Sunday, November 12, 2017

MKOA WA IRINGA WAADHIMISHA SIKU YA KISUKARI KWA MAZOEZI YA VIUNGO



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa- Iringa
Wananchi wa mkoa wa Iringa wametakiwa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara ili kuondokana na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa kisukari.

Kauli hiyo ilitolewa na mratibu wa Mkoa kwa magonjwa yasiyoambukizwa Dr. Tatu Mbotoni alipokuwa akielezea umuhimu wa mazoezi katika uwanja wa kumbukumbu ya Samora mjini Iringa katika mazoezi maalum ya viungo katika maadhimisho ya siku ya kisukari duniani jana.


Dr. Mbotoni alisema “mazoezi ya leo tarehe 11 Novemba, 2017 yamefanyika ngazi ya mkoa kuadhimisha siku ya kisukari duniani kwa mkoa wetu wa Iringa. Nichukue nafasi hii kuwataarifu kuwa tarehe 18 Novemba, 2017 tutafanya zoezi la upimaji wa afya hasa ugonjwa wa kisukari ikiwa ni maadhimisho ya siku ya kisukari duniani”

Alisema kuwa wananchi watatangaziwa eneo zoezi hili litakapofanyika baada ya taratibu za kiutawala kukamilika.

Alisema kuwa ugonjwa wa kisukari ni kati ya magonjwa yasiyoambukiza unaosababishwa na mfumo wa maisha usio wa kiafya. Mifumo hiyo aliitaja kuwa ni unene uliopitiliza na uzito mkubwa. 

Ni muhimu kufanya mazoezi ili kupunguza uzito na mafuta hatarishi mwilini vitu ambavyo visipothibitiwa vinaweza kusababisha ugonjwa wa kisukari” alisisitiza Dr. Mbotoni.

Mazoezi maalum ya viungo kwa mkoa wa Iringa yamefanyika kuadhimisha siku ya kisukari dunuani yakiongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Wanawake na kisukari, haki yetu ya afya bora ya baadae’. 

Mazoezi hayo yamehudhuriwa na mamia ya wakazi wa Manispaa ya Iringa na viunga vyake pamoja na watumishi kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi wakiongozwa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa.
=30=  

No comments:

Post a Comment