Tuesday, October 20, 2015

NEC YAVITAKA VYAMA KUELIMISHA WANANCHI TARATIBU ZA UCHAGUZI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imevitaka vyama vya siasa nchini kuwaelimisha wananchi kufuata taratibu ili kufanikisha uchaguzi huru na salama nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na Kamishna wa Tume hiyo Jaji Mary Longway alipokuwa akifungua mkutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na viongozi wa vyama vya siasa mkoani Iringa.
 
Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Mstaafu) Mary Longway akifungua mkutano
Jaji Longway alisema “vyama vya siasa vina nafasi kubwa katika kuelimisha na kuhamasisha jamii, Tume inaamini kwamba ili mpiga kura aweze kufanya maamuzi sahihi ni muhimu kwake kupata elimu sahihi. Hivyo basi, Tume inatarajia kuona mkitumia majukwaa yenu vema katika kuhamasisha na kuelimisha si tu wananchi wenu bali jamii ya watanzania”. 

Alisema kuwa kuelekea uchaguzi mkuu, Tume imeandaa vituo vya kupigia kura 64,736. Tanzania bara vituo 63,156 na Zanzibar vituo 1,580. Aliongeza kuwa kila kituo kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wapiga kura 450 na wasizidi 500. “Hata hivyo kituo kinapokuwa na wapiga kura zaidi ya 500 kinabidi kigawanywe ili viwe viwili yaani kituo “A” na “B” na namba ya wapiga kura itakuwa nusu kwa nusu. Mnaombwa kuwahamasisha wapiga kura wanashauriwa kwenda katika vituo walivyojiandikishia kupiga kura siku nane kabla ya siku ya kupiga kura ili kuweza kujua vituo vyao halisi vya kupigia kura” alisisitiza Jaji Longway.

Kamishna Longway alisema kuwa Tume imekuwa ikisikitishwa na baadhi ya vyama vya siasa kutumia majukwaa vibaya wakati wa kampeni. “Tume kwa namna ya pekee inawaomba katika kipindi hiki kifupi kilichobaki kutumia nafasi zenu majukwaani kuelezea sera za vyama vyenu ili kuweza kuwasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi baada ya kuwa na taarifa sahihi”. 

Tume imekuwa ikisikia katika vyombo vya habari malalamiko juu ya uvunjifu wa maadili ya uchaguzi katika kipindi hiki cha kampeni, “nitumie nafasi hii kuwaasa viongozi wa vyama vya siasa kupeleka malalamiko yenu katika kamati za maadili na si kukimbilia katika vyombo vya habarir kama ambavyo baadhi ya vyama vya siasa na wagombea mmekuwa mkifanya”.
Viongozi wa Vyama vya Siasa Mkoa wa Iringa

Ndani ya ukumbi wa Siasa ni Kilimo

Aidha, aliwataka kuepuka kutoa taarifa na shutuma zisizo sahihi kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kujikita katika kufikisha taarifa zilizo sahihi na zilizokusudiwa kwa wafuasi na wananchi kwa ujumla na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kushiriki katika uchaguzi mkuu tarehe 25 Oktoba, 2015.
=30=

No comments:

Post a Comment