Monday, March 17, 2014

SERIKALI KUSIMAMIA UTUNZAJI VYANZO VYA MAJI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa 17/3/2014
SERIKALI mkoani Iringa imejizatiti kusimamia utunzani wa vyanzo vya maji na misitu kwa kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaokiuka na kuharibu vyanzo vya maji.
 
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akizindua maadhimisho ya wiki ya maji katika mkoa wa iringa katika kijiji cha Ihimbo wilayani Kilolo.

Wamoja amesema “serikali itachukua hatua stahiki kwa mtu au kikundi cha watu pale itakapobainika kwamba sheria ya utunzaji wa mazingira imekiukwa. Sheria ya mazingira ya mwaka 2002 inakataza shughuli yoyote ya kibinadamu umbali wa mita 60 kutoka ukingo wa mto”. Amewataka wananchi kuzingatia sheria hiyo muhimu ili kuweza kuepuka usumbufu wa kuchukuliwa hatua za kisheria na kuwezesha utunzaji wa rasilimali maji. 

Akiongelea kaulimbiu ya maadhimisho ya wiki ya maji isemayo uhakika wa upatikanaji wa maji na nishati, amesema kuwa serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kaulimbiu inatekelezwa kwa kulinda sheria mbalimbali za utunzaji wa vyanzo vya maji na misitu. Amesema kuwa kaulimbiu inakumbusha changamoto inayoukabili mkoa ikiwepo ya utunzaji wa vyanzo vya maji kama chemchem, mabwawa, mito na misitu.

Amesema kuwa utunzaji wa rasilimali hizo utauhakikishia mkoa upatikanaji wa maji na nishati. Amesema kuwa maji na nishati vinategemeana na maji yanatumika kama vyanzo vya kuzalisha nishati kama mojawapo ya nishati. Ameongeza kuwa maji hustawisha misitu inayozalisha nishati. Kwa msisitizo amesema kuwa uhakika wa maji na nishati unategemea sana utunzaji wa mazingira.
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa amewataka wananchi kudumisha jumuiya za watumia maji kama chombo cha kutunza miradi ya maji. 

Amesema “napenda kuwakumbusha kuwa serikali imejitoa katika kutunza na kuendesha miradi ya maji” amesisitiza Wamoja. Amesema kuwa ni jukumu la jamii nzima kuunga mkono jumuiya za maji zinazoundwa katika maeneo yao. Amewataka kutimiza wajibu kwa kutoa michango inayohitajika na waliyojipangia katika jumuiya zao.

Akiwasilisha taarifa ya hali ya upatikanaji huduma ya maji katika mkoa wa Iringa kwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya maji mkoani Iringa, Mhandishi wa Maji mkoa wa Iringa, Shaban Kitambulio Jellan amesema kuwa wananchi wanaopata huduma ya maji safi mijini katika mkoa wa Iringa ni 189,644 kati ya wananchi 247,156 ambayo ni sawa na asilimia 76.7 ya wananchi wote waishio mijini.

Aidha, hali ya huduma ya maji inategemewa kuongezeka mara baada ya kutekelezwa kwa miradi katika miji ya Ilula, Kilolo na Mafinga. Amesema kuwa miradi hiyo inategemewa kutekelezwa kupitia progrmu ya maendeleo ya sekta ya maji (WSDP) na wananchi wapatao 57,512 wanatarajiwa kupata huduma bora ya maji safi na salama.

Akiongelea ujenzi wa miradi ya matokeo makubwa sasa (BRN), Mhandishi Jellan amesema kuwa mkoa unajenga miradi 42 ya maji yenye kuleta matokeo makubwa sasa. Amesema kuwa miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Amesema kuwa mkoa wa Iringa unahitaji kiasi cha Tshs. Bilioni 11.582 kwa ajili ya kuwalipa makandarasi, wataalamu waelekezi na usimamizi na ufuatiliaji wa ujenzi wa miradi hiyo.
=30=

Sunday, March 16, 2014

MAN U 0-3 LIVERPOOL

STEVEN GERRARD & LUIS SUARES akunaga!

STEVEN GERRARD hakunaga!

STEVEN GERRARD hakunaga!

MARTIN & LUIS hakunaga!

ONGEZEKO LA WATU IRINGA WAONGEZA MAHITAJI YA ARDHI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Ongezeko kubwa la idadi ya watu katika manispaa ya Iringa linaenda sambamba na ongezeko la shughuli kuichumi hatimae kusababisha kuongezeka kwa mahitaji na matumizi ya ardhi.
 
Afisa Mipango Miji wa Manispaa ya Iringa, Immaculate Senje
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Mipango Miji wa Manispaa ya Iringa, Immaculate Senje alipokuwa akiwasilisha mada ya Mpango kamambe wa mji wa Iringa (Iringa Master Plan) 2015-2035 katika mkutano wa wadau wa maandalizi ya Mpango Kamambe wa Mji wa Iringa uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari ya Lugalo.

