Wednesday, October 9, 2013

TAARIFA YA MKUU WA MKOA WA IRINGA DKT. CHRISTINE ISHENGOMA KWA WAANDISHI WA HABARI




TAARIFA YA MKUU WA MKOA WA IRINGA KWA VYOMBO VYA HABARI KUELEZEA HATUA MBALIMBALI ZA MAANDALIZI YA SHEREHE ZA KILELE CHA MBIO ZA MWENGE WA UHURU, KUMBUKUMBU YA BABA WA TAIFA  NA WIKI YA VIJANA KITAIFA MWAKA 2013-MKOANI IRINGA

Utangulizi:
Mkoa wa Iringa uliteuliwa kuwa mwenyeji wa Sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya Baba wa Taifa na Wiki ya vijana kitaifa mwezi Septemba 2012. Mkoa uliupokea uteuzi huo.
Historia fupi ya Mwenge wa Uhuru nchini Tanzania.

Mwenge wa Uhuru Kabla ya Uhuru
Chimbuko la Mwenge wa Uhuru na Mbio za Mwenge wa Uhuru linatokana na Azimio alilolitoa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa Mwenyekiti wa TANU tarehea 22, Oktoba 1959 wakati akihutubia wajumbe wa Bunge la kikoloni lililojulikana kama LEGICO pale aliposema:

“Sisi (Watanganyika), tunataka kuuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo pale ambapo pana chuki, heshima ambapo pamejaa dharau.” 

Baada ya kupata Uhuru, Baba wa Taifa akiwa Rais wa Tanganyika alitimiza ahadi hiyo mwaka 1961 kwa kuuwasha Mwenge wa Uhuru na Kuupandisha juu ya Kilele cha mlima Kilimanjaro.
Maneno aliyoyatoa Baba wa Taifa mwaka 1959, yalikuwa ni yenye uzito mkubwa na yaliyojaa busara na hamasa kubwa. Kwani kupitia tamko lile Watanganyika walipata moyo wa kupigania Uhuru, hali kadhalika kujenga umoja, mshikamano na udugu miongoni mwa Watanganyika na Matokeo yake ni kupata Uhuru pasipo kumwaga tone lolote la damu.

Mwenge wa Uhuru baada ya Uhuru
Baada ya Uhuru, Mwenge wa Uhuru ulianza kukimbizwa nchi nzima ukiwa na malengo yaleyale ambayo ni Kuhimiza umoja, upendo, heshima kwa Watanzania wote, haki na umoja wa kitaifa. Aidha, kila Mwaka Mwenge wa Uhuru huwa na Kauli mbiu ambayo hubeba ujumbe maalumu kulingana na mahitaji na malengo ya Taifa katika Mwaka husika. Sambamba na ujumbe maalumu; Mwenge wa Uhuru hubeba ujumbe wa Kudumu ambao ni Mapambano dhidi ya Ukimwi, Mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya na Mapambano dhidi ya Rushwa. 

Aidha, Mwenge wa Uhuru umekuwa ukihimiza na kuchochea maendeleo ya wananchi. Kila mwaka Mwenge wa Uhuru umekuwa ukipita Mikoa yote nchini ukipitia miradi mbalimbali ya maendeleo na kuizindua, kuifungua, kuweka mawe ya Msingi na kuikagua. Jambo hili limechochea sana uibuaji wa miradi ya maendeleo ya umma na ya wananchi na uendelezaji wa miradi hiyo.

Ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2013:
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu 2013, Umebeba ujumbe usemao:  Watanzania ni wamoja” wenye kaulimbiu “Tusigawanywe kwa misingi ya tofauti zetu za dini, Itikadi, Rangi na rasilimali” 

Ujumbe huu, umeandaliwa kwa mwaka huu ili kutoa msisitizo kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuimarisha umoja na amani katika nchi yetu. 

Ndugu wananchi,
Ujumbe huu umebeba dhana kubwa sana, kwani sote tunafahamu umuhimu wa kudumisha amani na madhara ya kuchezea amani. Sote tunajionea nchi jirani zinazotuzunguka ambapo wamekuwa wahanga wa madhara yanayowapata kutokana na kuzembea kudumisha amani. Ni rahisi sana kupoteza amani na umoja lakini ni vigumu sana kurejesha amani, umoja na udugu uliopotea. Kutokana na umuhimu wa amani na umoja nchini, Serikali imeona  ni vema kutumia Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu 2013 kuhimiza Umoja wa Kitaifa.

Maadhimisho ya Sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya Baba wa Taifa na Wiki ya Vijana Kitaifa.

Ndugu wananchi,
Kama nilivyoeleza awali kwamba Mkoa wetu wa Iringa mwaka jana ulipewa heshima ya kuandaa sherehe za Kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya Baba wa Taifa na Wiki ya Vijana Kitaifa mwaka huu 2013, tulizipokea rasmi.

Sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Sherehe hizi zitafanyika katika Uwanja wa Samora tarehe 14 Oktoba, 2013. Kutakuwa na mambo mbalimbali ya kuvutia. Kutakuwa na Maonesho ya Halaiki, Burudani za vikundi vya sanaa, salaam na hotuba mbalimbali za Viongozi.

