Maadhimisho
ya wiki ya vijana yanalenga kuendeleza fikra za Mwalimu Julius Nyerere za
kuhamasisha amani na usawa katika jamii ili wananchi wajiletee maendeleo yao.
Hayo
yamesemwa na Katibu Mkuu- Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,
Sihaba Nkinga, akitoa maelezo mafupi kuhusu wiki ya vijana kitaifa mkoani
Iringa, yaliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya
vijana-Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, James Kajugusi katika
uwanja wa shule ya msingi Mlandege.
Sihaba
amesema kuwa serikali iliamua kuziunganisha shughuli za vijana na madhimisho ya
kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru pamoja na kumbukumbu ya kifo cha Baba wa
Taifa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1999. Amesema “maamuzi ya Serikali
yalizingatia haja ya kuendelea
kuenzi fikra za Baba wa Taifa za
kuutumia Mwenge wa Uhuru kama chombo maalum cha kuhamasisha amani na umoja,
kuondoa dhuluma, kukuza moyo wa kujitolea hasa kwa Vijana, na kuleta maendeleo
ya watu katika nchi yetu na nje ya mipaka yetu”.
Akiongelea
fursa watakazopata vijana katika wiki hiyo ya maonesho, Katibu Mkuu amesema
kuwa vijana watapata fursa ya kukutana, kuonyesha shughuli wanazozifanya na
kutathimini mchango wao katika kulijenga Taifa la Tanzania. Amesema kuwa vijana
wataweza kutumia wiki hiyo kutengeneza mitandao na kubadilishana uzoefu katika
masuala mbalimbali yanayohusu maisha yao ya kila siku.
Akielezea
shughuli za wiki ya vijana kitaifa, Sihaba amesema kuwa shughuli hizo
zimegawanyika katika sehemu tatu. Amezitaja sehemu hizo kuwa ni maonesho ya
shughuli mbalimbali zinazofanywa na vijana ambayo yatakuwa kwenye mabanda
maalum. Shughuli nyingine ni midahalo ya vijana, ambapo vijana watapata fursa
ya kujadili na kujifunza mambo mengi kupitia mada mbalimbali.
Mada hizo ni Ujue
Mkoa wa Iringa, Maudhui ya Wiki ya Vijana, Fursa za ajira kwa Vijana, Ushiriki
na ushirikishwaji wa Vijana katika maendeleo, Huduma ya hifadhi ya Jamii kwa
Vijana na Wajibu wa Vijana katika kutunza amani ya nchi. Shughuli ya mwisho ni
huduma ya kupima virusi vya ukimwi kwa hiyari itakayotolewa bure.
Washiriki
wa maonesho hayo ni vijana kutoka mikoa yote ya Tanznia Bara na Visiwani
kupitia kwenye vikundi vyao vya uzalishaji mali, makampuni na taasisi za vijana,
mashirika na idara za Serikali pamoja wadau mbalimbali wa maendeleo ya vijana
hapa nchini.
=30=
No comments:
Post a Comment