Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkuu
wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela ametakiwa kusimamia ulinzi na usalama
katika wilaya ya Iringa ili mkoa uwe salama katika kipindi cha kampeni kuelekea
uchaguzi mkuu.
Kauli
hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza muda mfupi baada ya
kumuapisha mkuu wa wilaya mteule wa Iringa katika ofisi ya mkuu wa mkoa leo.
Masenza
alisema “suala la ulinzi na usalama ni muhimu sana katika wilaya ya Iringa ili
mkoa uwe salama. Hivyo, lazima ulisimamie ipasavyo. Binafsi nina imani na wewe
na utendaji wako wa kazi hivyo hautashindwa katika kutekeleza majukumu yako”. Alisema
kuwa wilaya ya Iringa ikiwa salama wananchi wataendelea kushiriki katika
mampeni za kisiasa kwa uhuru na amani na hatimae kupiga kura salama.
Mkuu
wa mkoa alimtaarifu masuala ya kipaumbele kwa mkoa wa Iringa kuwa ni lishe,
ukimwi na usafi wa mazingira. Alimtaarifu kuwa katika ratiba yake ya kazi
lazima ijikite katika utekelezaji wa mpango mkakati wa mkoa unaolenga
kukabiliana na changamoto za lishe, hali ya maambukizi ya ukimwi na usafi wa
mazingira.
Katika
salamu za mkuu wa wilaya ya Iringa mteule Richard Kasesela alimshukuru Rais wa
Jamhuri kwa imani aliyonayo kwake. Aidha, alisema kuwa katika kipindi hiki
suala la amani ni agenda yake ya mwanzo kuelekea uchaguzi mkuu wa tarehe 25
Oktoba, 2015. Alisema kuwa yeyote katika wilaya ya Iringa atakayetishia watu
kwenda kupiga kura hasa wanawake atashughulikiwa. Alisema kuwa lazima wananchi
wote katika wilaya ya Iringa washiriki katika zoezi la kupiga kura kikamilifu
pasipo woga ili wafurahie haki yao ya kupiga kura kikatiba.
Akiongelea
masuala ya kimkakati katika mkoa, mkuu wa wilaya mteule alisema “nitajitahidi
kuhakikisha suala la lishe bora kwa wananchi hasa wanawake wajawazito na watoto
wachanga linaboreka katika wilaya ya Iringa na mkoa kwa ujumla. Tatizo hili
lazima liishe”.
Aidha,
suala la ukimwi aliahidi kukabiliana nalo ipasavyo. Alisema kuwa ngono zembe ni
jambo linalohitaji kuangaliwa kwa umakini zaidi. Wilaya itaangalia upya viashiria
vya ukimwi na mitego ili kuangalia jinsi ya kuitegua mitego hiyo hatimae
kupunguza maambukizi mapya. Akiongelea usafi wa mazingira alisema “mtu ni afya
hivyo usafi wa mazingira ni afya pia. Lazima usafi wa mazingira uanzie kwa mtu
mwenyewe katika mazingira ya nyumbani kwake na mazingira yanayomzunguka”.
Mkuu wa wilaya ya Iringa aliapishwa leo mjini
Iringa kufuatia uteuzi wa Rais wa wakuu wapya wa wilaya 13 na kuhamishwa kwa
wakuu saba wa wilaya tarehe 4/10/2015.
=30=
No comments:
Post a Comment