Tuesday, July 26, 2016

WATUMISHI SERIKALI ZA MITAA WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA WAKURUGENZI WAPYA IRINGA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa watakiwa kutoa ushirikiano mzuri Wakurugenzi walioteuliwa hivi karibuni na Rais ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo alioikuwa akiongea na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo, mjini Iringa jana.


Jafo alisema kuwa ili Wakurugenzi waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo, ushirikiano baina ya watumishi na wakuu wa idara ni muhimu na kuwataka watumishi hao kuwapa ushirikiano mzuri Wakurugenzi hao wateule. “Wakurugenzi wapya hakikisheni mnatengeneza mtandao mzuri na wafanyakazi wote. Wapo baadhi ya watumishi kazi yao ni kutengeneza makundi ya fitna kwa Wakurugenzi ili wawachukie baadhi ya watumishi. Mkurugenzi ukikumbatia watumishi wa aina hiyo, basi watumishi hao watakupeleka mahali pabaya” aliongeza Jafo.


Kuhusu ukusanyaji wa mapato, Naibu Waziri alisema kuwa haridhishwi na ukusanyaji mapato hasa vijijini ambapo maeneo mengi hayatumii mfumo wa kieletroniki katika kukusanya mapato ya serikali. “Mapato ya ndani yanaathiriwa sana na mfumo dhaifu wa ukusanyaji mapato, ndiyo maana maelekezo ya serikali ni kutumia mfumo wa kieletroniki katika kukusanya mapato. Mapato ya ndani yasipokusanywa yanatuathiri sote na kushindwa kutekeleza majukumu yetu ikiwa ni pamoja na kwenda vijijini kwa wananchi kufanya kazi” aliongeza Jafo.

Alisema kuwa wapo baadhi ya watumishi wasio waadilifu ambao wametengeneza mfumo wa ulaji kupitia mfumo wa ukusanyaji mapato ya Halmashauri na kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuwa makini katika kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato ya serikali.

Naibu Waziri huyo, alisema “agenda ya Rais, John Magufuli ni mabadiliko ya kiuchumi, na wananchi wote wanataka mabadiliko ya kweli. Mabadiliko hayo lazima yaletwe na watumishi wa Halmashauri kwa kutimiza wajibu wao katika kufanya kazi. Kama sekta ya maji, afya, elimu, ujenzi na sekta nyingine hazitaenda sawa katika kutekeleza majukumu yake ni dhahiri kuwa wananchi watailalamikia serikali yao, malalamiko hayo yatatokana na baadhi ya watumishi wa Halmashauri kutotimiza wajibu wao”.

Alimshauri Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kupitia taarifa za kibenki za Halmashauri hiyo na kujiridhisha na mwenendo wa matumizi ya fedha za serikali kabla ya kuingia katika vikao vya Kamati ya fedha ili kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya fedha za serikali.
=30=

Sunday, February 7, 2016

MKUU WA MKOA ALIPOTEMBEA WAHANGA WA MAFURIKO WA MAPOGOROMkuu wa Mkoa wa Iringa


Hali ya barabara kuelekea Ruaha National Park



Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza (kushoto) akiongozwa na afisa Tarafa ya Idodi

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina masenza akisalimiana na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mapogoro Faustine Lova

Hali ya barabara iliyomeguliwa na maji




Tafakari ikiendelea


Baadhi ya nyumba zilizoharibiwa kabisa

Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Patrick Golwike








RC MASENZA AWATAKA WAKAZI 300 KUHAMA DHIDI YA MAFURIKO MAPOGORO



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wahanga wa mafuriko ya mto Mapogoro zaidi ya 300 wametakiwa kuhama katika nyumba zao kutokana na kupata unyevu kiwango cha kuhatarisha maisha yao.

Tahadhari hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipowatembelea wananchi wa Kijiji cha Mapogoro katika Tarafa ya Idodi wilayani Iringa walioathiriwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali wilayani Iringa.
 
Nyumba ya mwanakijiji iliyobomolewa na maji
Masenza alisema “nyumba zilizopata unyevu kutokana na mafuriko ya maji muhame, sitaki kusikia mwananchi hata mmoja amedondokewa na nyumba. Kutokana na nyumba nyingi kujengwa bila misingi na hata zinazojengwa kwa misingi, misingi hiyo inakuwa si imara hivyo hatari ya kudondoka nyumba inaweza kuwa kubwa katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha”. Kwa tathmini ya haraka kaya 137 katika kitongoji cha Kitanewa chenye wakazi zaidi ya 300 wanatakiwa kuhama ili kuepukana na kadhia ya mafuriko.   

Akiongelea sababu za mafuriko hayo, Masenza alisema kuwa miongoni mwa visababishi ni uharibifu wa mazingira. Alisema shughuli za kilimo pembezoni mwa kingo za mto na ukataji miti ovyo vinachangia mafuriko ya mara kwa mara maeneo yasiyotarajiwa. Aliwataka waheshimiwa madiwani na watendaji wa kata na vijiji kuwaelimisha wananchi dhidi ya athari ya uharibifu wa mazingira.

Mkuu wa mkoa aliwataka wazazi na wananchi kwa ujumja kuwalinda watoto dhidi ya hatari ya maji hayo. “Ndugu zangu lazima muwe waangalifu kwa watoto wasiende kwenye maji na kusombwa nawaomba sana” alisisitiza.  

