MGAWANYO WA RASILIMALI USIO HAKI CHANZO CHA KUVUNJIKA KWA AMANI NCHINI
Mgawanyo wa rasilimali za nchi usio usiozingatia usawa na haki ni miongoni mwa vyanzo vya kuvunjika kwa amani katika jamii.
Rai hiyo imetolewa na Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Fredrick Sumaye katika hotuba yake wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa kituo cha teknolojia ya Habari na mawasiliano (Orphanage ICT and School) kwa ajili ya watoto yatima mkoani Iringa iliyofanyika katika uwanja wa Samora mjini hapa.
Sumaye amesema “mgawanyiko wa mali usiozingatia usawa na haki na hasa utajiri unapojikusanya kwa wachache lazima amani itatoweka”. Amesema nchi ikiwa na matajiri sana na masikini wa kutisha hasa wakiwa ndio wezi sana amani hutoweka. Aidha, amesisitiza kuwa amani ni rasilimali kubwa kuliko zote katika taifa na pindi inapotoweka si rahisi kuirudisha.
Amesema kuwa ubaguzi na chokochoko za kiimani nazo huchangia uvunjifu wa amani. Amesisitiza kuwa “ubaguzi wa dini unapoota mizizi amani huyeyuka kama pande la barafu”.
Kuhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini amesema “uvumilivu wa vyama vya siasa ni jambo la msingi sana katika kulinda amani ya nchi”. Amesema ni lazima taifa lijifunze kujadiliana bila kupigana na kupingana kwa sera na hoja pasina kupigana na kuchochea uvunjifu wa amani.
Kwa upande wa rushwa na ufisadi, Waziri Mkuu mstaafu amesema “penye rushwa mwenye haki hunyimwa stahili yake na asiye na haki hununua haki ya mwingine”. Amesema kuwa rushwa hupofusha macho ya wanaoona na ni adui wa haki.
Awali akitoa taarifa fupi ya kituo hicho, Mratibu wa shirika la Children Care Development Organization (CCDO) Sixtus Kanyama amesema kuwa lengo kuu la shirika lake ni kuimarisha uwezo wa jamii katika kukuza elimu, afya na kutoa msaada wa kimaeneleo kwa jamii kupitia mafunzo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT). Amesema kituo hicho kitatoa mafunzo ya teknolojia kwa watoto kuanzia shule ya awali, msingi na sekondari na lugha za kigeni za kiingereza, kichina, kifaransa, kijerumani na kiarabu. Kituo hicho kwa kuanzia kinatarajiwa kugharimu shilingi milioni 120.
No comments:
Post a Comment