UKUAJI WA UCHUMI UZINGATIE UHIFADHI WA MAZINGIRA
IRINGA
Serikali imeihimiza dhana ya ukuaji
wa uchumi kuzingatia matumizi endelevu ya rasilimali yasiyoathiri mazingira kwa
kuzingatia athari za muda za muda mrefu kwa mazingira kwa faida ya vizazi
vijavyo.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohamed Gharib Bilal alipokuwa
akihutubia uzinduzi wa jukwaa la uchumi wa kijani uliofanyika katika ukumbi wa St. Dominic mjini
Iringa.
Dkt. Bilal amesema “matumizi yasiyo
endelevu ya rasilimali hauna manufaa katika dunia ya leo. Watu wanapaswa
kuachana na mbinu za kizamani za ukuaji wa uchumi wa matumizi shinikizi ya
rasilimali, ambapo maendeleo yamekuwa yakigharimu mazingira; badala yake,
wanapaswa kufuata mbinu mpya ambazo tija huongezwa kwa kutumia na kusimamia
maliasili kwa ufanisi zaidi”.
Amesema kuwa shughuli za kujiletea
uchumi lazima ziangalie kwa makini athari za muda mrefu kwa mazingira na haja
ya kuhifadhi urithi wa nchi kwa manufaa ya vizazi kilichopo na vizazi vijavyo.
Amesema kuwa uchumi wa kijani ni muhimu kwa sababu huchochea ukuaji wa uchumi,
mapato na ajira. Amesisitiza kuwa hii ndiyo aina ya uchumi inayoleta maendeleo
ya kiuchumi ya muda mrefu na yanayotoa fursa kwa wananchi wengi.
Makamu wa Rais amesema kuwa katika
sekta mbalimbali kama kilimo, ujenzi, misitu
na usafiri, uchumi wa kijani ndio uchumi unaotengeneza ajira nyingi kuliko
ajira zilizopo katika hali ya kawaida. Ametolea mfano wa sekta ya uvuvi,
“uchumi wa kijani utalazimisha kushuka kwa mapato na ajira katika muda mfupi na
wa kati ili kujazia hifadhi asilia, lakini hali hii hubakia ya muda mfupi na
baadaye sekta hukua na kutoa tija kubwa wananchi”.
Dkt. Bilal amesema kuwa ili jitihada
za maendeleo ziweze kufanikiwa nchini, lazima zielekezwe katika uhalisia wa
mambo. Amesema “zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wan chi hii huishi vijijini.
Hivyo, jitihada madhubuti za kupunguza umasikini na kuleta maendeleo lazima
zilenge wakazi na uchumi wa vijijini ili kuwa na matokeo mazuri”.
Amesema kuwa upo uhusiano mkubwa wa
wananchi masikini wa vijijini na mazingira yao kwa sababu huishi karibu na
mazingira ya asili na hutegemea rasilimali za ardhi, maji na misitu kwa maisha
yao.
Katika salamu za Mkoa wa Iringa
zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amesema kuwa
zoezi la kupanda miti na kuhakikisha inatunzwa ni mkakati shirikishi
unaowashirikisha wananchi na taasisi mbalimbali. Kila Halmashauri inazingatia
agizo la serikali la kuwa na uzalishaji wa miche ya miti kwenye vitalu vyake
isiyopungua miche 1,500,000 kila msimu. Amesema kwa miaka mitano iliyopita
Mkoauliweka malengo ya kupanda miti 197,910,000 na kufanikiwa kupanda miti
266,871,064.
Akiziainisha changamoto
zinazokwamisha juhudi za kutunza na kuhifadhi mazingira amezitaja kuwa ni
uchomaji moto ovyo, ukataji miti ovyo bila kufuata kanuni na kulima kwenye
vyanzo vya maji na miteremko mikali.
Jukwaa la uchumi la kijani
linaratibiwa na taasisi ya Uongozi kwa lengo la kuwa na uchumi endelevu nchini.
=30=
No comments:
Post a Comment