Thursday, February 13, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI TSHS.BILIONI 16 ZATUMIKA KUTEKELEZA ILANI YA CHAMA CHA MAPINDUZI JULAI – DESEMBA 2013





JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA

       Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,                            
                     S. L. P. 320,
                       Shinyanga

          10 Februari, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TSHS.BILIONI 16 ZATUMIKA KUTEKELEZA ILANI YA CHAMA CHA MAPINDUZI JULAI – DESEMBA 2013

Mkoa wa Shinyanga umetumia jumla ya Shilingi 16,097,445,854 kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kipindi cha Mwezi  Julai hadi Desemba Mwaka 2013.

Fedha hizo zimetumika katika sekta mbalimbali kama ilivyoainishwa katika maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya uchaguzi mkuu na malengo yaliyopangwa kutekelezwa kwa kipindi hicho.

Utekelezaji wa Ilani umezingatia malengo ya Mpango wa Matokeo Makubwa sasa na malengo ya maendeleo ya milenia hadi ifikapo 2015.

Katika kipindi cha nusu ya mwaka 2013/2014, mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta za Elimu,Afya,Maji,Kilimo,Miundombinu, Mapato ya Ndani ,Mifugo n.k. kama ifuatavyo:-

Mapato ya ndani
Hadi kufikia Desemba 2013 mkoa umekusanya mapato ya ndani kiasi cha Sh. 5,983,590,960 sawa na asilimia 47.3 ya Lengo kwani Mkoa umejiwekea Lengo la kukusanya kiasi cha Sh.11,356,021,186 kwa mwaka wa Fedha 2013/14.

Elimu
Kwa kipindi cha miezi sita,upande wa Elimu ya msingi,serikali imefanikiwa kuongeza madawati 1692, kusambaza vitabu 157,051 katika shule zote, kujenga nyumba za walimu 31 kujenga matundu ya vyoo 136 na madarasa 38 kwa Tshs 2,991,101,190 sawa na ongezeko la asilimia 40 ya mwaka jana 2012/2013. 

Aidha, madawati 459 kwa ajili ya madarasa ya awali yametengenezwa na ununuzi bado unaendelea,vilevile jumla ya watoto 3070 wenye ulemavu walimbuliwa na kuandikishwa katika Elimu ya Msingi.

Katika Elimu ya sekondari,Mkoa umetumia jumla ya Tshs. 1,348,013,030 kusambaza madawati, kujenga vyumba14 vya maabara na vifaa vya maabara hizo, kujenga maktaba na kununua vitabu 2975, kujenga nyumba za walimu 4, kujenga madarasa 17 na vyoo matundu 23.

Afya
Katika sekta ya Afya serikali imetumia kiasi cha Tsh.3,464,084,797 katika kuajiri watumishi 145 wa kada mbalimbali,kukarabati vituo vya Afya15,nyumba 11 za watumishi wa sekta ya Afya, ujenzi wa zahanati 40 unaendelea,ununuzi wa vifaa tiba,ujenzi wa hospitali ya wilaya unaoendelea, ununuzi wa gari moja la wagonjwa,usafirishaji wa wagonjwa 520 kwenda hospitali za rufaa, ujenzi wa jengo la OPD  na kufanya matengenezo ya magari yanayotumika kwa ajili ya ufuatiliaji na usimamizi wa huduma za Afya.

Maji
Tshs. 6,064,397,831 zimetumika katika kuboresha sekta ya maji kwa shughuli zifuatazo:- kujenga miradi ya maji ya visima virefu 17 ikiwa ni pamoja na kutandika mabomba na kufunga pampu za mikono kwenye visima virefu, mafunzo mbalimbali yamefanyika na vikundi vya maji 19 vilivyoundwa na kaya 115 kuhusu uvunaji wa maji ya mvua. 

Aidha vituo 42 vya kuchotea maji vimejengwa, mabirika 67 ya kunyweshea ng’ombe yamejengwa, visima vifupi 15 vimechimbwa sambamba na uchambaji wa mitaro ya kulaza mabomba.

