Mkuu
wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma amekemea vikali wizi wa vifaa katika
ujenzi wa barabara unaoendelea katika maeneo mengi ya Mkoa wa Iringa na
kuwataka wananchi kuimarisha ulinzi shirikishi na kuwabaini wale wote wanaohusika
na uhalifu huo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Kauli
hiyo ameitoka katika kijiji cha Nyang’oro kilichopo katika Wilaya ya Iringa
alipotembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya Iringa-Dodoma kwa kiwango cha lami
na kuzungunza na wananchi wa maeneo yanayozunguka mradi huo.
Dkt.
Christine amesema kuwa Serikali ya awamu ya nne inatengeneza barabara kwa fedha
nyingi lengo likiwa ni kuharakisha kuwaletea maendeleo wananchi wake. Amesema
kuwa jitihada hizo za Serikali zimekuwa zikikwamishwa na baadhi ya watu wasio
na mapenzi mema na nchi niongoni mwao ni wananchi wanaozunguka ujenzi wa mradi
huo wa barabara kwa kufanya vitendo vya wizi wa mafuta na vifaa mbalimbali vya
ujenzi kama saruji. Amesema “wizi si kitu kizuri, wizi unaupa sifa mbaya mkoa
wetu na nchi yetu, ninyi wezi mnaonisikia tafadhali acheni wizi huo mara moja”
alisisitiza Dkt. Christine.
Amewataka
wananchi kufanya mikutano ya kuwabaini wezi hao ili waweze kufikishwa katika
vyombo vya dola na kusisitiza ulinzi shirikishi. Akionesha masikitiko yake na
kwa ukali alisema kuwa kama watafumbia macho vitendo hivyo ni dhahiri kwamba
ujenzi huo wa barabara utakapokamilika wezi hao watawaibia wananchi wenyewe.
Aidha,
amewataka vijana kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali kwa ajili ya
kufanya kazi za maendeleo. Amesema kwa kuwa mvua zinanyesha, ni vizuri vijana
hao wakajikita katika kilimo.
Akiwasilisha
taarifa ya utekelezaji mradi wa ujenzi wa barabara ya Iringa- Dodoma kwa
kiwango cha lami (Km 260) Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Iringa,
Mhandisi Bashiri Rwesingisa amesema kuwa mradi huo unaofadhiliwa kwa pamoja na
Benki ya Maendeleo ya Africa (ADB), Shirika la Misaada la Japan (JICA) na
Serikali ya Tanznaia umetekelezwa kwa asilimia 35 na muda uliotumika ni miezi
16 sawa na asilimia 47 ya muda wote wa utekelezaji wa mradi huo na Mkandarasi
yupo nyuma kwa miezi minne. Amesema ili kuongeza kasi ya utekelezaji, katika
sehemu ya kwanza ya (Lot 1) Iringa- Migori (Km 95.2) Mkandarasi anatumia timu
nne. Amezitaja timu hizo kuwa ya kwanza imeanzia Nyang’oro kuelekea Izazi, timu
ya pili imeanzia Izazi kuelekea Migori, timu ya tatu inafanya kazi ya kupasua
miamba eneo la mlima Nyang’oro wakati timu ya nne inafanya kazi kati ya
Nyang’oro na Igingilanyi.
Sehemu
ya pili (Lot 2) Migori- Fufu Escarpment (Km93.8) kiwango cha utekelezaji wake
hadi Septemba, 2012 kilikuwa wastani wa asilimia 40 wakati muda uliotumika ni
miezi 18 sawa na asilimia 50 na Mkandarasi yupo nyuma kwa miezi mitatu.
Aidha,
Sehemu (Lot 3) Fufu Escarpment – Dodoma (Km 70.9), amesema kuwa sehemu hiyo
inasimamiwa na Meneja wa Wakara wa barabara Mkoa wa Dodoma.
Akielezea
changamoto katika mradi huo, Mhandisi Rwesingisa amesema kuwa wizi wa vifaa vya
ujenzi kama mafuta na saruji umekuwa ukikwamisha maendeleo ya utekelezaji wa
miradi kwa kuwa Makandarasi wamekuwa wakitumia muda mwingi kujaribu kupambana
na wizi huo badala ya kutumia muda huo kufanya kazi za mradi. Changamoto
nyingine ameitaja kuwa ni migomo ya wafanyakazi wakidai nyongeza ya mishahara
na posho. Nyingine ameitaja kuwa ni upasuaji wa miamba yam awe mlima Nyang’oro
kwa ajili ya kupanua barabara umbali wa Km. 15 na ukosefu wa maji katika eneo
hilo.
=30=
No comments:
Post a Comment