Monday, March 26, 2018

Viongozi Iringa kupunguza Maambukizi ya Kifua Kikuu-RC Masenza



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Viongozi mkoani Iringa wametakiwa kujipanga kuhakikisha maambukizi ya kifua kikuu yanapungua ili wananchi waweze kutekeleza shughuli za maendeleo.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani yaliyofanyika ngazi ya mkoa katika mji wa Ilula wilayani Kilolo hivi karibuni.
 
Masenza alisema kuwa viongozi katika ngazi zao wanajukumu la kuhakikisha maambukizi ya kifua kikuu yanapungua katika jamii inayowazunguka ili jamii hiyo iweze kufanya kazi za kuzalisha mali. “Kwa hiyo katika vikao vyote vitakavyofanyika katika maeneo yetu ya kazi, katika ngazi zote kifua kikuu iwe ni agenda ili kuweza kupanga mikakati ya uboreshaji wa huduma za kifua kikuu” alisema Masenza. 

Aidha, alizitaka Halmashauri katika mkoa wa Iringa kupanga na kufanya shughuli za uchunguzi wa dalili za kifua kikuu katika makundi hatarishi. Aliyataja makundi hayo kuwa ni shule, magareza na maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu.

Mkuu wa mkoa alisema kuwa katika kuadhimisha juma la siku ya kifua kikuu duniani, katika eneo la Ilula Sokini, huduma mbalimbali zilikuwa zikitolewa kwa wananchi bila malipo. Huduma hizo alizitaja kuwa ni uchunguzi wa dalili za kifua kikuu na matibabu, upimaji wa maambukizi ya VVU, uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi, uchangiaji na utoaji wa damu, huduma ya uzazi wa mpango, elimu kuhusu lishe, na elimu kuhusu kifua kikuu.

Maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani yamefanyika ngazi ya mkoa katika mji wa Ilula yakiongozwa na kaulimbiu isemayo ‘viongozi tuwe mstari wa mbele kuongoza mapambano ya kutokomeza kifua kikuu’.
=30=

SERIKALI KUENDELEZA BIASHARA NDOGO- RC MASENZA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Serikali imeandaa mkakati wa kuendeleza biashara ndogo kwa lengo la kufikia uchumi unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua maonesho ya wajasiriamali wadogo na wa kati katika uwanja wa mashujaa mjini Mafinga jana.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza akikagua bidhaa katika Maonesho ya wajasiriamali mjini Mafinga

Masenza alisema kuwa katika nchini nyingi duniani, asilimia kubwa ya pato la watu binafsi linatokana na biashara ndogo na za kati. 

Hivyo kuendeleza sekta hii ni mkakati wa kutimiza  malengo ya dira ya maendeleo ya kuwa na uchumi imara unaotegemea  uzalishaji katika viwanda  ifikapo 2025” alisema Masenza. Aidha, aliwataka SIDO kuandaa mkakati wa kuwasaidia wajasiriamali waweze kupata masoko ya kudumu ndani na nje ya nchi.

Akiongelea changamoto ya uingizaji bidhaa kutoka nje, mkuu wa mkoa alisema kuwa uzalishaji wa bidhaa nyingi ndiyo suluhisho la kujitegemea kwa mkoa wa Iringa. Alisema kuwa uzalishaji huo utapunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi na kuongeza matumizi ya malighafi zinazozalishwa ndani kutumika katika viwanda vya ndani. 

Utaratibu huu utasaidia kulinda viwanda vyetu wenyewe bila kutegemea masoko ya nje tu kwa baadhi ya malighafi zetu” alisema mkuu wa mkoa.

Katika kipindi hiki chenye changamoto za kiuchumi duniani tujitahidi kuzalisha bidhaa kwa wingi na zenye ubora wa hali ya juu ili kuongeza ajira na pato la Taifa. Wananchi wote, wafanyabiashara na viongozi mliobahatika kutembelea maonesho haya, hii ni fursa nzuri ya kuweka miadi na kununua au kuchangia mawazo yenu katika kuboresha bidhaa zetu za hapa nchini, ili kusaidia kujenge msingi imara wa viwanda na uchumi wetu” alisisitiza mkuu wa mkoa.

Maonesho ya wajasiriamali kwa mkoa wa Iringa ni ya kwanza ya aina yake yaliyoandaliwa na T-LED, SIDO, TCCIA, TWCC  kwa kushirikiana na Halmashauri ya mji wa Mafinga.
=30=


MATUKIO KATIKA PICHA MAONESHO YA WAJASIRIAMALI MAFINGA


























Tuesday, February 27, 2018

WAKANDARASI UJENZI BARABARA WATAKIWA KUJIPANGA SAWASAWA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Serikali mkoani Iringa imewataka wakandarasi wa ujenzi wa miradi ya barabara kujipanga sawasawa katika kutekeleza miradi ya ujenzi ili idumu kwa muda mrefu.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake ya halfa ya utiaji saini mikataba baina ya TARURA na wakandarasi katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa Mkoa jana.
 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza
Masenza aliwataka wakandarasi wote walioshinda zabuni za ujenzi wa barabara katika Mkoa wa Iringa kujipanga sawasawa. “Serikali imewekeza pesa nyingi katika ujenzi wa barabara kwa lengo la kujenga na kuimarisha barabara ili mwananchi aweze kunufaika na barabara hizo. Tumesikia katika taarifa ya mratibu wa TARURA Mkoa wa Iringa kuwa gharama za ujenzi wa barabara ni shilingi bilioni 3.56” alisema Masenza. 