Serikali ipo katika mchakato wa kupeleka huduma ya maji katika wilaya ya Kishapu kutoka bomba kuu la maji ya Ziwa Viktoria.Tayari michoro ya kupeleka maji imekamilika na kazi inayoendelea sasa ni kupata mkopo kwenye taasisi za fedha na pia kushirikiana na mgodi wa Almasi wa Mwadui.

Kilimo
Kiasi cha Tshs.1,557,687,000 zimetumika kufanikisha mapinduzi ya kilimo ikilinganishwa na tshs.907,664,635 zilizotumika mwaka 2012/2013 sawa na ongezeko la asilimia 58 ikilinganishwa na kipindi cha Januari hadi Juni 2013.Shughuli zilizofanyika katika kipindi hiki ni pamoja na ufuatiliaji wa mashamba darasa ya wakulima, ujenzi wa vituo vya rasilimali za kilimo, kuanzisha mashamba ya uzalishaji wa mbegu bora, kuongeza upatikanaji wa pembejeo, kununua vikatuzi nguvu yaani Power Tillers” 6, jumla ya vocha 8441 zimsambazwa, mbegu bora za mtama aina ya Macia zimesambazwa tani 12.7,kata 20 zimehamasishwa kulima mazao yanayostamili ukame,vyama vitatu vya SACCOS vimepewa mafunzo na zana za kilimo na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.

Ufugaji
Katika sekta ya ufugaji zimetumika shilingi 148,530,310 kutoa mafunzo ya ugani kwa wafugaji 3431,kujenga malambo matatu,na jumla ya mifugo 33,686 imepatiwa chanjo. Aidha, vikundi 38 vya wafugaji vimeundwa kufikia Desemba 2013.

Wanyamapori na Misitu
Tsh.4,656,000 zimetumika kuunda vikundi 7 vya mtandao wa ushirika wa ufugaji wa nyuki,mikutano ya hamasa juu ya kufuga kwa kutumia mizinga ya nyuki ya kisasa imefanyika katika kata 24, kuandaa na kutoa mizinga ya kisasa 1641 kwa ajili ya kujifunzia, kuendeleza msukumo katika ufugaji wa nyuki na kutoa Elimu kwa wafugaji nyuki.

Mkoa unaendelea na juhudi za kulinda na kuhifadhi mazingira ikiwa ni pamoja na kutunza vyanzo vya maji. Jumla ya miti 126,000 imeoteshwa na kupandwa na watu binafsi na shule za msingi.

Miundombinu
Kwa kipindi cha miezi sita,serikali imetumia shilingi 1,126,973,000 kufanya shughuli za kutoa hatimiliki za kimila na ugawaji wa ardhi.Matengenezo ya kawaida ya barabara katika sehemu korofi jumla ya km 539.52, usanifu wa ujenzi wa kiwango cha lamo wa km 15,uchimbaji wa mitaro ya maji ya mvua yenye ukubwa wa ujazo wa(cubic meter) 6100 matengenezo makalavati jumla ya mistari 21.

Aidha, uwanja wa ndege wa Ibadakuli upo kwenye mchakato wa kuboreshwa kwa kiwango cha lami kwenye njia ya ndege,kujenga ghorofa moja la abiria na maegesho ya magari madogo. Ujenzi huo utagharimu shilingi Bilioni 17 na tayari zabuni ya kumpata Mhandisi mshauri imetangazwa.

Utawala Bora
Ili kudumisha utawala bora wenye kufuata misingi ya haki na usawa, kiasi cha shilingi 197,045,196 zimetumika kuendesha vikao vya kamati za maendeleo ya kata, mabaraza ya wafanyakazi na mabaraza ya madiwani.