Kumbukumbu ya Baba wa Taifa
Baba wa Taifa Mwalimu Julius  Kambarage Nyerere alifariki tarehe 14 Oktoba, 1999; tangu kifo chake Maadhimisho ya sherehe za Kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na Kilele cha Maonesho ya Wiki ya Vijana zimekuwa zikiadhimishwa pamoja katika tarehe ambayo Baba wa Taifa alifariki. Tangu tarehe 8 hadi 14 Oktoba, 2013 kutakuwa na Maonesho ya Hotuba za baba wa Taifa, vitabu na makala mbalimbali zinazohusu maisha ya Baba wa Taifa wakati wa Uhai wake ambayo pia ni Wiki ya Vijana. Aidha, tarehe 14 Oktoba, 2013 saa 1.00 asubuhi kutakuwa na Ibada maalumu ya kumwombea Baba wa Taifa katika Kanisa Katoliki- Parokia ya Kihesa. Ninawaomba watu wote tushirikiane kila mmoja kwa imani yake kumwombea Baba wa Taifa.

Wiki ya Vijana Kitaifa
Maonesho ya Wiki ya Vijana yatafunguliwa na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Amos Makala (Mb.) tarehe 8 Oktoba, 2013 na kilele chake kitakuwa tarehe 14 Oktoba, 2013 ambapo Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atayapitia mabanda, kukagua na kuona shughuli za maonesho ya vijana. Maonesho ya vijana yatafanyika katika Uwanja wa shule ya Msingi Mlandege.

Maonesho haya yanavutia sana, kwa sababu vijana kutoka nchi nzima hushiriki kuonesha kazi zao mbalimbali wanazozifanya. Aidha, hii ni fursa kwa vijana wa Iringa kuonesha kazi zao pia kujifunza kwa vijana wenzao kutoka Mikoa mingine nchini na vikundi vingine kutoka Mikoani. Ninatoa Wito kwa Vijana na hususani Vikundi vya vijana kujitokeza kwa wingi kuomba nafasi ya kupewa maeneo ya kuonesha kazi zao. Pia ninatoa wito kwa wananchi wote wa mkoa wa Iringa kujitokeza kwa wingi kwenda kutembelea Mabanda ya maonesho katika uwanja wa shule ya Msingi Mlandege kuanzia tarehe 8 mpaka 14 mwezi huu wa kumi.

Midahalo ya Vijana
Ndugu wananchi,
Maonesho ya wiki ya vijana yataenda sambamba na  Midahalo ya Vijana ambayo itaanza tarehe 9 Oktoba, 2013. Midahalo hiyo itafanyika katika Chuo cha VETA ambapo vijana wapatao 300 watashiriki Midahalo hiyo. Katika midahalo hiyo Mada mbalimbali zitawasilishwa na washiriki kuchangia katika mada zitakazowasilishwa. Midahalo hiyo itarushwa na vyombo vya habari.  Natoa wito kwa vijana kufuatilia Midahalo hiyo kwa kushiriki kikamilifu na pia kwa kupitia vyombo vya habari ili kupata mafunzo mbalimbali ambayo yatawajenga katika maisha yenu.
Umoja na mshikamano wakati wa maadhimisho

Ndugu wananchi,
Sherehe hizi zinatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa kimataifa, kitaifa, Mikoa yote ya Tanzania, Mabalozi wa Nchi mbalimbali, wawakilishi wa taasisi mabalimbali za Kitaifa na Kimataifa watendaji wa Serikali na Vijana kutoka nchi nzima. Kutokana hali hiyo, hii ni fursa adhimu kwa Wananchi wa Iringa kuonesha zalendo wetu, upendo na ukarimu kwa wageni wote watakaokuwa Mkoani katika sherehe hizo, ili wakapotoka waukumbuke Mkoa wetu kwa mambo mazuri. Ninawaomba wananchi wote tushikamane pamoja kushirikiana na kujawa furaha na upendo wakati wote kama ilivyo kawaida yetu tufanikishe jukumu hili kwa amani na utulivu. Kila mmoja ajione ni sehemu ya kufanikisha sherehe hizi.

Ulinzi na Usalama
Ndugu wananchi,
Serikali yenu imejidhatiti vya kutosha kuhakikisha hali ya amani, utulivu na usalama wa watu na mali zao wakati wote wa maadhimisho haya. Vitendo vyovyote vya uharifu havitavumiliwa, wahusika wa vitendo hivyo watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Ninaomba wananchi wote tushirikiane kikamilifu na vyombo vyetu vya dola hususani jeshi la Polisi kuhakikisha kwamba vitendo vyovyote vya uharifu vinadhibitiwa. Penye shaka na tatizousichelewe kutoa ripoti kwa viongozi wahusika walio karibu na wewe.

Usafi wa Mazingira
Ndugu wananchi,
Sherehe hizi zitafanyika hapa Manispaa ya Iringa ambapo ndiyo makao makuu ya Mkoa, hivyo, hapa ndipo sura na sifa ya Mkoa huanza kuonekana. Ni kioo cha Mkoa mzima wa Iringa. Ninawasihi sana, ndugu wananchi, tujitahidi kufanya usafi na kuhakikisha Mazingira ambayo yanatuzunguka nayo masafi. Kila mmoja atazame mazingira yanayomzunguka na kuona kama kuna uchafu na afanye usafi. 

Ndugu wananchi,
Natoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Iringa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya ili kuonesha upendo na mshikamano wetu kwa Taifa letu kwa kujitokeza kwa wingi sana katika Maashimisho ya Sherehe hizi na hasa kilele tarehe 14 Oktoba, 2013 pale uwanja wa Kumbukumbu ya Samora.
Kwa wewe uliyenisikiliza nakuomba mueleze na mwenzio ambaye hakunisikiliza. 

Namalizia kwa kusema kumbuka kushiriki maadhimisho haya wewe mwenyewe, familia yako, rafiki yako na njoo uwanjani na wale wote waliokuzunguka.

Pamoja Tunajenga Iringa Yetu



No comments:

Post a Comment