Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Viongozi
mkoani Iringa wametakiwa kujipanga kuhakikisha maambukizi ya kifua kikuu
yanapungua ili wananchi waweze kutekeleza shughuli za maendeleo.
Kauli
hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza aliyekuwa mgeni rasmi
katika maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani yaliyofanyika ngazi ya mkoa
katika mji wa Ilula wilayani Kilolo hivi karibuni.
Masenza
alisema kuwa viongozi katika ngazi zao wanajukumu la kuhakikisha maambukizi ya
kifua kikuu yanapungua katika jamii inayowazunguka ili jamii hiyo iweze kufanya
kazi za kuzalisha mali. “Kwa hiyo katika
vikao vyote vitakavyofanyika katika maeneo yetu ya kazi, katika ngazi zote
kifua kikuu iwe ni agenda ili kuweza kupanga mikakati ya uboreshaji wa huduma
za kifua kikuu” alisema Masenza.
Aidha, alizitaka Halmashauri katika mkoa
wa Iringa kupanga na kufanya shughuli za uchunguzi wa dalili za kifua kikuu
katika makundi hatarishi. Aliyataja makundi hayo kuwa ni shule, magareza na
maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu.
Mkuu
wa mkoa alisema kuwa katika kuadhimisha juma la siku ya kifua kikuu duniani,
katika eneo la Ilula Sokini, huduma mbalimbali zilikuwa zikitolewa kwa wananchi
bila malipo. Huduma hizo alizitaja kuwa ni uchunguzi wa dalili za kifua kikuu
na matibabu, upimaji wa maambukizi ya VVU, uchunguzi wa saratani ya mlango wa
kizazi, uchangiaji na utoaji wa damu, huduma ya uzazi wa mpango, elimu kuhusu
lishe, na elimu kuhusu kifua kikuu.
Maadhimisho
ya siku ya kifua kikuu duniani yamefanyika ngazi ya mkoa katika mji wa Ilula
yakiongozwa na kaulimbiu isemayo ‘viongozi tuwe mstari wa mbele kuongoza
mapambano ya kutokomeza kifua kikuu’.
=30=