Aidha, alitumia hafla hiyo kuwataka wakandarasi wote kufanya kazi kwa kuzingatia muda uliopangwa na viwango vya ubora wa kazi. Serikali haitamvumilia mkandarasi yeyote atakayefanya kazi chini ya muda uliopangwa kwenye mkataba wala kazi iliyofanywa chini ya kiwango, aliongeza Masenza.

Katika kuhakikisha ubora wa kazi za ujenzi, mkuu wa mkoa wa Iringa aliwataka mameneja wa TARURA wa halmashauri kuwasimamia wakandarasi ili watekeleze majukumu yao. “Serikali imeajiri mameneja wa TARURA katika halmashauri. Jukumu kubwa la mameneja hawa ni kuwasimamia wakandarasi ili watekeleze wajibu wao. Hivyo, mameneja wa halmashauri pia mjipange sawasawa kuhakikisha ubora na thamani ya fedha inapatikana” alisisitiza mkuu wa mkoa.

Mkuu wa mkoa alitoa wito wa kulipwa kwa wakati pindi wakandarasi watakapotimiza wajibu wao kwa kuzingatia vigezo vya ubora kwa mujibu wa mikataba iliyosainiwa. Alisema kuwa kuna wakati malipo ya wakandarasi yamekuwa yakicheleweshwa kutokana na uzembe na kutofuata taratibu. “Utekelezaji huo utawafanya kuongeza morari ya kazi na pia kuondoa malalamiko yasiyo ya lazima kwa Serikali” alisema mkuu wa mkoa.

Awali mratibu wa TARURA Mkoa wa Iringa, mhandisi Juma Wambura katika taarifa yake alisema kuwa TARURA Mkoa wa Iringa ilitangaza miradi ya barabara za halmashauri zote za Mkoa jumla ya zabuni 26 zenye thamani ya shilingi bilioni 6.5. “Leo utaishuhudia mikataba 18 ikisainiwa na wazabuni walioshinda baada ya mchakato mzima wa manunuzi kukamilika yenye thamani ya shilingi bilioni 3.56. Mhe. mkuu wa mkoa, mikataba takribani 8 itasainiwa baadae baada ya taratibu za manunuzi kukamilika” alisema mhandisi Wambura.

Mratibu huyo alisema kuwa lengo la TARURA ni kufanikisha dhima kuu ya Serikali kuwa miundombinu ya barabara inaboreshwa na kusonga mbele kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi ili iweze kuboresha uchumi wa wananchi.

TARURA mkoa wa Iringa inahudumia mtandao wa barabara wenye jumla ya Kilomita 4,601.25 inayojumuisha halmashuri tano za Manispaa, halmashauri za wilaya za Iringa, Kilolo, Mufindi na Mji wa Mafinga.
=30=

MIKATABA 18 YA UJENZI WA BARABARA YASAINIWA IRINGA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Jumla ya mikataba 18 imesainiwa na wazabuni walioshinda zabuni yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3 mkoani Iringa.

Kauli hiyo ilitolewa na Mratibu wa Wakala wa Barabara za vijijini na mijini (TARURA) Mkoa wa Iringa, Mhandisi Juma Wambura katika taarifa fupi ya TARURA iliyowasilikswa kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hafla fupi ya utiaji saini mikataba ya ujenzi wa barabara na vivuko baina ya TARURA na wakandarasi katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Iringa jana.
 
Mhandisi Juma Wambura
Mhandisi Wambura alisema TARURA mkoa wa Iringa ilitangaza miradi ya barabara ya halmashauri zote za mkoa. 

Mhe. mkuu wa mkoa, TARURA Mkoa wa Iringa ilitangaza miradi ya barabara ya halmashauri zote za mkoa jumla ya zabuni 26 zenye thamani ya shilingi bilioni 6.5 ambayo leo utaishuhudia mikataba 18 ikisainiwa na wazabuni walioshinda baada ya mchakato mzima wa manunuzi kukamilika yenye thamani ya shilingi bilioni 3.56” alisema mhandisi Wambura. Alisema kuwa mikataba minane itasainiwa baada ya taratibu za manunuzi kukamilika.

Mratibu wa TARURA mkoa aliwaasa wazabuni hao kutekeleza miradi hiyo kwa weledi na ufanisi mkubwa pasipo kuchelewesha kama utaratibu wa miaka ya nyuma ulivyokuwa. 

Aidha, ninawakumbusha wazabuni kuacha mazoea ya kutekeleza kazi chini ya kiwango kwa visingizio mbalimbali. TARURA haitamvumilia mkandarasi yeyote atakayezembea katika utekelezaji wa miradi hii” alisema mratibu wa TARURA. Aliwahakikishia wakandarasi kupata ushirikiano unaostahili katika kutekeleza majukumu yao.

Wakala wa barabara za vijijini na mijini (TARURA) ulianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya wakala za serikali sura 245 na kutangazwa katika Gazeti la serikali Na. 211 la tarehe 12/05/2017.
=30=