Friday, July 26, 2013

RS IRINGA YAPOKEA WATUMISHI WAPYA 9



Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa imepokea watumishi wapya tisa na kukamilisha mchakato wa ajira kwa lengo la kuimarisha na kuboresha utendaji kazi katika Mkoa.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Utawala na Rasilimali Watu, Scolastica Mlawi wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Sehemu ya utumishi na utawala kwa kipindi cha robo ya nne mwezi Aprili-Juni, 2013 katika kikao cha kamati ya mkoa ya kusimamia, kudhibiti na kuratibu mapato na matumizi ya serikali kwa robo ya nne, mwaka 2012/2013 kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa.

Scolastica amesema kuwa kwa Kipindi cha Aprili–Juni,  2013, Sekretarieti ya Mkoa  imepokea watumishi wapya tisa wa Kada mbalimbali za afya toka wizara ya afya na ustawi wa jamii na kukamilisha mchakato wa ajira na kuwapangia vituo vya kazi. Amewataja watumishi hao kuwa ni Fredrick Galcian (Daktari daraja II), Atupele Mwandiga (Daktari wa Meno II), Walter Munisi (Physiotherapia daraja II), Bi. Happy Mbilinyi (Afisa Muuguzi Msaidizi II), Despina Mbuta (Muuguzi daraja I), Lucy Mwonge (Afisa Muuguzi Msaidizi II), Lucy Bayo (Afisa Mteknolojia Maabara), Furaha Magubika (Muuguzi II), Thomas Lyapa (Daktari II) wote wamepangiwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa. Aidha, ameongeza kuwa watumishi wote wameingizwa kwenye mfumo wa taarifa za Kiutumishi na mishahara ili waweze kupatiwa cheki namba.

Amewataja watumishi waliohamia katika Sekretarieti ya mkoa wa Iringa kuwa ni Said Gharama Kinderu (Afisa Elimu Mkuu) aliyetoka Halmashauri ya Mji wa Masasi, John Xavery Kiteve (Afisa Ushirika Mkuu I) aliyetoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo na Christopher S. Mbata (Tabibu Mwandamizi) aliyetoka Wizara ya afya na ustawi wa jamii. 

Akiwasilisha kazi zilizotekelezwa na Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya utawala amesema kuwa ni kusimamia ulinzi na usalama ambapo alihakikisha kuwa mkoa unakuwa katika hali ya utulivu na amani. Katika kuhalilisha hali hiyo aliendesha vikao vya kamati ya ulinzi na usalama kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizopo. Kazi nyingine ni kuhamasisha shughuli za maendeleo katika vijiji, halmashauri na mkoa. Amesema kuwa katika jukumu hilo mkuu wa mkoa aliwahamasisha vijana kujiunga katika vikundi vya ufugaji nyuki, kilimo, ujasiliamali ili kujiongezea kipato. Aidha, aliwaagiza watendaji kuhakikisha wanatenga maeneo kwa ajili ya shughuli za vijana katika maeneo ya vijiji.

Shughuli nyingine Scolastica ameitaja kuwa ni kusikiliza na kutatua malalamiko ya wananchi, amesema kuwa mkuu wa mkoa kwa kushirikiana na wataalamu wa Sekretarieti ya mkoa waliweza kuyashughulikia malalamiko mbalimbali na kuyapatia ufumbuzi na hatimae kudumisha utawala bora.
=30=

No comments:

Post a Comment