Kupungua kwa upendo baina ya wananchi ni
chanzo cha kuvunjika kwa amani nchini kutokana na watu kukosa hofu ya Mungu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa
Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alipokuwa akifungua mkutano wa kuzungumzia
mchango wa uislam katika kuleta amani Duniani ulioandaliwa na Jumuiya ya
waislamu wa Ahmadiyya Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo,
mjini Iringa.
Dkt. Christine amesema kuwa uvunjifu wa
amani nchini unatokana na kupungua kwa upendo baina ya wananchi. Amesema kuwa
watu wanapungukiwa upendo kwa sababu wanakosa hofu ya Mungu. Amesema “natumaini
kuwa wote tu mashaidi kuwa katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia au kusikia
matukio yasiyo ya kawaida ya ukiukaji na uvunjifu wa amani nchini katika maeneo
mbalimbali. Tumuombe Mwenyezi Mungu, apishe mbali, tuweze kudumisha amani na
utulivu kwa kila mmoja”.
Amesmea “matukio haya ni dalili mbaya kwa
nchi yetu ambayo waasisi wetu walitujengea misingi mizuri ya umoja, amani,
upendo na mshikamano wa kitaifa. Kutonaka na misingi hiyo ndiyo maana
watanzania hatuna ubaguzi katika misingi ya udini na ukabila. Misingi hii ni
mizuri na hatunabudi kuidumisha muda wote”.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi
kuhakikisha wanadumisha misingi ya amani iliyowekwa na waasisi wa Taifa kuanzia
kwa Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere. “Nawaomba sana ndugu zangu wa Mkoa wa
Iringa, kwa umoja wetu tuhakikishe tunasimamia na kudumisha misingi hiyo ili
kizazi cha sasa na kijacho kiweze kufurahia amani hii tuliyonayo. Tusikubali
kuyumbishwa na kuacha amani na utulivu ipotee” alisisitiza Dkt. Christine.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa amewataka viongozi wote kutikomeza vitendo
vinavyopelekea uvunjifu wa amani katika mkoa wa Iringa na Taifa kwa ujumla.
Amesema “ni wajibu wetu viongozi wa serikali na dini kuhakikisha tunatokomeza
kabisa vitendo vyote vinavyopelekea uvunjifu wa amani katika mkoa wetu wa
Iringa na nchi yetu kwa ujumla” Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Akiongelea mchango wa uislamu katika
kuleta amani duniani, Amir na mbashiri mkuu wa Jumuiya ya waislamu waahmadiyya
Tanznaia, Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry amesema kuwa uislamu maana yake ni
amani na utii hivyo ni kitu cha ajabu kuitumia dini kufundisha kinyume na
amani. Amesema kwa msingi huo, mwanadamu anatakiwa aishi kwa amani na muumba
wake, nafsi yake, wanadamu wenzake na viumbe wengine. Amesmea kuwa muislamu wa
kweli siku zote anakuwa ni mtu mnyenyekevu, mpole, mwenye huruma na anayejali
haki za kila mtu na kila kitu.
Sheikh Chaudhry amesema kuwa katika
kusisitiza amani, uislamu unafundisha udugu wa wanadamu wote na kuhimiza
uadilifu uliokamilika hata mbele ya maadui na kufundisha uhuru kamili wa
kuabudu.
Akiongelea sababu za kuvunjika kwa amani,
amezitaja sababu hizo kuwa ni sababu za kiuchumi, kijamii, kisiana na kidini. Amesema
kuwa miongoni mwa sababu hizo zote sababu za kidini ndizo zinazopelekea
uvunjifu mkubwa wa amani pamoja na kuwa zimeungana na sababu nyingine.
=30=
No comments:
Post a Comment