Na. Mwandishi Maalumu, Iringa
Wataalam
mkoani hapa wametakiwa kujikita katika kutafuta mbinu za kuwasaidia wanufaika
wa mpango wa kunusuru kaya masikini Tasaf III ili wajikwamue katika lindi la
umasikini.
Agizo
hilo lilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa
akifungua kikao kazi cha wataalam wa wilaya na mkoa wa Iringa cha kupanga
mikakati ya jinsi ya kuzisaidia kaya masikini zinazonufaika na ruzuku ya Tasaf
kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Bonde la Rufiji mjini Iringa.
Ayubu
alisema “lengo la kikao kazi hiki ni
kuwashirikisha ninyi wataalam wa sekta za afya, elimu, kilimo, mifugo,
maendeleo ya jamii na ushirika ambazo kwa kiasi kikubwa zimeguswa na walengwa
wa mpango huu wa Tasaf. Mnafahamu kuwa walengwa wengi wa Tasaf wapo vijijini na
wameanzisha miradi midogomidogo ya ufugaji wa kuku, bata, simbilisi, nguruwe,
mbuzi na kondoo.
Aidha, wengine wanaboresha makazi yao, wote hawa wanahitaji
msaada na ushauri wa kitaalam na ufuatiliaji wa karibu”. Aliongeza kuwa
wataalam wa serikali wanawajibu wa kuwasaidia na kuwaelekeza wanufaika hao
kuweza kufikia malengo yao. Aliwataka kuona kuwa kuwasaidia wanufaika hao ni
jukumu lao na kuwataka kuweka katika mpango kazi wao na ratiba ya kazi ya kila
mwezi.
Akiongelea
wanufaika wanaopata ruzuku yenye masharti ya elimu na afya, Katibu Tawala Mkoa
aliwataka kuwasimamia walengwa ili watimize masharti hayo. “Mfano, upande wa afya mlengwa atapata ruzuku
kama ametimiza sharti la kupeleka mtoto kliniki aliye chini ya umri wa miaka
mitano. Kwa upande wa elimu mlengwa atapata ruzuku kama atahakikisha mtoto wake
anahudhuria shuleni siyo chini ya asilimia 80 ya mahudhurio yanayohitajika”
alisisitiza Ayubu. Ni jukumu la kikao kazi hiki kujadili na kupanga namna bora
ya kufanya ufuatiliaji wa karibu na kutoa ushauri kwa walengwa ili malengo ya
serikali ya kupunguza umasikini yaweze kutimia.
Awali
Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Iringa, William Kingazi alimtaarifu Katibu Tawala Mkoa
kuwa mkoa wa Iringa ulipata fedha kupitia mpango wa Tasaf III kwa ajili ya
kuziwezesha kaya masikini sana ili ziweze kujikimu. Mpango huo ulianza mwezi
Januari, 2015 ambapo kaya 26,321 zilitambuliwa kuwa masikini sana. Hadi kufikia
mwezi Septemba, 2016 mkoa ulipokea shilingi 6,525,080,001.
=30=