Saturday, February 10, 2018

IRINGA YAJIVUNIA HIFADHI YA TAIFA RUAHA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-Iringa

Mkoa wa Iringa unajivunia hifadhi kubwa ya taifa ya Ruaha yenye upekee unaovutia watalii wa ndani na nje ya nchi kuitembelea.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akisoma taarifa ya maendeleo ya Mkoa wa Iringa kwa Makamu wa Rais, mama Samia Suluhu Hassan jana katika rest house ya NSSF mjini Iringa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza

Masenza alisema kuwa Mkoa wa Iringa una hifadhi za taifa mbili hifadhi ya Taifa Ruaha na hifadhi ya Taifa ya Udzungwa. Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ina ukubwa wa Kilometa za mraba 20,226. 

“Asilimia 38 ya eneo la hifadhi ya Ruaha ambayo ni sawa na Kilometa za Mraba 777 zipo katika Mkoa wa Iringa. Hifadhi ya Ruaha ni kubwa kuliko hifadhi zote za Tanzania na ya pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya ile ya Kafue iliyopo nchini Zambia” alisema Masenza. Aliongeza kuwa upekee wa hifadhi hiyo ni uwepo wa mwingiliano wa bioanuwai za kusini na kaskazini mwa Tanzania.

Akiongelea hifadhi ya Taifa ya milima ya Udzungwa yenye ukubwa wa Kilometa za mraba 1,990 ambapo asilimia 80 sawa na Kilometa za mraba 1,596.8 za eneo lote la hifadhi ya Milima Udzungwa ipo katika Mkoa wa Iring alisema kuwa hifadhi hiyo ni hifadhi pekee iliyopo katika milima ya tao la mashariki. 

“Hifadhi hii ina hazina ya aina nyingi za mimea, ndege, vyura wa Kihansi na wanyamapori ambao hawapatikani katika sehemu nyingine yoyote duniani. Baadhi ya viumbe hao ni mbega mwekundu wa Iringa (Iringa red colobus monkey) na Sanje Crested mangabey” alisema Masenza.
=30=

No comments:

Post a Comment