Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma
amewataka wananchi wa mkoa huo kutumia fursa ya maadhimisho ya siku ya utalii
duniani yanayofanyika kimkoa katika manispaa ya Iringa kutembelea maonesho hayo
na kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo ili kuweza kupata elimu na
taarifa z utalii.
Wito huo ameutoa katika hotuba yake ya ufunguzi wa
maadhimisho ya siku ya utalii duniani yanayofanyika kimkoa katika uwanja wa
Samora, Manispaa ya Iringa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (wa kwanza kulia) akiwa katika moja ya mapango ya kihistoria katika kuhamasisha utalii wa ndani.
Dkt. Christine amesema “natoa wito kwa wananchi wote kutumia fursa hii
kutembelea maonesho na kushiriki katika
shughuli mbalimbali za maadhimisho haya”.
Amesema maonesho hayo yatatoa fursa ya kufahamiana
na kupanua wigo wa kufanya biashara za utalii. Amesema kuwa maadhimisho yatahusisha
maonesho ya bidhaa na shughuli mbalimbali za kitalii, michezo, kutembelea
vivutio vya kitalii vilivyopo mkoani Iringa na kutoa elimu kuhusu uendeshaji wa
biashara za utalii.
Akielezea madhumuni ya maadhimisho hayo, Mkuu wa
Mkoa wa Iringa amesema kuwa madhumuni ya maadhimisho hayo ni Kutoa umuhimu wa sekta
ya utalii kwa maendeleo ya mwanadamu katika nyanja mbalimbali. Amezitaja nyanza
hizo kuwa ni pamoja na utamaduni, uchumi, mazingira pamoja na nyingine.
Dkt. Christine amesema kuwa matokeo ya maadhimisho
hayo hayawezi kuonekana kwa muda mfupi kwa sababu ni suala linalohitaji hamasa
ya muda mrefu. Ameelezea matumaini yake kuwa Mkoa wa Iringa utazidi kuendeleza
kwa kasi iliyopo, ukuaji wa utalii na hatimae wananchi kunufaika na utalii huo.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa mkoa wake
umejaaliwa kuwa na vivutio Vinci vya utalii ambavyo bado havijafahamika sana
kwa wananchi na wadau wengine. Amevitaja vivutio vilivyopo kuwa ni pamoja na mila
na desturi za watu wa ukanda huo, maeneo ya hifadhi za mimea na wanyama,
mandhari nzuri na za kuvutia, maeneo ya kilimo, maporomoko ya maji na maeneo ya
kihistoria.
Nae mwenyekiti wa Kamati ya kuendeleza utalii kwa
mkoa wa Iringa ambae pia ni katibu Tawala msaidizi, Sehemu ya Uchumi na Sekta
za Uzalishaji, Adam Swai amesema kuwa malengo mahususi ya kufanya maadhimisho
katika manispaa ya Iringa ni kuhamasisha wadau mbalimbali kutambua umuhimu wa
sekta ya utalii katika kujiletea maendeleo. Ameyataja maadhimisho hayo kuwa ni chachu
ya kuendeleza sekta ya utalii katika ukanda wa Kusini ili wananchi waweze
kufaidika na utalii huo.
Ikumbukwe kuwa Mkoa wa Iringa ulitangazwa na
serikali kuwa kutovu cha kuendeleza utalii kwa Ukanda wa kusini mwaka 2009.
aidha, maadhimisho hayo yatafanyika kwa siku tatu, kuanzia tarehe 25 hadi 27
Septemba 2012.
=30=
No comments:
Post a Comment