Sunday, May 19, 2013



Serikali itaendelea kuwekeza katika kukuza mifumo ya kiteknolojia kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya watanzania na dunia kwa ujumla.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi wakati akifungua majadiliano ya kikanda ya ushirikiano wa manufaa kwa wote, yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo kikuu cha Ruaha.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Uratibu na Bunge William Lukuvi akihutubia mkutano huo
 
Lukuvi amesema “sote tunatarajia katika maendeleo ya nchi yetu na dunia kwa ujumla. Teknolojia huboresha tija kwa kubadilishana miundo ya mfumo wa uzalishaji kutoka mfumo mmoja na kuingia mifumo ambayo italeta ufanisi na manufaa zaidi katika shughuli za kiuchumi na kijamii”. Amesema “hapo awali Tanzania haikuwekeza sana katika mipango na kuweka utaratibu wa kuchagua, kujitwalia na kuhamisha teknolojia ambayo ingeingizwa kwenye teknolojia yetu kutokana na utafiti na maendeleo”. 

Aidha, amesema kuwa kwa sasa hatua za makusudi zinafanywa na Serikali kuhakikisha kuwa uhamishaji teknolojia unaenda kwa kasi na unakuwa endelevu ikiwa ni pamoja na kupitia mikutano na majadiliano ya ushirikiano wa manufaa kwa wote.  

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Uratibu na Bunge amesema kuwa lengo la majadiliano hayo ni kutoa fursa kwa viongozi wa Serikali ngazi zote kukutana na jumuiya mbalimbali za wananchi ili kujadiliana na kupata maoni kutoka kwa wananchi yatakayopelekwa kwa viongozi tofauti na utaratibu uliozoeleka wa viongozi kutoa maagizo. Akiongelea umuhimu wa ushirikishwaji wa wananchi, amesema kuwa uzoefu unaonesha kuwa wananchi wanaposhirikishwa kikamilifu katika kutoa maoni na wakawa na uelewa mzuri wa masuala yaliyoamuliwa, utekelezaji wake kuwa rahisi. Amesema kuwa ushirikishwaji huo utasaidia katika kutekeleza Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025 na Mipango ya Maendeleo ya miaka mitano.

Katika salamu za Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amesema kuwa majadiliano hayo yanamanufaa makubwa sana kwa mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya hivyo ni fursa nzuri kwa wadau hao wa maendeleo kujadili na kuainisha fursa za ushirikiano zilizopo na zinazohitajika kuboreshwa kwa manufaa ya wote. Amesema kuwa katika mkoa wa Iringa utaendelea kuboresha mazingira ya utoaji huduma katika kuharakisha mageuzi ya kiuchumi na kijamii katika mkoa. 

Majadiliano ya kikanda ya ushirikiano wa manufaa kwa wote yanafanyika katika kanda nane za Tanznaia Bara na mbili za Zanzibar. Katika kanda ya nyanda za juu kusini majadiliano hayo yamefanyika katika mkoa wa Iringa na kujumuisha mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya.

 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma akiusindikiza ujumbe wa Waziri Lukuvi
 
=30=

No comments:

Post a Comment