Tuesday, September 20, 2011

RC IRINGA AHAIDI USHIRIKIANO KUKUZA PATO LA MWANANCHI


Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma ameahidi kushirikiana na viongozi wa Mkoa huo ili kuinua pato la mwananchi wa chini kwa minajili ya kumuinua kiuchumi.

Kauli hiyo ameitoa ofisini kwake wakati akipokea taarifa ya makabidhiano ya Mkoa wa Iringa iliyowasilishwa kwake na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka.

Amesema “ni matumaini yangu kuwa tutakuwa bega kwa bega ili kuhakikisha mwananchi wa chini anainua uchumi wake yeye mwenyewe hasa kwa kuongeza pato lake”.

Dkt. Ishengoma ameitaja changamoto nyingine inayoukabili Mkoa wa Iringa kuwa ni ile ya maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI. Amesema Mkoa unachangamoto mahususi ya kuhakikisha inateremsha kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI kutoka asilimia 15.7 ya sasa  hadi kufikia angalau asilimia tano. Amesema kuwa japokuwa dawa ya ugonjwa huo bado haijapatikana ila wananchi wenyewe wanayo dawa ikiwa ni pamoja na kubadili tabia.

Aidha, amewataka viongozi wa Mkoa kuangalia maeneo yanayohitaji kufikishiwa zaidi elimu ya maambukizi ya UKIMWI ili kuweza kuinusuru jamii na janga hilo. Amesema kuwa ugonjwa huo ni lazima jitihada za kuudhibiti zifanyike ili kupunguza idadi ya yatima na wajane wanaotokana na matokeo ya ugonjwa huo.

Awali akiwasilisha taarifa ya makabidhiano ya Mkoa wa Iringa, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka amesema kuwa katika mwaka 2005 pato la Mkoa wa Iringa lilikuwa ni shilingi 867,482,000,000 huku Mkoa ukishika nafasi ya tano kitaifa. Aidha, pato la mkazi lilikuwa ni shinlingi 558,444 na Mkoa ulishika nafasi ya pili kitaifa.

Amesema katika mwaka 2010/2011 pato la Mkoa lilifikia Shilingi  1, 469, 720, 000,000 na pato la mkazi lilikuwa limeongeka kufikia Tshs 859,875 ambalo ni ongezeko la Shilingi 301,431 (54%).

Mpaka amesisitiza kuwa pato la Mkoa linaonekana ni kubwa lakini kwa kiasi kikubwa huchangiwa na mashamba makubwa ya chai, viwanda vya chai, misitu na viwanda vya mbao.

Upande wa Maambukizi ya UKIMWI Katibu Tawala huyo amesema kuwa Mwaka  2003/2004 maambukizi yalikuwa 13.4% na Mwaka 2010/11 maambukizi yamefikia 15.7%. Aidha, hadi Desemba, 2010/11 wananchi 74,632 wenye Virusi vya UKIMWI walioandikishwa kwenye Mpango wa Dawa za kupunguza makali.

Mkoa umekamilisha Mpango wa miaka minne 4 wa kupambana na tatizo la UKIMWI. Mpango huu ni kuanzia Oktoba 1998 hadi Septemba 2012.

No comments:

Post a Comment