Wananchi wametakiwa
kudumisha amani na umoja wa kitaifa kwa kuenzi juhudi za baba wa Taifa Mwalimu
Julius Nyerere alizoziweka wakati wa kuweka misingi ya Taifa kupitia mbio za
Mwenge wa Uhuru.
Kauli hiyo
imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma alipokuwa akiongea
na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru,
Kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na wiki ya vijana kitaifa
mkoani Iringa.
Dk. Christine
amesema kuwa wananchi wanawajibu wa kuhakikisha amani na umoja wa kitaifa
vinadumu na kuwa endelevu nchini. Amesema kudumisha amani na utulivu ni njia
mojawapo ya kuenzi misingi na kazi alizofanya baba wa Taifa Mwalimu Julius
Nyerere kwa Taifa la Tanzania. Amesema “sehemu yoyote yenye amani na utulivu,
yapo maendeleo kwa sababu wananchi wanafanya shughuli za maendeleo kwa uhuru,
hii ndiyo maana yam bio za Mwenge wa Uhuru” alisisitiza Dk. Christine.
Akiongelea ujumbe
wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2013, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa
mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2013, zimebeba ujumbe usemao: “watanzania ni
wamoja” wenye kaulimbiu “tusigawanywe kwa misingi ya tofauti zetu za dini,
itikadi, rangi na rasilimali”.
Amesema lengo la ujumbe huo ni kutoa msisitizo
kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuimarisha umoja na amani nchini. Amesema kuwa
ni ushahidi kwa nchi jirani unaonesha madhara ya kuichezea amani na kuongeza
kuwa ni rahisi sana kupoteza amani na umoja lakini ni vigumu sana kuirejesha.
Amesema kutokana na umuhimu huo, Serikali imeona ni vizuri kutumia mbio za
Mwenge wa Uhuru mwaka 2013 kuhimiza umoja wa kitaifa.
Akiongelea wiki ya
vijana kitaifa iliyoanza tarehe 08/10/2013, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa maonesho
hayo yameandaliwa vizuri ili yaweze kuwa na mvuto muda wote. Amesema kuwa
vijana kutoka nchi nzima wanashiriki katika maonesho hayo na kutoa rai kwa
vijana wote kutumia maonesho hayo kujifunza shughuli wanazofanya za kujiletea
kipato.
Ametoa wito kwa
wananchi wote kujitokeza kwa wingi kutembelea mabanda ya maonesho katika uwanja
wa shule ya msingi Mlandege kuanzia ufunguzi hadi kilele tarehe 14/10/2013.
Amesema kuwa
sambamba na maonesho hayo kutakuwa na midahalo ya vijana itakayofanyika kuanzia
tarehe 9/10/2013-13/10/2013 katika ukumbi wa chuo cha VETA itakayohusisha
vijana zaidi ya 300 kila siku. Amesema kuwa midahalo hiyo itarushwa na vyombo
vya habari na kuwataka vijana kushiriki kikamilifu katika midahalo hiyo.
=30=
No comments:
Post a Comment