Sunday, October 1, 2017

IRINGA KITOVU CHA UTALII KUCHOCHEA UCHUMI



Na Mwandishi Maalum, IRINGA
Mkoa wa Iringa uliteuliwa kuwa kitovu cha utalii kwa mikoa ya nyanda za juu kusini kwa maana ya kuwa kichocheo cha kukuza uchumi kwa ukanda wa kusini.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza katika salamu zake katika ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya utalii Duniani, maonesho ya Karibu Kusini na shughuli za viwanda vidogo (SIDO), yaliyofanyika katika uwanja wa kichangani Manispaa ya Iringa jana.

Mheshimiwa Masenza alisema kuwa mkoa wa Iringa uliteuliwa kuwa kitovu cha utalii kwa mikoa ya kusini na wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2002. Alisema katika mwaka huo maonesho ya Utalii Karibu Kusini yalifanyika kwa mara ya kwanza katika ukanda huo. 
Kwa msingi huo tupo hapa leo kuendeleza jitihada hizo za kuendeleza utalii. Lakini kwa kuwa serikali yetu inahimiza maendeleo ya viwanda, maonesho haya ya Utalii ya Karibu Kusini yanafanyika sambamba na maonesho ya shughuli za wajasiriamali (SIDO) katika kuenzi na kuendeleza maendeleo ya viwanda” alisema mheshimiwa Masenza.

Mkuu wa mkoa wa Iringa, alisema kuwa hulka ya sekta ya utalii, maendeleo yake yanategemea na sekta nyingine, “mikoa ya nyanda za juu kusini inatupasa kuendeleza sekta nyingine kama kilimo, ufugaji, usindikaji wa bidhaa mbalimbali, matumizi ya teknolojia bora na nafuu, uanzishwaji wa miradi mbalimbali ya utunzaji mazingira na kutafuta mitaji na masoko kwa ajili ya kukuza biashara ya utalii” alisema Masenza.

Aidha, aliahidi kuwa mkoa wake daima utakuwa mstari wa mbele kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa ya mfano na kukua kwa kasi.
Siku ya utalii Duniani, maonesho ya Utalii Karibu Kusini na shughuli za viwanda vidogo SIDO yanalenga kuelimisha umuhimu wa sekta ya utalii na viwanda kwa maendeleo ya wananchi wa mikoa ya kusini. 
=30=


IRINGA KITOVU CHA UTALII NYANDA ZA JUU KUSINI



Na Mwandishi Maalum, IRINGA
Mkoa wa Iringa ni kitovu kikuu cha kuendelea utalii kwa mikoa ya nyanda za juu kusini kwa mujibu wa mipango ya wizara ya Maliasili na Utalii ya kuendeleza utalii nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe wakati wa kufungua maadhimisho ya siku ya utalii Duniani, maonesho ya Karibu Kusini na maonesho ya shughuli za viwanda vidogo (SIDO) mjini Iringa jana.

Prof. Maghembe alisema “napenda kuchukua fursa hii kuendelea kuwakumbusha mipango yetu juu ya maendeleo ya utalii ukanda wa kusini. Kwa mujibu wa mpango kabambe wa kuendeleza utalii nchini wa mwaka 2002 (integrated Tourism Master Plan 2002), Iringa ni kituo kikuu (hub) ya maendeleo ya utalii ukanda wa kusini”. Aliongeza kuwa tayari juhudi za kufanikisha jambo hilovzinaendelea vizuri. 

Kupitia mradi resilient natural resources management for growth, pamoja na mambo mengine tunalenga kuimarisha miundombinu ya ndani ya hifadhi, kuboresha vivutio vya utalii, kuhamasisha uwekezaji wa biashara za utalii kuimarisha utangazaji, kujenga ofisi ya wizara ya kanda” alisema Prof. Maghembe.

Nae mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza alisema kuwa mkoa wake daima utakuwa mstari wa mbele kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa ya mfano na kukua kwa kasi.
=30=

SEKTA YA UTALII YAENDELEA KUKUA KILA MWAKA



Na Mwandishi Maalum, IRINGA
Sekta ya utalii imekuwa ikikuwa na kuchangia katika mapato ya Taifa zaidi ya dola za kimarekani milioni 2,000 mwaka 2016.

