JENGENI UTAMADUNI WA KUPANDA MITI
Watanzania wametakiwa kuachana na utamaduni wa kupanda miti kwa mazoea hasa katika kipindi cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira kitaifa na kujenga utamaduni kwa kupanda miti mara kwa mara ili kujihakikishia mazingira salama ya kuishi.
Rai hiyo imetolewa na Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka katika hotuba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mizengo Pinda alipomuwakilisha kwenye kilele cha Maadhimisho ya wiki ya Mazingira Duniani yaliyofanyika kitaifa katika Mkoa wa Ruvuma , manispaa ya Songea.
Prof. Tibaijuka amesema “kupanda miti si fasheni bali ni kazi ya kudumu” hivyo utamaduni wa kupanda miti katika siku za maadhimisho hauna budi kuachwa na kufanya upandaji miti kuwa ni zoezi endelevu. Amesema mazingira ni sehemu ya maisha ya binadamu na uhai hivyo utunzaji wake ni jambo la lazima kwa kizazi hiki ili kijacho kiweze kujivunia hazina hiyo.
Amesema maadhimisho haya yanaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘panda miti na kuitunza ili kuhifadhi mazingira’. Kaulimbiu inawataka watanzania kukaa chini na kutafakari na kujipima kama hatua zinazostahili zimechukuliwa katika kulinda.
Aidha, amesema kuwa misitu husaidia sana upatikanaji wa mvua jambo linalotegemewa sana katika kilimo na shughuli nyingine za kijamii. Vilevile, amekemea tabia inayoendelea kukua ya utakaji miti na uchomaji wa mioto ovyo. Amesema “kupanda miti si kuboresha mazingira tu bali na kuongeza kipato tukokana na mazao ya misitu”.
Awali katika utangulizi wake, Dkt. Terezya Huvisa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira amesema kuwa Serikali kupitia Wizara yake imeandaa mkakati wa kuhifadhi mazingira uliojikita katika kuielimisha na kuihamasisha jamii juu ya umuhimu wa mazingira na uhifadhi wa uoto wa asili.
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ni matokeo ya azimio la umoja wa Mataifa la mwaka 1972, la Stockhorm –Sweden na kitaifa yalizinduliwa tarehe 1 Juni, 2011 katika kiwanja cha Majimaji kilichopo Manispaa na Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal. Maadhimisho yaha yamekwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuri wa Tanzania na miaka 47 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment