. Ameseme “mkakati huu unalenga kuongeza ufahamu kwa wananchi juu ya rushwa, kuongeza wigo wa mapambano dhidi ya rushwa, kuboresha huduma za jamii na kuongeza uwezo wa ushiriki wa sekta binafsi na taasisi zisizo za kiserikali katika mapambano hayo”.


Amesema kupitia mpango huo Mkoa wa Iringa umeweza kusambaza jumla ya machapisho 16,488 yenye ujumbe wa mapambano dhidi ya rushwa ambayo yamekuwa yakigawiwa katika semina 77, mikutano ya hadhara 27 na mijadala ya shule za sekondari.


Mwenge wa Uhuru umeanza mbio zake Mkoani Iringa ambapo utapitia jumla ya miradi ya maendeleo 48, kuweka mawe ya msingi, kukagua, kuzindua na kufungua miradi hiyo yenye thamani ya shilingi bilioni 1,867,759,277.

=30=


No comments:

Post a Comment