Serikali itaendelea kuwekeza katika
kukuza mifumo ya kiteknolojia kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya
watanzania na dunia kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi wakati
akifungua majadiliano ya kikanda ya ushirikiano wa manufaa kwa wote,
yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo kikuu cha Ruaha.
Lukuvi amesema “sote tunatarajia
katika maendeleo ya nchi yetu na dunia kwa ujumla. Teknolojia huboresha tija
kwa kubadilishana miundo ya mfumo wa uzalishaji kutoka mfumo mmoja na kuingia
mifumo ambayo italeta ufanisi na manufaa zaidi katika shughuli za kiuchumi na
kijamii”. Amesema “hapo awali Tanzania haikuwekeza sana katika mipango na
kuweka utaratibu wa kuchagua, kujitwalia na kuhamisha teknolojia ambayo
ingeingizwa kwenye teknolojia yetu kutokana na utafiti na maendeleo”.
Aidha,
amesema kuwa kwa sasa hatua za makusudi zinafanywa na Serikali kuhakikisha kuwa
uhamishaji teknolojia unaenda kwa kasi na unakuwa endelevu ikiwa ni pamoja na
kupitia mikutano na majadiliano ya ushirikiano wa manufaa kwa wote.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-
Sera, Uratibu na Bunge amesema kuwa lengo la majadiliano hayo ni kutoa fursa
kwa viongozi wa Serikali ngazi zote kukutana na jumuiya mbalimbali za wananchi
ili kujadiliana na kupata maoni kutoka kwa wananchi yatakayopelekwa kwa
viongozi tofauti na utaratibu uliozoeleka wa viongozi kutoa maagizo. Akiongelea
umuhimu wa ushirikishwaji wa wananchi, amesema kuwa uzoefu unaonesha kuwa
wananchi wanaposhirikishwa kikamilifu katika kutoa maoni na wakawa na uelewa
mzuri wa masuala yaliyoamuliwa, utekelezaji wake kuwa rahisi. Amesema kuwa
ushirikishwaji huo utasaidia katika kutekeleza Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025
na Mipango ya Maendeleo ya miaka mitano.
Katika salamu za Mkuu wa Mkoa wa
Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amesema kuwa majadiliano hayo yanamanufaa
makubwa sana kwa mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya hivyo ni fursa nzuri kwa
wadau hao wa maendeleo kujadili na kuainisha fursa za ushirikiano zilizopo na
zinazohitajika kuboreshwa kwa manufaa ya wote. Amesema kuwa katika mkoa wa
Iringa utaendelea kuboresha mazingira ya utoaji huduma katika kuharakisha
mageuzi ya kiuchumi na kijamii katika mkoa.
Majadiliano ya kikanda ya ushirikiano
wa manufaa kwa wote yanafanyika katika kanda nane za Tanznaia Bara na mbili za
Zanzibar. Katika kanda ya nyanda za juu kusini majadiliano hayo yamefanyika
katika mkoa wa Iringa na kujumuisha mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya.
=30=
No comments:
Post a Comment