Tuesday, August 6, 2013

VYUO VIKUU VYATAKIWA KUANDAA PROGRAMU ZA KILIMO




Vyuo vikuu nchini vimeshauriwa kuwekeza katika kuandaa program za shahada za kilimo na mifugo ili kuzalisha wataalamu wengi zaidi wa kilimo nchini.
 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma akisaini kitabu cha wageni katika banda la University Computing Cente
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alipotembelea maonesho ya Nanenane kanda ya Nyanda za Juu kusini yanayoendelea katika uwanja wa John Mwakangale mjini Mbeya.

Dkt. Christine amesema kuwa ni vizuri sasa vyuo vikuu vikawekeza katika kuandaa program za shahada za kilimo na mifugo ili kutayarisha wataalamu wengi zaidi katika kada hizo. Amesema kwa sasa chuo kinachotegemewa ni chuo kikuu cha Sokoine, pamoja na kuwa kinafanya vizuri, ni vizuri vyuo vingine vikaanzisha program hizo ili kuongeza wigo wa kuandaa wataalamu nchini. 

Aidha, ameshauri kuwa vyuo vikuu vyote vya ukanda wa Nyanda za Juu Kusini vishirikishwe ipasavyo katika maandalizi na maonesho ya Nanenane kutokana na nafasi yao muhimu katika uzalishaji wa wataalamu wa fani mbalimbali.

Akiongelea ushiriki wa Halmashauri za mkoa wa Iringa katika maonesho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa halmashauri hizo zinafanya vizuri ikiwa ni pamoja na kuonesha uhalisia wa shughuli zinazofanyika katika halmashauri zao. “Halmashauri za mkoa wa Iringa zinaonesha uhalisia wa shughuli zinazofanyika huko, hii ni hatua nzuri zaidi ukilinganisha na mwaka jana” alisisitiza Dkt. Christine.

Ametoa wito kwa wakulima wa pareto nchini kuongeza uzalishaji wa zao hilo kutokana na uhitaji wake katika soko kuwa juu tofauti na uzalishaji wake. Amesema kuwa kiwanda cha pareto nchini kipo kimoja tu wilayani Mufindi na kimekuwa kikifanya kazi chini ya kiwango kutokana na kutokuzalishwa kwa wingi kwa zao hilo.
=30=

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma aliyekaa akiangalia kielelezo toka UCC. Kushoto ni Kaimu RAS Wamoja Ayubu.

 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma aliyekaa akiangalia kielelezo toka UCC

No comments:

Post a Comment