Senje amelitaja ongezeko la idadi ya watu katika mji wa Iringa linaloenda sambamba na ongezeko la shughuli za kiuchumi linasababisha kuongezeka kwa mahitaji na tumizi ya ardhi. Amesema ili kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya matumizi ya ardhi upo umuhimu wa kuwa na mwongozo unaotoa dira ya ukuaji wa mji ambao ni endelevu.

Akiongelea matumizi ya ardhi, Afisa Mipango Miji wa Manispaa ya Iringa amesema kuwa mji wa Iringa kama ilivyo miji mingine nchini unayo maeneo ya makazi yaliyopangwa na kupimwa pamoja nay ale yanayoenelezwa kiholela. Amesema kuwa eneo la makazi lililopangwa wakati wa ukoloni liko katika makundi matatu ambayo ni ujazo wa chini, ujazo wa kati na ujazo wa juu.

Akiongelea maeneo ambayo yameendelezwa kiholela, ameyataja maeneo hayo kuwa yanapatikana katika kata za Mwangata, Ruaha, Mkwawa, Mtwivila, Kihesa na Nduli. Amesema kuwa yapo maeneo ya vijiji vilivyoingia katika Manispaa siku za karibuni kama Kigonzile, Nduli, Mgongo, Mkoga na kitongoji cha Ulonge kuwa yana makazi yaliyotawanyika.

Akielezea matarajio yake baada ya mkutano, Senje amesema kuwa masuala muhimu, kero na changamoto zinazowakabili wakazi wa Iringa zitaibuliwa na kuwa msingi mkuu utakaoongoza uandaaji wa Mpango Kamambe utakaokidhi mahitaji ya wakazi wa Manispaa ya Iringa.
=30=

SERIKALI KUTENGENEZA MASTER PLAN KWA KUSHIRIKISHA WADAU



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Serikali imedhamiria kuona mji wa Iringa unakuwa na kuwa na maendeleo endelevu kwa ustawi wa kwa kuandaa mipango shirikishi kwa wananchi.
 
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita
Kauli hiyoimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa wadau wa maandalizi ya mpango kamambe wa mji wa Iringa (Iringa Master Plan) iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita.

Dkt. Ishengoma amesema “lengo kuu la kuandaa mpango kamambe ni kuwezesha ukuaji wa mji ambao ni endelevu katika Nyanja za kiafya, usalama, mpangilio mzuri, muonekano mzuri na ustawi wa jamii”. Amesema kuwa katika kufanikisha mpango huo, ushirikishaji mipango iliyopita na inayoendelea ya kisera katika ngazi mbalimbali za utendaji utazingatiwa.

Mkuu wa Mkoa amesema kuwa mpango kamambe husimamia uendeshaji wa mji kwa muda wa miaka 20. Amesema kuwa mpango huo unaweza kufanyiwa mapitio baada ya miaka mitano (5). Akiongelea umuhimu wa mpango amesema kuwa mpango hutoa mwongozo wa matumizi mbalimbali kwa ujumla kulingana na mahitaji ya jamii husika. Ameyataja matumizi hayo kuwa ni makazi, biashara, viwanda, kilimo, ufugaji na matumizi mengineyo.

Akiongelea Sheria ya Mipango Miji namba 8 ya mwaka 2007 na Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria nyinginezo, hifadhi ya mazingira husimamiwa na mamlaka ya upangaji kwa kushirikiana na wadau wa mji husika.
=30=

UCHAGUZI WA JIMBO LA KALENGA KUFANYIKA KWA AMANI NA UTULIVU



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa amewataka wananchi wa jimbo la Kalenga kujitokeza kwa wingi kupiga kura za kumchagua mbunge wa jimbo hilo.
 
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma
Kauli hiyo ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma ameitoa alipoongea na waandishi wa habari ofisini kwake kuelezea hali halisi katika jimbo la uchaguzi la Kalenga na kuwataka wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi kumchagua mbunge katika uchaguzi utakaofanyika tarehe 16/03/2014.

Akiongelea ulinzi na usalama, Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama katika Mkoa wa Iringa amewahakikishia wananchi kuwa ulinzi utakuwepo wa kutosha na vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kuhakikisha amani na usalama kwa wananchi katika kipindi chote cha kupiga kura na wakati wa kutoa matokeo.

Dkt. Ishengoma amesema kuwa maandalizi yamekamilika na vifaa vyote vinavyohitajika vimefika katika vituo vya kupigia kura. Amesema kuwa vituo vyote vitakuwa wazi kuanzia asubuhi hadi jioni kwa muda uliopangwa.
=30=