Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma amekemea tabia
ya ulimaji kandokando ya mto Ruaha ili kukulinda na kuhifadhi mazingira na
vyanzo vya maji.
Kauli hiyo ameitoka katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake
na Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa Hamza Ginga ambaye ni diwani wa Kata ya
Kwakilosa katika kijiji cha Kiwere Wilayani Iringa.
Dkt. Christine amesema kuwa tatizo la ulimaji kandokando ya mto
Ruaha na mito mingine ni chanzo cha uharibifu wa mazingira. Amesema kuwa maeneo
ya kando kando ya mito katika wilaya zote mkoani Iringa yamevamiwa na watu
ambao wamekuwa wakilima hadi kwenye kingo za mito.amesema kuwa pamoja na kuwepo
kwa sheria zinazozuia ulimaji huo, bado utekelezaji wake ni hafifu. Aidha,
katika kudhibiti uharibifu huo amezitaka Halmashauri kuchukua hatua za kisheria
dhidi ya waharibifu hao.
Mkuu wa Mkoa ameziagiza Halmashauri na vijiji kuhakikisha
ulimaji kandokando ya mito na kwenye vyanzo vya maji unaachwa mara moja.
Amesema kuwa watu wanaolima kandokando ya mito na kwenye vyanzo vya maji na
maeneo mengine yaliyokatazwa kisheria wachukuliwe hatua za kisheria. Amesema
kuwa tabia ya ulimaji wa vinyungu umechangia sana kupunguza maji katika mito
kutokana na kupungua kwa akiba ya maji katika maeneo oevu. Amewataka wananchi
kuzingatia sheria ya maji ambayo mtu haruhusiwi kulima karibu na kingo za mito
katika umbali wa mita 100 kutoka kwenye kingo ya mto.
Dkt. Christine amewaagiza wananchi kuhakikisha kuwa miti
iliyopandwa inatunzwa na kuzuia moto kichaa kuchoma miti hiyo. Aidha, ameutaka
uongozi wa wilaya kusimamia kwa umakini na kuwachukulia hatua kali wale wote
watakaobainika kujihusisha na uchomaji moto miti. Amewataka wananchi kuwajibika
kuzuia misitu isiungue moto na kuhakikisha kuwa hakuna moto kichaa mahali
popote.
Akiongelea vyanzo vya maji, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema “vyanzo
vya maji ni urithi wa taifa kila mtanzania ana haki ya kufaidika na rasilimali
hii. Hivyo kila mtanzania ana wajibika kutunza vyanzo vya maji”. Amewataka wale
wote waliovamia vyanzo vya maji na kukata miti na kulima katika maeneo
hayo waondoke mara moja na Serikali za
vijiji ziwachukulie hatua wavamizi hao.
Siku ya mazingura duniani katika mkoa wa Iringa ilitanguliwa na
shughuli mbalimbali zikiwemo kutoa mafunzo maalumu kuhusu vyanzo vya maji na
elimu juu ya mpango wa usimamizi shirikishi wa misitu, kutoa elimu juu ya
madhara ya uharibifu wa mazingira, kufanya kampeni za kuzuia ulimaji kandokando
ya vyanzo vya majina kutengeneza barabara za moto kuzuia misitu ya asili na ya kupandwa
kuungua.
=30=