Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine
Ishengoma ameitaka Mamkala ya Mapato Tanzania kuongeza kasi ya ukusanyaji wa
mapato ya Serikali ili kuongeza wigo wa utoaji huduma nchini.
Kauli hiyo ameitoa katika majumuisho
ya ziara ya Nanenane baada ya kutembelea mabanda ya maonesho likiwemo banda la
mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) yaliyopo katika uwanja wa Mwakangale, Uyole
Mbeya.
Dkt. Christine amesema kuwa mamlaka
ya mapato Tanzania inafanya kazi nzuri, lakini bado inatakiwa kuongeza kasi
katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Amesema kuwa Serikali bado inapoteza
mapato mengi kwa sababu mamlaka hiyo haijakusanya mapato kiasi cha kutosha. Aidha,
ameitaka mamlaka hiyo kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato ya Serikali ili
kuongeza wigo wa serikali katika kutoa huduma kwa wananchi wake.
Amesema kuwa katika kipindi hiki
ambapo serikali inaendelea kutekeleza mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN) ni
pamoja na kuongeza mapato ya ndani kwa ajili ya kuimarisha utoaji huduma kwa
wananchi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliyekuwa
mgeni rasmi katika siku ya mkoa wa Iringa katika maonesho ya Nanenane,
amewataka mamlaka ya mapato kuongeza kasi na mikakati ya kuwahamasisha wananchi
kudai risiti wanaponunua bidhaa ili kuziba mwanya wa upotevu wa mapato ya
Serikali. Katika kuimarisha elimu na hamasa kwa wananchi juu ya kudai risiti
wanaponunua bidhaa, Dkt. Christine ametaka viongozi na wadau wote kushirikiana
katika kutoa elimu hiyo. Amesema “jukumu hili si la TRA pekee, bali ni jukumu
letu sote.
Lazima viongozi wote na wadau mbalimbali kuhamasisha na kutoa elimu
kwa wananchi juu ya kudai risiti”. Amesema kuwa kwa kufanya hivyo tutapunguza
mwanya na hatimae kuondoa kabisa upotevu wa mapato ya serikali kwa njia hiyo.
Akiongelea hali halisi ya maonesho ya
Nanenane baada ya kutembelea mabanda,, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa,
Wamoja Ayubu amepongeza jinsi Halmashauri na wadau walivyojipanga katika kuonesha
bidhaa zinazozalishwa katika maeneo yao na shughuli mbalimbali zinazofanyika
katika maeneo yao. Aidha, ametoa wito kwa washiriki wote kutumia maonesho hayo,
si kuona tu, bali pia kujifunza juu ya matumizi ya teknolojia katika kukuza na
kuboresha kilimo na mifugo.
Maonesho ya Nanenane mwaka 2013
yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “zalisha mazao ya kilimo na mifugo kwa kulenga
mahitaji ya soko”.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. chrisrine Ishengoma (mwenye kofia) na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa Wamoja Ayubu wakipata maelezo katika Banda la TRA
=30=
No comments:
Post a Comment