Saturday, April 28, 2018

Wafanyakazi Rasilimali Muhimu Uchumi wa Viwanda- Waziri Mwijage


Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Wafanyakazi ni rasilimali muhimu katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kukuza pato la nchi ikilinganishwa na rasirimali nyingine zote.

Kauli hiyo ilitolewa na waziri wa viwanda na biashara, Charles Mwijage alipokuwa akifungua kongamano la Tanzania ya viwanda lililofanyika katika ukumbi wa Kichangani mjini Iringa jana.

Waziri wa viwanda na biashara, Charles Mwijage

Waziri Mwijage alisema kuwa nchi ina rasilimali nyingi sana. Rasilimali muhimu aliitaja kuwa ni rasilimali wafanyakazi. Alisema kuwa wafanyakazi ni muhimu katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kukuza pato la taifa.

Akiongelea uchumi wa kati, waziri huyo alisema kuwa uchumi wa kati unategemea shughuli za watu katika kujenga viwanda vinavyochakata na kusindika malighafi za mazao ya shamba. 

Dhamira ya serikali ni kuhakikisha nchi inakuwa na sekta ya viwanda iliyo imara, shindani na endelevu. Alisema kuwa viwanda vinavyoongelewa siyo viwanda vya kufa kama binadamu, bali ikitokea vikafa, vinazaliwa vingine na kuendeleza nyororo wa thamani. Alisema kuwa watu wengi wamekuwa na mtazamo tofauti wa dhana ya kiwanda, alisisitiza kuwa mtu akiwa na cherehani nne hicho tayari ni kiwanda kidogo. Viwanda vidogo vinasaidia kupunguza kusafirisha mazao na hatari ya mazao hayo kuharibika wakati wa usafirishaji wake.

Waziri Mwijage alitoa wito kwa jamii kuwashawishi wafanyakazi kuanzisha viwanda tofauti na utaratibu wa sasa wa kukopa kwa ajili ya kununua magari. Aidha, alizitaka mamlaka za serikali za mitaa kutenga maeneo kwa ajili ya uanzishwaji wa viwanda. Alishauri viwanda vinavyoanzishwa viwe vinavyoongeza thamani.

Waziri Mwijage, alisema kuwa mipango iliyopo ni kuufanya uchumi ujikite katika maendeleo ya watu. “Uchumi tulionao ni wa maendeleo ya vitu zaidi kuliko maendeleo ya watu, hivyo tunataka kufanya mageuzi ya maendeleo ya watu ambayo yanapimwa kwa vitu vitatu”. Alivitaja vitu hivyo kuwa ni elimu, afya na kipato kitakachopatikana kutokana na uchumi wa viwanda.

Alisema kuwa serikali inajukumu la kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji.
=30=

No comments:

Post a Comment