KILIMO CHA MTAMA KIIMARISHWE
Viongozi wa Mkoa wa Iringa wameshauriwa kuweka juhudi za dhati katika kilimo cha mtama ili kukabiliana na baa la njaa linayoyakabili baadhi ya maeneo katika Wilaya za Iringa na Kilolo mkoani hapa.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Darry Rwegasira wakati akitoa uzoefu wa jinsi Wilaya ya Mpwapwa ilivyofanikiwa katika kilimo cha mtama na kukabiliana na baa la njaa.
Rwegasira amesema mapokeo ya viongozi ni jambo la msingi sana katika kufanikisha kilomo cha zao la mtama. Kwa upande wa Wilaya yake amesema “mapokeo ya viongozi wa Wilaya ya Mpwapwa ni mazuri sana ”. Amesema Wilayani kwake kuanzia Mkuu wa Wilaya, Madiwani, Afisa Kilimo, Katibu wa CCM na Maafisa Watendaji wanalima zao la mtama jambo linalowafanya wananchi kuona mfano na umuhimu wa kilimo hicho kutoka kwa viongozi wao.
Mkuu wa Wilaya amesema kuwa Wilaya ilitengeneza sheria mdogondogo zinazosimamia utekelezaji wa mkakati wa kilimo cha mtama Wilayani hapo. Aidha, alishauri kuwa nguvu kupindukia zisitumike badala yake uhamasishaji na elimu ndio msingi pekee wa kuwafanya wananchi kukubaliana na kilimo hicho na kwa kuangalia mifano kutoka kwa viongozi wao.
Vilevile, mkakati mwingine uliotumika ulikuwa ni uundaji wa timu na kamati kuanzia ngazi za kijiji hadi Wilaya zikiwahusisha wataalamu wa kilimo na viongozi.
Wilaya ya Mpwapwa ilichagua kata tisa za mfano na kila kijiji kilikuwa na wakulima 98 wanaotumika kama walimu wa kuwaelimisha wenzao.
Nae kiongozi wa timu iliyokwenda kujifunza kilimo cha mtama Wilayani Mpwapwa, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Asseri Msangi, amewashauri wakulima wa Wilaya ya Mpwapwa kutumza ardhi vizuri dhidi ya uharibifu unaotokana na mmea uitwao kidua. Amesema kutokana na hatari yam mea huo kwa ardhi na mazao Serikali ya kikoloni ilitunga Sheria ya 1946 kwa ajili ya kulinda ardhi dhidi ya kuharibika. Msangi amesema “tunzeni ardhi yenu vizuri, ardhi ni mali msipoitunza mtaumbuka”, “msipoitunza ikaharibika mtaenda wapi kwingine tumejaa”. Vilevile, amewashauri wataalamu wa kilimo kuwa watu wanaopenda mabadiliko na kwenda na wakati katika kuboresha na kuinua kilimo.
No comments:
Post a Comment