Ulinzi na Usalama
Hali ya ulinzi na usalama katika mkoa ni ya kurdhisha tofauti na kipindi cha nyuma kwani matukio makubwa ya uhalifu yamepungua,kwa kipindi cha Julai-Desemba,2013 mauaji ya Albino na yale yanayohusishwa na ushirikina yamepungua kwa asilimia 99 ikilinganishwa na asilimia 95 ya kipindi kilichopita.

Mkoa umewaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri kutenga fedha kwenye bajeti ya 2014/14 kwa ajili ya mgambo na ujenzi wa vituo vya polisi na Mahakama katika maeneo yao ya utawala ili kuimarisha haki, ulinzi na usalama.

Kuendeleza makundi maalum ya Wanawake,Watoto,Vijana na Walemavu

Katika kudumisha shughuli na ustawi wa makundi maalumu, shilingi 102,738,000 zimetumika kuimarisha mifuko ya uwezeshaji wa wanawake na kuhamasisha vyama vya kuweka na kukopa(SACCOS na VICOBA),vikundi 12 vya wanawake vimeelimishwa,vikundi 75 vimesajiliwa na kupewa mafunzo ya kuimarisha mifuko ya mikopo,vikundi 20 vya wanawake wajasiriamali vimewezeshwa kwa mikopo na kurejesha mikopo hiyo. 

Vilevile, Mkoa umesimamia Halmashauri kutoa michango ya asilimia 5 kwenye mfuko wa maendeleo ya wanawake.

Aidha, mkoa umefanya juhudi kubwa katika kuhakikisha kwamba haki za watoto zinasimamiwa ipasavyo kwa kutoa Elimu katika vijiji 32 kwa kushirikiana na mashirika ya Save the Children, AMREF na UMATI / JOICEF.

Vikundi 12 vya vijana wajasiriamali na ushirika wa kuweka na kukopa yaani SACCOS na VIKOBA vimeanzishwa na usimamizi wa matumizi ya fedha za maendeleo ya vijana umeimarishwa ili kuwanufaisha vijana wengi zaidi,na kuhakikisha asilimia 5 ya mfuko wa vijana inatengwa.

Kwa upande wa walemavu jumla ya shilingi 4,120,000 zimetumika kuwaendeleza pamoja na kuwaandikisha watoto wenye ulemavu na wenye uhitaji maalum. Watoto 3,070 wenye mahitaji maalum wametambuliwa na kuandikishwa darasa la kwanza.

Elimu ya ujasiriamali imetolewa kwenye vikundi 6 vya watu wenye ulemavu,pia walemavu wamewezeshwa katika maadhimisho ya sherehe zao za siku ya fimbo nyeupe, siku ya walemavu duniani na siku ya Albino.

Viwanda
Mkoa unaendelea na juhudi za kuendeleza viwanda pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji nje na ndani ya nchi yetu.Hadi Desemba 2013 hali halisi ya viwanda ilikuwa kama ifuatavyo:-
§  Kiwanda cha ngozi cha Xinghua Investment Co.Ltd kilikuwa kimekamilika hivyo mwekezaji alikuwa anatarajia kujaribu mitambo mwezi Januari 2014, kabla ya kuanza uzalishaji na mwezi huu Februari kimeanza uzalishaji.
§  Kiwanda cha nyama cha Xinghua Investment kinatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka huu 2014.
§  Mwekezaji Dahong Cotton Product Limited amekamilisha kiwanda cha kuchambua nyuzi za pamba klichopo Nhelegani.
§  Kiwanda cha kukamua mafuta ya kupikia ya pamba cha Jielong Holding (T)Ltd kilichopo Nhelegani pia kimekamilika.

Serikali ya mkoa wa Shinyanga inazidi kuwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na viongozi wao kuanzia ngazi za vijiji na mitaa,kata,tarafa na wilaya katika kuibua na kutatua changamoto zinazowakabili kwenye maeneo yao, na changamoto zinazohitaji ushauri wa ngazi ya mkoa zifike na zitaendelea kushugulikiwa.

Imetolewa na
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Shinyanga

No comments:

Post a Comment