Mafuriko hayo yalisababisha maafa ya kusombwa nyumba 14, hekari 717 katika vijiji vya Idodi, Mapogoro na Kitisi, eneo la banio la maji katika mfereji Mapogoro limefunikwa na mchanga na sehemu ya barabara kusombwa na maji na kusababisha magari ya upande mmoja kushindwa kuvuka kuelekea upande wa pili. Aidha, meneja wa Tanroads mkoa wa Iringa, mhandishi Daniel Kindole alisema kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha barabara iliyomegwa na maji inakarabatiwa na kuendelea kupitika kama kawaida. Aliongeza kuwa vifaa kazi zinaendelea kukusanywa ili kupelekwa eneo la tukio kurejesha hali ya kawaida.

Uongozi wa wilaya, mkoa na shirika la msalaba mwekundu wanaendelea ja jitihada za kutafuta mahema na chakula kwa ajili ya kuwasaidia watu ambao nyumba zao zilizolewa na chakula chao kuharibiwa na maji hayo.
=30=

Friday, January 1, 2016

TADB YATOA MIKOPO YA KILIMO IRINGA




Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa - IRINGA
Sekta ya kilimo ni muhimili wa uchumi nchini pamoja na kukabiliwa na changamoto nyingi katika ukuaji wake hasa upatikanaji mikopo.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza wakati wa utiaji saini makubaliano ya mikopo kati ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania na wakulima wadogo wadogo wa mkoa wa Iringa katika kijiji cha Igomaa wilayani Mufindi.
 
Mkuu wa Mkoa wa Irirnga, Amina Masenza
Masenza alisema “ikumbukwe kuwa umuhimu wa sekta ya kilimo unachagizwa na ukweli kuwa ni sekta ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wanaoishi vijijini, ambao wanategemea kilimo, ufugaji na uvuvi kwa ajili ya maisha yao. Kadhalika, wakulima, wafugaji na wavuvi wanatumia zana na mbinu duni katika shughuli zao, hivyo kushindwa kupata matokeo mazuri ya mazao”. Aliongeza kuwa pamoja na mchango mkubwa wa wakulima kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi, kwa mujibu wa takwimu zilizopo kuhusu hali za maisha ya wakulima nchini siyo ya kuvutia hata kidogo. Wengi mapato yao yapo chini na wanaishi maisha duni sana.

Lengo la serikali ya awamu ya tano ni kuimarisha sekta ya kilimo ili iweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa nchi na kuwanufaisha wakulima, wafugaji na wavuvi katika kuyabadilisha maisha yao  kwa kupitia mikopo na pembejeo za kisasa na mbegu bora zaidi. “Naamini ujio wa benki ya maendeleo ya kilimo (TADB) ni mwanzo tu wa maandalizi ya matokeo halisi ya ndoto na matamanio ya rais wetu, hivyo sina budi kuwapongeza na kuwaunga mkono katika hatua zote mnazozifanya katika kuwakopesha wakulima wadogo wadogo” alisisitiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Akiongelea changamoto iliyopo katika upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya kilimo katika taasisi za kifedha, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, alisema kuwa upatikanaji wa fedha ni mgumu kutokana na mikopo mingi kuelekezwa katika biashara za bidhaa na riba kubwa kwenye mikopo ya kilimo. Aliongeza kuwa masharti ya dhamana ni kikwazo kikubwa kwa wakulima wadogo wengi. Alisema kuwa kuanzishwa kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ni fursa kubwa kwa wakulima nchini.
=30= 

Monday, December 21, 2015

RC IRINGA AWATAKIA HERI MAJERUHI WA AJALI YA BASI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza amewatakia heri na kupona haraka majeruhi wote wa ajali ya basi ili waweze kuungana na familia zao na kuendelea na majukumu yao.

Kauli hiyo aliitoa muda mfupi baada ya kufanya ziara ya kustukiza katika hospitali ya rufaa ya Iringa kujionea jinsi majeruhi wa ajali ya basi la kampuni ya New Force wanavyohudumiwa hospitalini hapo.

Masenza akiyeambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Iringa alisema kuwa ajali hiyo imemuhuzunisha yeye binafsi na mkoa kwa ujumla. Alisema kuwa anawaombea kwa Mungu majeruhi wote kupata nafuu na kupona kabisa ili waweze kuendelea na majukumu yao ya ujenzi wa Taifa.

Akiongelea hali ya huduma hospitali hapo, Masenza alisema kuwa ameridhishwa na jinsi majeruhi wa ajali hiyo walivyopokelewa na kutibiwa hospitalini hapo. Aidha, aliwataka madaktari na wauguzi kuendelea kuonesha moyo wa huruma na uwajibikaji wanapowahudumia majeruhi wa ajali hiyo. Aidha, aliwahakikishia majeruhi hao kuwa serikali ipo pamoja nao kuhakikisha wanapata huduma bora ili wapone haraka na kuendelea na majukumu yao.

Ajali hiyo ilitokea kwa basi kugongana na lori ilitokea tarehe 18 Disemba, 2015 mchana baada ya tairi la lori lori namba T 616 DES la kampuni ya Ranfad Ltd kupasuka kupasuka na lori kukosa muelekeo na kuligonga basi la kampuni ya New Force namba T 483 CTF na kusababisha vifo vya abiria 12 na majeruhi 28. Miongoni mwa majeruhi hao, watatu ni raia wa Kongo DRC na mmoja raia wa Afrika Kusini.

=30=