Na Tulizo
Kilaga
Wizara ya Maliasili na
Utalii imeanza mikutano ya mchakato wa kupokea maoni kutoka kwa watu na makundi
mbalimbali kuhusu uanzishwaji wa Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA).
Mkutano wa kwanza
umefanyika leo jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii
kampasi ya Bustani kwa kuanza kupokea maoni kutoka kwa viongozi waliowahi kuwa
mawaziri,makatibu wakuu na wakurugenzi wa wizara kuhusu uanzishwaji wa Mamlaka
hiyo.
Akizungumza kuhusu
hatua hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Khamis Kagasheki wakati
akifungua mkutano huo alisema Sheria ya Wanyamapori ya Mwaka 2009 inaitaka
Wizara kuanzisha Mamlaka ya Wanyamapori kazi ambayo itakamilika Novemba mwaka
huu.
Mhe. Waziri alisema
kuwa Wizara kwa kutambua umuhimu wa ushirikishwaji imeamua kuanza na viongozi
waliowahi kuitumikia Wizara ili waweze kutoa maoni juu ya Sheria na Muundo wa
Mamlaka ya Wanyamapori pamoja na Sheria ya Idara ya wanyamapori itakayobaki
katika Wizara.
“Nyalaka hizi
zimetengenezwa na watu wa ndani ya Wizara wenye uzoefu wa muda mrefu na hivyo
tumeona ni vizuri tuwashirikishe ninyi viongozi mliowahi kuitumikia Wizara ili
muweze kutoa michango yenu itakayotuwezesha kupata kitu bora kitakachopelekwa
katika Baraza la Mawaziri na kisha kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ili Bunge
la Novemba tuweze kuiwakilisha ikiwa ina baraka na maoni kutoka kwa kamati ya
Bunge ili ipitishwe kama Sheria ya Mamlaka ya Wanyamapori,” alisema Mhe.
Waziri.
Kuanzishwa kwa Mamlaka
ya Wanyamapori kutasaidia katika kurahisisha usimamizi wa rasilimali watu,
kujitegemea kimaamuzi, na kuwa na uwezo wakujiendesha yenyewe bila kutegemea
fedha kutoka hadhina.
Miongoni mwa mawaziri waliohudhuria
mchakato huo ni Mhe. George Kahama, Mhe. Getruda Mongella, Mhe. Ezekiel Maige,
Mhe. Dkt. Juma Ngasongwa, Mhe. Zabehi Mhita na Mhe. Arcado Ntegazwa.
Makatibu wakuu
waliofika ni Mhe. Philimon Luhanjo, Mhe. Marten Rumbanga, Mhe. Rose Lugembe, Mhe.
Balozi Dkt. Ladislaus Komba, Mhe. Alhaj Muhidin Ndolanga, Mhe. Salehe Pamba na waliowahi kuwa
wakurugenzi wa Idara ya Wanyamapori.
No comments:
Post a Comment