Kauli hiyo ilitolewa na waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe wakati wa kufungua maadhimisho ya siku ya utalii Duniani, maonesho ya Karibu Kusini na maonesho ya shughuli za viwanda vidogo (SIDO) mjini Iringa jana.

Prof. Maghembe alisema kuwa mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka dola za marekani milioni 1,353.29 mwaka 2011 hadi kufikia dola za marekani 2,131.57 mwaka 2016. “Mapato haya yamechangiwa na watalii wa kimataifa waliotembelea nchini ambao waliongezeka kutoka watalii 867,994 mwaka 2011 hadi kufikia watalii 1,284,279 kwa kipindi hicho. Takwimu zinaonesha kuwa sekta hii inachangia zaidi ya 11% ya ajira zote hapa nchini” alisema Prof. Maghembe.

Akiongelea mchango wa utalii katika ukuaji wa uchumi, waziri huyo alisema kuwa sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta zinazochangia sana ukuaji wa uchumi nchini. “Nyote mtakubaliana na mimi kwamba, utalii ni moja kati ya sekta inayochangia ukuaji wa uchumi nchini kutokana na kuwa chanzo cha kuliingizia Taifa fedha za kigeni. Utalii huongeza ajira na kipato kwa jamii, pia ni chachu kwa ukuaji wa sekta zingine. Sekta hii huchangia 25% ya mauzo nchi za nje.

Prof. Maghembe alisema kuwa ukuaji wa sekta ya utalii nchini unachangiwa kwa kiasi kikubwa na juhudi za serikali katika usimamizi, uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali, utangazaji, mazingira bora ya uwekezaji pamoja na ushirikiano madhubuti baina ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Nae mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza alisema kuwa mkoa wake daima utakuwa mstari wa mbele kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa ya mfano na kukua kwa kasi.
=30= 

Thursday, September 21, 2017

WADAU WAOMBWA MICHANGO KUFANIKISHA UTALII NA KAZI ZA VIWANDA VIDOGO



Na. Dennis Gondwe, IRINGA
Wadau wa maendeleo ya utalii mikoa ya nyanda za juu kusini wameombwa kuchangia maonesho ya Utalii Karibu Kunisi na shughuli za wajasiliamali wa viwanda ili yafanikiwe na kuchangia katika uchumi wa Taifa.

Ombi hilo lilitolewa na katibu msaidizi wa kamati ya maonesho ya utalii mkoa wa Iringa, Hawa Mwechaga alipokuwa akikabidhi stakabadhi ya malipo kwa mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Jackson Ngowi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa jana.

Mwechaga alisema “nichukue nafasi hii kwa niaba ya Katibu Tawala mkoa wa Iringa, kumshukuru Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kwa mchango wake wa shilingi milioni moja fedha taslimu katika kufanikisha maonesho ya Utalii Karibu Kusini na shughuli za wajasiliamali wa SIDO”. Alisema kuwa wadau wa utalii na biashara wana nafasi nzuri kuchangia katika kufanikisha maonesho hayo kwa sababu watafahamika na kukuza biashara na huduma wanazofanya.

Mwechaga alisema kuwa kupitia sekta ya utalii inayokuwa kwa kasi nchini, wadau wameweza kutangaza bidhaa na huduma wanazotoa na kuwafikia wananchi wengi zaidi. Lakini kupitia maonesho ya utalii wananchi wengi wameweza kupata maono mapya ya kufanya kazi za kiutalii na wengine kuboresha kazi walizokuwa wakifanya awali.

Maonesho ya Utalii Karibu Kusini mwaka 2017 yatafanyika mkoani Iringa kwa pamoja na maonesho ya shughuli za wajasiliamali wa viwanda vidogo (SIDO) yakihusisha mikoa ya nyanda za juu kusini katika uwanja wa Kichangani mjini Iringa kuanzia tarehe 27/9/2017 -02/10/2017.
=30=