Wafanyakazi
mkoani Iringa wametakiwa kufanya kazi kwa kujituma na kusimamia vizuri
rasilimali zilizopo ili ziweze kuwanufaisha wananchi wengi na hatimae kujiletea
maendeleo yanayopimika.
Kauli
hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma katika nasaha
zake alizozitoa katika tafrija ya kumuaga Katibu Tawala Mkoa aliyestaafu Gertrude
Mpaka baada ya kuutumikia Umma kwa zaidi ya miaka 36 na kuukaribisha mwaka 2013
iliyofanyika katika ukumbi wa St. Dominic Manispaa ya Iringa.
Dkt.
Christine amesema “kwa kuwa tunaukaribisha mwaka 2013, natoa rai kwa watumishi
wenzangu kuwa kila mmoja kwa nafasi yake awe msimamizi mzuri wa rasilimali
mbalimbali tulizonazo”. Amewataka wafanyakazi kufanya kazi kwa kutenda haki
katika maeneo yao ya kazi na kuipiga vikali rushwa kwa sababu ni adui wa haki.
Amewataka
wafanyakazi kufanya kazi kwa kujituma na kujiwekea malengo yanayopimika ili
kuhakikisha utendaji kazi unakuwa wa kiwango cha juu hasa katika kutoa huduma
kwa wananchi.
Mkuu
wa Mkoa amesisitiza suala la kudumisha amani ili taifa liendelee kuwa na
utulivu. Amesema mahali penye amani maendeleo hujidhihirisha kwa sababu
wananchi wanakuwa huru kufanya kazi za maendeleo.
Katika
risala ya watumishi kwa Katibu Tawala Mkoa mstaafu, iliyosomwa na Kaimu Katibu
Tawala Mkoa, Wamoja Ayubu amesema amempongeza kwa utumishi wake uliotukuka na
kusema kuwa ataendelea kuwa mfano mzuri wa kuigwa kwa watumishi wote katika
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na mkoa wa Iringa kwa ujumla.
Amesema “tumefanya kazi pamoja
kwa muda mrefu sana, kwa upendo na ushirikiano mkubwa na kwa kufuata taratibu
na kanuni zilizopo kwa weledi katika utumishi wa Umma”. Amesema kuwa
ushirikiano wake uliusaidia mkoa wa Iringa kufanya kazi kwa ufanisi na kupiga
hatua kimaendeleo na kuwa mfano wa kuigwa kwa mikoa mingine.
Tofauti
na utendaji kazi wa Gertrude, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa amezitaja sifa
za kipekee alizokuwa nazo Katibu Tawala mstaafu kuwa ni mahusiano na
ushirikiano mzuri kwa watumishi wote pasipo kujali nafasi zao. Wamoja amesema
“hukuwa na ubaguzi kwa watumishi na ulihakikisha kuwa watumishi wanakuwa na
mazingira mazuri ya kufanya kazi na kusimamia ujenzi wa Ofisi za Tarafa katika
Mkoa wa Iringa na Njombe. Ameitaja sifa nyingine kuwa ni wepesi wake katika
kushirikiana na watumishi wote wakati wa shida na raha.
Katika
hotuba ya Katibu Tawala Mkoa mstaafu, Gertrude Mpaka, alipongeza mafanikio
yaliyopatikana katika kuanzishwa kwa mkoa mpya wa Njombe na kuyaita kuwa ni
mafanikio makubwa yaliyotokana na ushirikiano mkubwa kutoka kwa watu
mbalimbali. Ameongelea mafanikio katika sekta za kilimo, mifugo, elimu, afya,
mazingira na maji.
Aidha,
Gertrude alitumia muda huo kuwaomba radhi wale wote aliowakosea kwa namna moja
au nyingine wakati akitekeleza majukumu yake. Amesema“nilikuwa nafanya kazi za
kuwahudumia wananchi nikiwa na wenzangu inawezekana kabisa kwamba wapo watu
ambao niliwakwaza au kuwaudhi kwa kauli au matendo yangu wakati wa utekelezaji
wa kazi zangu, kama wapo watu wa aina hiyo naomba kutumia nafasi hii kuwaomba radhi.
Sikudhamiria kumuudhi au kumkwaza mtu, kama ilitokea basi ni kwa bahati mbaya
naomba mnisamehe. Vivyo hivyo kwa upande wangu sina yeyote ambaye nina kinyongo
nae” alisisitiza Gertrude.
=30=
No comments:
Post a Comment