MAAFISA MICHEZO LAZIMA MUONEKANE
Maafisa Michezo wa Halmashauri wametakiwa kutoka na kushiriki katika shughuli zote za michezo katika Halmashauri zao ili kudhihirisha uwepo wao na kuinua kiwango cha michezo katika Mkoa wa Iringa.
Agizo hilo limetolewa na Kenneth Komba, Afisa Michezo Mkoa wa Iringa, wakati akizungumza katika kikao maalumu cha kuweka mikakati ya kufanikisha michezo ya Umoja wa Michezo na Sanaa Sekondari (UMISSETA) mkoani hapa kilichowakutanisha Wakuu wa Shule za Sekondari, Maafisa Elimu Taaluma Sekondari, Walimu wa Michezo na Afisa Michezo Mkoa muda mfupi baada ya kuzipokea timu za michezo mbalimbali ya UMISSETA kutoka katika Halmashauri nane za Mkoa wa Iringa uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari ya Mpeche Wilayani Njombe.
Komba amesema ili kuimarisha michezo yote katika Mkoa wa Iringa “ni lazima Maafisa Michezo wa Halmashauri watoke na kushiriki katika shughuli za michezo katika Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wengine wa michezo kwa sababu nyie ndio wataalamu katika tasmia ya michezo”. Aidha, amesisitiza ushirikishwaji wa Maafisa Michezo hao katika shughuli za michezo ili jamii iweze kunufaika na taaluma yao .
Komba ambaye pia ni Meneja wa timu ya UMISSETA ya Mkoa aliushukuru uongozi wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari (TAHOSSA) ngazi ya Wilaya na Mkoa kwa kujipanga na kufanikisha kuanza kwa mashindano ya UMISSETA mkoani hapa. Amesema kuwa TAHOSSA wamefanikisha kuanza kwa mashindano hayo kutokana na nguvu waliyonayo iliyojengeka katika misingi madhubuti ya umoja wao na kuheshimiana. Amesema jambo lolote la kimichezo haliwezi kukwama kwa namna yoyote ile hasa likiwa ni shirikishi kwa wadau na likifanyika kwa moyo wa umoja na mshikamano mkubwa.
Mwenyekiti wa TAHOSSA Mkoa wa Iringa, Andrew Kauta, amewataka walimu wote kusimamia kwa dhati suala la nidhamu kwa wanamichezo wote pasipo kujali mipaka ya Halmashauri au Wilaya zao na kusisitiza kuwa katika nidhamu hakuna mipaka. Aidha, amesisitiza kuwa michezo ni umoja, mshikamano na burudani hasa suala la nidhamu likidhibitiwa zaidi katika mavazi na matumizi ya lugha.
Vilevile, amewata walimu wa michezo kuwasilisha takwimu sahihi za wanamichezo na michezo wanayoshiriki kwa kila Halmashauri ili kuondokana na upotoshaji wa takwimu na usalama wa wanamichezo.
Lengo la msingi la mashindano haya ya UMISSETA ngazi ya Mkoa ni kushindanisha Wilaya sita na Halmashauri zake nane za Mkoa wa Iringa na hatimaye kupata timu moja ya Mkoa itakayokwenda kushiriki mashindano ya Kanda yanayotarajia kutimua vumbi Mkoani Ruvuma kuanzia tarehe 2 Juni, 2011.
Michezo ya UMISSETA inatarajia kuanza leo ngazi ya Mkoa katika Wilaya ya Njombe na inatarajia kushirikisha jumla ya wanamichezo 1088 katika michezo mbalimbali.
No comments:
Post a Comment