Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Uimarishaji wa mawasiliano baina ya
watendaji wa kata na maafisa tarafa umeelezwa kuwa ni nyenzo muhimu katika
utekelezaji wa kazi za serikali.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala
Msaidizi, Sehemu ya Menejimenti ya Serikali za Mitaa, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Iringa, Bw. Wilfred Myuyu alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu majukumu ya
watendaji wa kata katika usimamizi wa shughuli mbalimbali za maendeleo wilayani
Kilolo.
Bw. Myuyu amesema kuwa katika
kutekeleza majukumu, mtendaji wa kata anatakiwa kuwasiliana mara kwa mara na
afisa tarafa. Amesema kuwa kwa mujibu wa miongozo ya mawasiliano serikalini,
afisa tarafa anajukumu la kusimamia watendaji wa kata ili watekeleze majukumu
yao ipasavyo. Amesema kuwa kwa mujibu wa sheria ya Tawala za Mikoa Na. 19 ya
mwaka 1997 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2006 inaweka wazi kuwa majukumu ya
afisa tafara ni kusimamia shughuli za watendaji wa kata, vijiji na mitaa katika
eneo lake.
Akiongelea majukumu ya watendaji wa
kata katika ujenzi wa maabara unaoendelea, Bw. Myuyu amesema kuwa watendaji wa
kata wanawajibu wa kuwatambua wadau mbalimbali wa maendeleo wanaoweza kuchangia
na kuwahamasisha kwenye shughuli za ujenzi wa maabara ikiwa ni pamoja na
wananchi. Ameongeza kuwa wanalo jukumu la kufanya ufuatiliaji na tathmini ya
ujenzi unaoendelea ili kujiridhisha na uzingatiwaji wa viwango kusudiwa pamoja
na kasi ya ujenzi. Amesema kuwa katika ufuatiliaji huo wanalojukumu la kufahamu
changamoto zilizopo kushauri na kuzipatia ufumbuzi.
Jukumu linguine amelitaja kuwa ni
kuhakikisha michango inayotolewa na wananchi na wadau inatumika kwa kuzingatia
taratibu zinazoongoza matumizi ya fedha za umma na kutoa taarifa ya matumizi ya
fedha hizo kwa wananchi.
Bw. Myuyu ameongeza kuwa jukumu
lingine ni kutoa taarifa za maendeleo ya ujenzi wa maabara juu ya hatua za
utekelezaji zilizofikiwa, changamoto zilizopo na hatua za utatuzi wa
changamoto.
=30=